Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Willy Isangula afariki Dunia

Bondia Pic Willy Isangula Willy Isangula.

Fri, 9 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bondia mkongwe, Willy Isangula amefariki dunia jana asubuhi, baada ya kuugua kwa zaidi ya miaka minane. Msiba wa bondia huyo aliyewahi kuiletea nchi medali ya Afrika mwaka 1987 uko Kigamboni Kisiwani, Dar es Salaam.

Akizungumza nasi, mtoto wa marehemu, Joseph Isangula amesema baba yake aliugua kwa zaidi ya miaka minane.

“Alipooza kwa muda mrefu, ikasababisha akawa hatembei kabisa, aliendelea na matibabu lakini hivi karibuni alizidiwa tukampeleka hospitali hadi leo asubuhi alipofariki akiwa anapatiwa matibabu Hospitali ya Muhimbili,” amesema kijana huyo.

Amesema taratibu za mazishi bado zinapangwa na familia, baada ya kikao ndipo watajua ni lini na wapi baba yao atazikwa.

Isangula aliyekuwa na umbo pana na mrefu kwa kimo, alikuwa miongoni mwa nyota walioweka rekodi ya kuiletea nchi medali nyingi kwenye michezo ya Afrika ya mwaka 1987 nchini Kenya, akiwa na timu ya Taifa ya ngumi.

Katika michezo hiyo iliyofanyika Kenya, Tanzania ilimaliza nafasi ya 12 kwenye matokeo ya jumla na kuweka rekodi ya kutwaa medali saba kwenye riadha na ngumi, rekodi ambayo haijawahi kuvunjwa hadi sasa.

Miongoni mwa medali hizo ilikuwa ya Willy Isangula, bondia wa uzani wa juu, huku mabondia wengine waliotwaa medali wakiwa ni Benjamin Mwangata (fedha), Nassor Michael na Rajabu Hussein wakishinda shaba.

Medali nyingine zilikuwa za riadha za Zakayo Malekwa (fedha – kurusha mkuki), Nata Nangae (shaba – mbio za mita 3,000) Matilda Kisava (sasa marehemu) alishinda medali ya shaba ya kurusha mkuki.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live