USHINDI wa bondia kutoka Morogoro Twaha Kiduku dhidi ya Mthailand Sirimongkhon Lamthuam juzi, unazidi kumfungulia milango ya baraka baada ya Meneja wa Nassibu Abdul ‘Diamond Plutnumz’ Hamis Shaban ‘Babu Tale’ kusema atamchukua na kumsimamia.
Kiduku alimshinda Lamthuam raundi ya saba ya pambano hilo lililochezwa katika ukumbi wa PTA Sabasaba baada ya kusalimu amri akiomba wasiendelee kutokana na kipigo kikali.
Babu Tale ambaye pia, kwa sasa ni Mbunge mteule wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki aliyeshinda katika Uchaguzi Mkuu kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) hivi karibuni, alisema watu wajue Kiduku yupo katika mikono salama.
“Kiduku nitamchukua na kumsimamia na kumtangaza kwa hiyo watu wajue kuwa yupo katika mikono salama,”alisema.
Hata hivyo, Kiduku alitaja siri ya ushindi dhidi ya bondia huyo mwenye uzoefu mkubwa imetokana na juhudi za mazoezi yake.
Bondia huyo aliwashukuru watu waliokuwa nyuma yake kumuunga mkono akiwemo Babu Tale, Mkuu wa mkoa wa Morogoro na viongozi wengine pamoja na wadau mbalimbali akisema wamechangia yeye kupata ushindi.
Pambano hilo lilikuwa na vituko vingi kutoka kwa mpinzani wa Kiduku ambaye alikuwa ni kama harushi ngumi sana na badala yake mara alikuwa anacheza, anaonyesha staili za nyani na muda mwingine alikuwa akimuita aje ampige.
Lamthuam alipoulizwa staili alizokuwa akizionesha alisema ngumi ni sehemu ya burudani kwa hiyo alikuwa akiburudisha.