Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadau wa ngumi wamlilia Ustaadh

F6577621bdc4b2e8b60ee7a9245db54e Wadau wa ngumi wamlilia Ustaadh

Wed, 9 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WADAU wa ngumi nchini wamesema kifo cha Yassin Abdallah ‘Ustaadh’ ni pigo katika ngumi na watamkumbuka kwa mengi aliyofanya enzi za uhai wake. Yassin Abdallah alifariki dunia juzi na kuzikwa jana katika makaburi ya Buza, Dar es Salaam.

Miongoni mwa wadau hao ni bondia wa zamani na Mwenyekiti wa Chama cha waamuzi wa ngumi za kulipwa, Ally Bakari ‘Champion’ aliyekuwa akifanya kazi na Ustaadh enzi za uhai wake.

“Ustaadh alikuwa ni mpambanaji na alikipigania chama cha waamuzi kama mjumbe wa Kamati ya Utendaji hadi tukasimama imara, hakika tutamkumbuka na tumepata pigo kubwa,” alisema huku akiwapa pole familia ya marehemu na kuwahimiza kuwa na moyo wa uvumilivu.

Pia alisema Ustaadh ndiye aliyemrejesha kwenye sekta hiyo baada ya kujitoa mwanzoni kutokana na migogoro. “Nakumbuka nilikuwa nimeacha ngumi kutokana na migogoro iliyokuwepo huko nyuma, lakini alinifuata akaniambia nirudi tuendeleze kwa pamoja,” alisema.

Promota Ally Mwazoa alisema atakumbuka mambo mengi kutoka kwa Ustaadh na namna alivyokuwa na msimamo tangu ilivyokuwa kwenye wakati mgumu miaka ya nyuma.

Alisema alifanya kazi na Ustaadh akiwa na Kampuni ya ngumi ya TPBO kwa zaidi ya miaka 20 akimpeleka Tanga bila kujali mazingira ya kimaskini na alikuwa ni mtu wa kukosoa hadharani pale alipoona mambo hayako sawa.

“Nakumbuka huko nyuma kulikuwa na migogoro juu ya uundwaji wa TPBRC, lakini alikubali mabadiliko na alikuwa ni mtu mkweli, likitokea jambo likimkera analiweka wazi na baadaye analimaliza,” alisema.

Kocha wa ngumi za kulipwa, Rajab Mhamila ‘Super D’ alisema Ustaadh alikuwa anaufahamu mchezo wa ngumi kiundani na kuchambua kwa sababu alikuwa mdadisi wa kufuatilia mapambano na mabondia wa ndani na nje.

Alisema kuna viongozi wengi wa ngumi lakini hawawezi kuchambua mchezo huo vizuri kama ilivyokuwa kwake. Naye bondia, Nassibu Ramadhan alisema alisaidia vipaji vingi kujulikana hata uwepo wake yeye ni moja ya mchango wake.

Alisema anakumbuka aliwahi kusafiri naye katika moja ya mapambano na alikuwa akimtia moyo na kumshauri baadhi ya mambo muhimu na yamemsaidia kuboresha kipaji chake.

Chanzo: habarileo.co.tz