Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tumemkomoa Mwakinyo kwa kukataa ‘Nani Zaidi’

Hassan Mwakinyo Jrrrr Bondia Hassan Mwakinyo

Mon, 23 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Bondia Hassan Mwakinyo anaweza kuonekana na wadau na watu wengine kuwa ni mtovu sana wa nidhamu baada ya kukataa pambano lake la hivi karibuni, akidai hawezi kuendekeza ubabaishaji kwenye mchezo huo.

Siku chache baadaye Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa ikatangaza eti kumfungia kucheza ngumi ndani na nje ya nchi kwa kosa hilo, lakini serikali, ambayo sasa ina mtu wa michezo kwenye wizara na ambaye amesomea sheria, imesema itachunguza adhabu hiyo kabla ya kutoa kauli yake.

Binafsi nilitarajia siku moja Mwakinyo atakuja kukumbana na adhabu za waendeshaji ngumi wa Tanzania ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitaka bondia huyo wa Tanga ashiriki katika mipango yao ya maokoto ya humu ndani, lakini Mwakinyo hajakubali kupanda ulingoni kwa hoja nyingi tu.

Ubishi wa vijiweni wa kujua nani ni mbabe katika ngumi Tanzania umekuwa ukiwapa mshawasha mapromota wa ngumi kutaka kuandaa pambano litakalomhusisha Mwakinyo na bondia ambaye kwa sasa anaonekana kuwa ndiye mbabe hapa nchini.

Ni kama vile mashabiki wa muziki wanavyotaka kutokea pambano baina ya Diamond Platnamuz na Ali Kiba, lakini hawapati hiyo nafasi ya kuandaa pambano hilo. Basi hata wawili hao waandae wimbo pamoja, lakini imeshindikana na badala yake kumekuwa na kurushiana vijembe kati ya wasanii hao, hali ambayo inazidi kuwafanya mapromota watamani kupata fursa ya kuwakutanisha wawili hao jukwaa moja.

Ndivyo ilivyo kwa Mwakinyo kutafutiwa mbabe wake kwa miaka kadhaa sasa. Yuko Twaha Kiduku, ambaye amekuwa akishinda mapambano yake yote ya ndani, kiasi kwamba watu wanaona ni muhimu akapambana na Mwakinyo ili kumaliza ubishi wa nani mbabe.

Lakini kila anapoulizwa kuhusu bondia huyo, Mwakinyo amekuwa na majibu yanayoudhi. Mara anasema yeye ni wa kimataifa na hawezi kupambana na mabondia ambao hawalipwi dola. Pamoja na Kiduku, wapo mabondia wengine kama Dulla Mbabe, Ibra Classic na wengine, ingawa msisitizo umekuwa kwa Mwakinyo na Kiduku.

Katika mahojiano na televisheni ya Azam, Mwakinyo aliwahi kusema kama watu wanataka sana hilo pambano, basi liwekwe dau na meneja wake akiridhia, “ndoa itafungwa” akimaanisha pambano litafanyika. Tangu hapo hakujatokea mtu akaweka dau ambalo limekubaliwa na Mwakinyo na menejimenti yake.

Kwa hiyo, kwa muda mwingi Mwakinyo amekuwa akionekana ni bondia anayeringa, hasa baada ya kupata mafanikio makubwa nje ya nchi. Hisia hizo ungeziona zaidi wakati Mwakinyo aliposhindwa Uingereza na kutoa sababu ambazo hakuna mtu amezielewa hadi leo.

Nilishangaa niposikia Mwakinyo amekubali kupanda ulingoni kwa pambano ambalo limeandaliwa na kampuni ya hapa Tanzania. Nilihisi ama wamekubaliana donge nono ama ni kama ni bomu ambalo litalipuka wakati wowote, kutokana na jinsi nimekuwa nikifuatilia misimamo ya Mwakinyo, ambaye hadi sasa ameshinda mapambano 20 kati ya 23 aliyocheza.

Mwakinyo alipangiwa kukutana na bondia kutoka Kenya, Rayon Okwiri, lakini saa chache kabla ya usiku wa pambano hilo kufika, waandaaji walibadilisha mpinzani na kumleta bondia kutoka Namibia, Julius Indongo.

Uamuzi huo ulimkera Mwakinyo na akaamua kutangaza kutopanda jukwaani, akisema huo ni ubabaishaji.

Ingawaje waandaaji wamejaribu kuingiza mambo ya kifamilia na undugu katika suala hilo, bado kuna kasoro zinazoonekana wazi kuwa kama kweli zilikuwepo, zilitakiwa kumalizwa mapema hata kabla ya pambano kutangazwa.

Lakini inaonekana, kama kweli hizo tofauti zilikuwepo, zilipuuzwa kwa kudhani kuwa zitakufa kifo cha kawaida na pambano kufanyika.

Lakini Mtanga huyo akashikilia msimamo wake wa kutopanda jukwaani na pambano halikufanyika. Binafsi nilijua wakati wa kumwadhibu Mwakinyo umeshawadia kwa kuwa sikuona hata mtu mmoja aliyekuwa upande wake; wote walitaka kumwona akipanda jukwaani juu ya ardhi ya Tanzania, ambako hawajamwona muda mrefu.

Hata angetoa sababu gani asingeeleweka kwani alishaonekana anajivuna, kiasi cha baadhi kuanza kudhani anaogopa mabondia wa Tanzania.

Matokeo yake yakawa ni kufungiwa na kamisheni hiyo ya ngumi za kulipwa ambayo sidhani kama ina uanachama wa mashirikisho ya ngumi ya ulimwenguni, kiasi cha kujitwalia mamlaka ya kumfungia.

Mashirikisho ya kimataifa ya ngumi kama IBF, WBO, WBC na mengine huwa na muundo wake kutoka ngazi ya nchi, kanda, bara hadi ulimwenguni. Na ngazi hizo huwa na wigo wa mamlaka yake, hivyo ni vigumu kwa taasisi ambayo si mwanachama wake kumfungia bondia ambaye yuko chini ya chama mwanachama wa shirikisho jingine, isipokuwa pale na kunakuwa na chombo kilichoundwa kwa sheria ya nchi.

Kwangu hilo liko wazi na halihitaji kufikiria sana, lakini ninachotaka kusema ni si lazima kampuni za hapa nchini au vyama vilazimishe Mwakinyo apambane Tanzania au dhidi ya mabondia wa ndani.

Isipokuwa pale bondia wa Tanzania anapokuwa anashikilia mkanda wa kimataifa na ili Mwakinyo aupate ni lazima apambane na huyo Mtanzania.

Mapambano ya kutafuta nani zaidi ndiyo ambayo Mwakinyo amekuwa akiyapinga na hivyo hakuna sababu ya kumtafutia sababu za kumkomoa kwa sababu tu hataki kupindishapindisha mambo.

Ni muhimu hao mabondia tunaodhani kuwa ni wazuri, wafanyiwe jitihada wapande katika chati za ubora duniani na baadaye wapate mapambano makubwa ya nje yatakayowawezesha kushinda mikanda, kuliko haya mapambano ya “nani zaidi”.

Mabondia wanahitaji kupata mapambano makubwa ya kuwania mikanda ndani ya bara la Afrika na duniani kwa ujumla. Tunahitaji kumuona Mtanzania akishiriki angalau katika mapambano ya awali ya pambano kubwa kama la Joshua Anthony na wengine na si haya ya “Nani Zaidi” ya kujiridha mioyo na kuzawadiwa gari.

Chanzo: Mwanaspoti