Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Mwakinyo ataja mambo 3 ya kumpiga Tinampay KO

85816 Pic+mwakinyo VIDEO: Mwakinyo ataja mambo 3 ya kumpiga Tinampay KO

Mon, 25 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bondia Hassan Mwakinyo ametaja sababu tatu zitakazompa ushindi wa Knock Out (KO) ya raundi ya pili dhidi ya Arnel Tinampay wa Philippines.

Mwakinyo ametamka hayo jana alipokutana na Tinampay kwa mara ya kwanza Dar es Salaam, zikiwa zimesalia siku nne kabla ya kuzichapa Novemba 29.

Mabondia hao watazichapa pambano la raundi 10 la uzani wa super welter litakalopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

“Tinampay ni bondia wa kawaida ambaye kamwe hawezi kucheza na kumaliza raundi zote 10,” alitamba Mwakinyo huku akishangiliwa na mashabiki waliojitokeza kwenye viwanja vya Leaders kuwashuhudia mabondia hao waliokutana kwa mara ya kwanza.

Mwakinyo amezitaja sababu hizo ni ubora, rekodi yake na maandalizi mazuri anayofanya yanampa nafasi ya kumaliza pambano hilo katika raundi ya pili.

Bondia huyo alisema endapo Mfilipino huyo atafikisha raundi ya tatu atakuwa amefanya kazi ya ziada.

“Mashabiki watakaochelewa kufika wajiandae kupishana na mashabiki wakitawanyika huyu Mfilipino havuki raundi ya pili, hana kiwango hicho kwangu,” alitamba Mwakinyo ambaye hata hivyo amezidiwa uzoefu na Tinampay ambaye ana rekodi ya kucheza mapambano 51, amepigwa mara 24 zote kwa pointi na endapo atampiga kwa KO litakuwa pambano la kwanza kupigwa KO.

Ameshinda mapambano 25, ametoka sare mara moja. Mwakinyo amecheza mapambano 17, ameshinda 15 na kupigwa mara mbili, moja ikiwa kwa KO.

Tinampay aliyeambatana na mashabiki wachache alisema si rahisi Mwakinyo kumpiga akisisitiza amekuja kushinda dhidi ya mpinzani wake.

“Naipenda Tanzania na watu wake ni wakarimu, lakini kwa Mwakinyo watanisamehe, nitampiga na baada ya pambano naamini tutakuwa marafiki,” alisema Tinampay.

Mwakinyo alisema ameomba pambano hilo lisiwe na kiingilio ili kuwapa fursa mashabiki wengi wa ngumi kushuhudia.

Promota wa pambano hilo Jay Msangi alisema wanaandaa utaratibu mzuri wa mashabiki kuingia uwanjani.

“Tunatarajia mashabiki 20,000 waingie uwanjani kushuhudia tutaweka utaratibu mzuri kwa wale ambao watakaa jukwaa kuu na majukwaa ya kawaida kwa mashabiki kuingia uwanjani,” alisema.

Mwakinyo amepiga kambi Lushoto, Tanga kujiandaa na pambano hilo ambalo litamuingizia fedha nyingi bila kujali ameshinda au amepigwa.

Hata hivyo akipigwa ataporomoka kwenye viwango vya dunia ambapo sasa ni bondia wa 19 duniani kwenye uzani wa super welter.

Tinampay ambaye ni bondia namba moja Philippines kwenye uzani huo hana cha kupoteza endapo atapigwa ingawa akishinda pambano atapanda kiwango katika ubora wa dunia kama ilivyokuwa kwa Mwakinyo alipozichapa na Samm Eggington aliyekuwa bondia namba nane wa dunia nchini Uingereza Novemba, mwaka jana.

Wakati huohuo, Mfaume Mfaume na Ally Keis ambao watazichapa katika pambano la utangulizi la kuwasindikiza Mwakinyo na Tinampay nusura wazichape kavukavu wakati wakitambulishwa.

Mabondia hao wanaotokea kambi ya Manzese na Mabibo Dar es Salaam watazichapa katika pambano la raundi 10.

Wakati wa kutambulishwa, Keis alimtambia Mfaume kuwa ajiandae kwa kipigo baada ya kumkwepa muda mrefu.

Mfaume alijibu mapigo kwa kumvamia Keis na kutaka wazichape lakini mabaunsa waliwazuia. Idadi kubwa ya mashabiki walijitokeza kwenye viwanja vya Leaders.

Chanzo: mwananchi.co.tz