Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPBRC yabadili upepo ngumi za kulipwa nchini

50031 NGUMI+PIC

Wed, 3 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kuundwa kwa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBCR) huenda kukabadili upepo wa uendeshaji wa mchezo huo nchini kutoka mfumo wa vyama vingi uliokuwa ukilalamikiwa kwa muda mrefu na wadau wa masumbwi.

Mabadiliko hayo yameviondoa rasmi vyama vya ngumi vya PST kinachoendeshwa na Emmanuel Mlundwa, TPBO (Yassin Abdallah ‘Ustaadh’) na TPBF kilichokuwa chini ya Chata Michael ambavyo awali vilikuwa na mamlaka yanayolingana katika mchezo wa ngumi.

Akizungumza Dar es Salaam jana, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa kamati ya muda ya ngumi za kulipwa nchini, Emmanuel Saleh alisema kuundwa kwa chombo hicho kunaweza kuchochea maendeleo ya ngumi nchini.

Alisema uwepo wa vyama vingi ulisababisha migongano katika mchezo huo kwani, bondia au wakala alikuwa akiharibu katika chama kimoja alikuwa na fursa ya kuhamia kingine na kuendelea na shughuli za ngumi.

“Vyama hivyo sasa havina mamlaka ya kuongoza ngumi. TPBRC itakuwa ikitoa vibali kwa mabondia kupigana, itatoa leseni kwa mabondia na itakuwa ikisimamia mapambano ya ubingwa wa Taifa wa TPBRC,” alisema nguli huyo katika mchezo wa ngumi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, waliokuwa viongozi wa PST, TPBO na TPBF walisema wameridhia vyama vyao kutofanya shughuli za kusimamia ngumi kama ambavyo Serikali iliagiza.

“Binafsi tumepokea uamuzi wa Serikali kwa kutaka mchezo wa ngumi usimamiwe na Kamisheni moja ambayo ni TPBRC, kama wenzetu wa Kamisheni wakihitaji mchango wetu watatuita, la wakiona hawahitaji mchango wetu basi tutaangalia fursa nyingine,” alisema Chata.

Kwa upande wake ‘Ustaadh’ wa TPBO alisema chama chake kimeondoka katika ngumi na mchezo huo sasa utakuwa chini ya TPBRC na wao watabaki kuwa mapromota.

Emmanuel Mlundwa wa PST alisema chama chake kitabaki katika ngumi kama wakala.

Akizungumza jana Rais wa TPBRC, Joe Anae alisema atafanya kazi na kila mmoja katika uongozi wake wa miaka mitatu na kipaumbele chake cha kwanza ni kuondoa makundi yaliyokuwepo awali sanjari na kuhakikisha mabondia wananufaika na jasho lao.

Joe alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa TPBRC juzi Jumapili baada ya kupata kura 109 na kumshinda bondia wa zamani nchini Ally Bakari ‘Champion’ aliyepata kura 12 katika uchaguzi huo.



Chanzo: mwananchi.co.tz