Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sports Countdown, Mwakinyo nomaa apanda viwango

Mwakinyoo Bondia Mtanzania, Hassan Mwakinyo (kushoto) akiwa ulingoni

Mon, 6 Sep 2021 Chanzo: eatv.tv

Stori kubwa leo ni bondia mtanzania Hassan Mwakinyo amepanda kwenye viwango vya ubora

6. Ni idadi pekee ya wachezaji wa timu ya taifa ya England waliofunga mabao kuanzia 40 wakiwa na jezi ya taifa hilo. Idadi hiyo imetimia baada mshambuliaji wa taifa hilo Harry Kane kufunga bao 1 kwenye mchezo wa kuwania kufuzu kombe la Dunia mchezo ambao England iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya timu ya taifa ya Andorra. Kane ambaye ni mshambuliaji wa klabu ya Tottenham aliifungia England bao la pili dakika ya 72 kwa mkwaju wa penati na kumfanya afikishe mabao 40 akiwa na kikosi hicho cha Simba watatu. Wafungaji wengine wa England kwenye mchezo huo ni Bukayo Saka, na Jese Lingard aliyefunga mara mbili.

Wachezaji wengine ambao Kane anaungana nao waliofanga mabao kuanzia 40 ni Wayne Rooney ambae ndio mfungaji bora wa muda wote akiwa na mabao 53, Sir Bobby Charlton mabao 49, Gary Lineker mabao 48, Jimmy Greaves mabao 44 na Michael Owen ana mabao 40 sawa na Harry Kane.

5. Ni sawa na muda ambao leo asubuhi kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Taifa stars Kim Poulsen na nahodha Mbwana Samatta watafanya mkutano na waandishi wa habari za Michezo, na kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirikisho la soka nchini TFF ajenda ya mkutoano huo ni maandalizi ya kiufundi ya timu ya Taifa Taifa Stars kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya timu ya taifa ya Madagascar ukiwa ni mchezo wa Kundi J wa kuwania kufuzu fainali za kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani 2022 nchini Qatar. Mkutano huu utafanyika katika ofisi za shirikisho la Soka nchini TFF zilizopo Karume Ilala Dar es salaam.

Kwenye mchezo wa roundi ya kwanza wa kundi hili Taifa Stars ilipata sare ugenini dhidi ya timu ya taifa ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo wakati Madagascar walifungwa na Benini bao 1-0.

4. Ni round ambayo Bondia mtanzania Hassan Mwakinyo alifanikiwa kulimaliza pambano lake dhidi ya Bondia Julius Indonga wa Namibia kwa kumpiga kwa TKO katika pambano lililokuwa la Raundi 12 pambano ambalo lilifanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza Jiji Dar es salaam siku ya Jumamosi Septemba 3, pambano hilo lilikuwa la kuwania mkanda wa ABU.

Na mara baada ya ushindi huo kwa mujibu wa taarifa ni kwamba Hassan Mwakinyo amepanda kwenye viwango vya ubora wa mabondia Dunia kwa mabondia wa uzito wa Super Welterweight, kutoka Nafasi ya 24 hadi ya 13. Lakini pia Mwakinyo ndio namba moja Barani Afrika kwa mabondia wa division yake.

3. Ni tofauti ya alama kati ya Max Verstappen dereva wa Red Bull na Lewis Hamilton wa Mercedes Benz kwenye msimamo wa mbio za magari za Langa langa yani Formulal1, ambapo Verstappen amerejea kilele mwa msimamo baada ya kushinda mbio za Dutch Grand prix zilizofanyika nyumbani kwao nchini Uholanzi ambapo ilikuwa ni kwa mara ya kwanza mbio hizo zikifanyika nchini humo baada ya miaka 36 na zaidi ya mashabiki elfu 70 walijitokeza kumshuhudia kijana wao wa nyumbani akimburuza Lewis Hamilton ambaye alimaliza nafasi ya pili.

Ushindi huo ni wa 7 kwa Verstappen msimu huu na umemfanya afikishe alama 224.5 wakati bingwa mara 7 wa Dunia na bingwa Mtetezi Lewis Hamilton ana alama 221.5. Hizi zilikuwa ni mbio za 13 na bado mbio takribani 10 kabla ya kuumaliza msimu hivyo kijana Verstappen mwenye umri wa miaka 24 bado anakazi ya kufanya ya kupambana na Hamilton na mbio zinazofata ni za Italia zitakazofanyika September 12.

2. Ni idadi ya madhambi (fouls) ambazo timu za Argentina na Brazil kila moja ilifanya kwenye mchezo wa kuwania kufuzo kombe la Dunia ambao ulichezwa kwa dakika takribani 5 tu na kuhairishwa baada ya Polisi wa nchini Brazil kuingia uwanjani na kutaka kuwatoa wachezaji 4 wa Argentina ambao wanatajwa walivunja kanuni za kujikinga na Uviko 19. Wachezaji hao wanne ni wale wanao cheza katika ligi kuu ya nchini England EPL ambao ni Emiliano Buendia na Emiliano Martinez wanaocheza Aston Villa, Giovani lo Celso na Cristian Romero wanacheza Tottenham Hotspur.

Kwa mujibu wa kanuni za Kujikinga na Uviko 19 nchini Brazil wageni wote wanaotoka nchini Uingereza wanapaswa kujitenga yani kukaa karantini kwa siku 14 lakini wachezaji hao hawakufanya hivyo. Na Shirikisho la soka Duniani FIFA limethibitisha mchezo huo kuhairishwa lakini haijatolewa taarifa mchezo utachezwa tena Lini.

1. Ni nafasi anayoshikilia mcheza tennis raia wa Serbia Novak Djokovic kwenye orodha ya viwango vya ubora wa tennis kwa wanaume Duniani, na mserbia huyo amefanikiwa kufuzu raundi ya 4 ya michuano ya wazi ya Marekani US Open kwa kumfunga mjapani Kei Nishikori kwa Seti 3 -1 ambapi Nishikori alishinda seti ya kwanza kwa 6-7 kabla ya Djokovic kushinda seti 3 mfululizo kwa 6-3 6-3 na 6-2, huu ulikuwa ni mchezo wa 17 mfululizo Novak Djokovic anamnyuka Kei Nisshkole. Na katika roundi hiyo ya nne Djkovic ataminyana na mmarekani Jenson Brooksby ambaye anashika nafasi ya 99 kwenye viwango vya ubora.

Djokovic mwenye umri wa miaka 34 ambaye ni bingwa mara 20 wa Grandslams anaiwania rekodi yakushinda Grandslams 21 endapo kama atafanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano hii ya US Open ambayo itamfanya kuwa mchezaji mwenye Grandslams nyingi upande wa wanaume, kwa sasa anamataji 20 sawa na Rodger Federer na Rafael Nadal ambao wote hawajashiriki katika michuano ya US Open.

Chanzo: eatv.tv