Kabla ya kuingia Aprili, mwaka huu, kuna uwezekano mkubwa wa lile pambano kubwa linalosubiriwa kwa hamu duniani kati ya Tyson Fury na Oleksandr Usyk likawa limefanyika, duru za awali zikipeleka pambano hilo huko Saudia kama mipango yote ya pande mbili ikitiki.
Tayari mapromota Bob Arum wa Fury na Alex Krasyuk wa Usyk wameshathibitisha uwepo wa pambano hilo, huku siku tatu zilizopita Krasyuk akifichua uwezako wa kusaini kabisa mkataba baina ya pande zote mbili ili hatimaye itangazwe rasmi tarehe na mahali mabondia wao watakapopigania.
Pambano hilo la kuwania mikanda minne ya uzito wa juu (heavyweight), litatoa bingwa asiyepigika (undisputed) kutokana na Usyk kushikilia mikanda ya WBO, IBF na WBA wakati Fury akiwa na ule wa WBC mshindi akienda kuondoa rekodi ya mwisho iliyowahi kuwe-kwa na bondia Lennox Lewis kuwa na mikanda hiyo.
Riddick Bowe, aliyewahi kuwa bingwa asiyepigika kwenye uzito wa juu duniani, hatimaye amekuja na wazo la kwamba, mabondia waliopigwa na Tyson Fury, hawakujua njia nzuri ya kumshinda ni kumchosha kwa kushambulia zaidi mwili wake hususani maeneo ya tumbo, ini na moyo jambo ambalo lingempa wakati mgumu Mwingereza huyo.
Huo ni kama ushauri wa bure ambao Usyk anaweza kuwa bondia wa kwanza kuutumia pindi atakapopambana na Fury ndani ya miezi miwili au mitatu ijayo.