Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Warembo wanaosumbuka na vitambi nitawasaidia

Jesca Warembo Warembo wanaosumbuka na vitambi nitawasaidia

Tue, 9 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Bondia wa kike Jesca Mfinanga (22) anayepigana katika uzani wa kilo 52 anapenda kutofautisha fani hiyo na maisha mengine ya nje, ili kuwafanya mabinti wasiuogope mchezo huo.

Katika mahojiano yake na Spoti Mikiki, Jesca anasema kitu wasichokijua watu kutoka kwake, ni kwamba anapenda sana urembo na kujishughulisha na biashara za hapa na pale ili asitegemee ngumi pekee kumpatia kipato.

Anasema ngumi si kigezo cha kumfanya ajiweke katika muonekano wa kiume na pia hujisikia vibaya anapoona watu mtaani wakiwaita majina mabaya wanawake. Anasema ameamua kuishi kwa kujipenda ili asiogopeshe mabinti wengine wanaoupenda mchezo huo.

“Napenda kupambana kujenga uchumi wangu, ili niweze kujisimamia mwenyewe kiuchumi na kuwasaidia ndugu, jamaa na marafiki, sasa mtu asije akanichukulia kama nataka niwe na muonekano wa kiume, nasisitiza mimi ni mrembo kabisa,” anasema na kuongeza;

“Kabla ya kujikita kwenye ngumi, nilianza na mambo ya kuigiza, ila nilikuwa napenda niigize filamu za kupigana, baba yangu mlezi Japhet Kaseba akaniunganisha na baadhi ya wasanii, lakini akataka anifundishe ngumi ili nikiigiza nisifanye mchezo.

“Nikaanza kufanya mazoezi ya ngumi, nikajikuta naangukia kuupenda mchezo huo, ambao bondia akizingatia mazoezi vizuri hawezi kuzeeka mapema.”

Jesca ambaye hakufika mwisho kusomea uandishi wa habari, anasema shughuli nyingine anayofanya ni kuwafundisha watu binafsi mazoezi ya kuondoa vitambi na unene, hivyo anajikuta muda mwingi anautumia kwenye kazi zake.

“Wale warembo ambao hawataki matumbo makubwa, nyama uzembe na kupunguza uzito mkubwa, basi hizo mishe nazipiga, nitawasaidia kuwa na mwili wa kuonekana kiurembo kabisa,” anasema.

UKAKAMAVU

Anasema anafanya mazoezi kwa siku mara mbili na akiwa na pambano anajifua mara tatu, na anapokuwa kwenye siku zake za mwezi anasema: “Najikaza siwezi kujibweteka, nikiona tumbo linaniuma sana, napumzika saa kadhaa kisha namwambia kocha ukweli, anakuwa anajua mazoezi gani anifanyishe kwa nyakati hizo.”

Anaongeza: “Mchezo huu unahitaji nidhamu ya hali ya juu, nikiwa na pambano naelekezwa na kocha namna ya kujitunza, ndio maana nashukuru kupata mpenzi anayeelewa kazi zangu, ili nikihitaji muda wa kujiweka fiti anakuwa anaelewa nini nakimaanisha.”

Anasema siku anazokuwa huru, mpenzi wake anampa muda wa kufurahi naye. “Nikipata muda wa kufurahi naye nafurahia, napika, nafua, nafanya kazi zote za nyumbani kama binti wa aina yoyote.”

Mbali na hilo, anataja vitu vya kuzingatia kwenye mchezo huo, kwamba ni vifaa vya kujikinga kuwa salama wakati wa mazoezi na mchezo wenyewe.

“Vifaa ni kila kitu, vinginevyo inakuwa ngumu kwa mtoto wa kike kuweza kuhimili,” anasema Jesca ambaye alijiunga na mchezo huo 2019.

Anasema maeneo hatari kwa mtoto wa kike ambayo anapaswa kuwa mwangalifu na kujikinga akiwa ulingoni ni kifuani, ambapo makocha wanawaelekeza namna ya kuwa waangalifu.

“Kwanza huo ni mchezo siyo vita, ingawa wakati wa kuwania ubingwa hakuna kucheza pale zinakuwa ngumi kweli kweli, lakini hakuna bondia anayetamani mwenzake apoteze maisha ulingoni hayupo kabisa, kwanza tunafundishwa kuhusu utu, hivyo ngumi ni burudani kama michezo mingine,” anasema.

Anazungumzia pambano alilopoteza hivi karibuni kwa pointi dhidi ya mpinzani wake Sara Alex kutoka Arusha kwamba, anakubaliana na matokeo anajipanga upya, anaamini awamu nyingine itakuwa ya kicheko kwake.

“Kwanza amefanya nipate nguvu ya kufanya mazoezi zaidi, naahidi siku nikirudiana naye atasimulia, kwa sasa yeye namwacha atambe kwani hata mimi ningeshinda ningetamba.”

Chanzo: Mwanaspoti