LEO hii tunamtaja kama bingwa wa dunia. Japo wengi walianza kumfahamu alipomchapa Stanley Mabesi kwa Knock Out (KO) Februari 12, 1994. hilo ndilo pambano lililompa chaneli kwenye ndondi za kulipwa, Rashid Matumla ‘Snake Man’.
Bondia huyo anakumbuka namna Mabesi ambaye sasa ni mchungaji nchini Uholanzi alivyokuwa hapigiki kirahisi. Alivyokuwa staa, lakini ghafla kibao kikageuka.
“Ilikuwa ngumu kumpiga Mabesi, alikuwa hashikiki ulingoni, nilipomchapa pale ndipo jina langu likaanza kuwika,” anasimulia Matumla.
Japo jina la kaka yake, Ally Matumla lilimbeba, Rashid anasema kipigo cha KO kwa Mabesi kilimtambulisha zaidi. “Lilikuwa ni pambano ambalo Mabesi na mashabiki wake hawakutarajia, lakini ile nia, nidhamu ya mchezo na shauku ya kutaka kutengeneza zama zangu kwenye ndondi vilinibeba,” anasema. “Wakati huo kaka yangu Ally alikuwa tayari ana jina kwenye ngumi, lakini sikutaka kusafiria nyota yake.”
ACHUNGULIA KABURI
Rashid anasema angekuwa mwoga, basi pambano la 1988 akiwa na timu ya taifa ya ngumi za ridhaa kwenye michezo ya Olimpiki ndilo lingemstaafisha masumbwi, lakini kwa kuwa aliupenda mchezo huo hakuhofu.
“Nilijua nakufa, kuna muda niliwaona hadi ndugu zangu wananisogelea kuniaga, sitakaa nilisahau tukio lile,” anasema.
Ilikuwa mjini Seoul, Korea Kusini ambako alikuwa miongoni mwa mabondia wanne waliofuzu kuiwakilisha nchi kwenye Olimpiki. Wengine ni Benjamin Mwangata (sasa marehemu), Haji Ally na Joseph Marwa.
“Nilicheza pambano la kwanza nikashinda raundi ya kwanza kwa RSC (alimchapa Dieudonne Kouassi wa Ivory Coast katika uzani wa light welter na kufuzu raundi ya pili ambapo alizichapa na Mrusi, Vyacheslav Yanovski).
“Tulipigana raundi mbili za mwanzo kwelikweli, Mrusi hakubali, alikuwa na nguvu za ajabu, raundi ya tatu alinipiga kwa RSC (refarii alisimamisha pambano ili kumuokoa Matumla).
“Nilipotoka pale, niliumwa kichwa, sijawahi kusikia maumivu kama yale katika maisha yangu ya ngumi, nilijua nakufa, kuna muda nilikuwa naona kama maluweluwe, naona ndugu zangu wamekuja kuniaga, lile pambano sitakaa nilisahau ila lilinijenga,” anasema.
Mrusi ndiye alikuwa bingwa kwenye uzani wa light welter huku Mwangata pia akisonga raundi ya pili baada ya kumchapa Mmalawi Peter Ayesu kwa pointi za majaji wote na kupigwa na Mghana Alfred Kotey. “Ile michezo ilinijenga na kama ningekuwa mwoga nafikiri pale ndipo ningeacha ngumi, lakini haikuwa hivyo hadi nikawa bingwa wa dunia wa WBU.”
KUMILIKI BENZ
Matumla ameacha historia ya kuendesha Benz wakati wake. Gari hilo alipewa na rafiki yake Msauzi aliyemtaja kwa jina la Peter Brandon. “Huyu alikuwa mfanyabiashara wa madini, alikuwa ni shabiki wangu, hivyo aliniletea Benz kama zawadi ingawa baadaye nililipiga bei kwani ilikuwa gharama kubwa kulitumia.
“Kwa mtazamo wa nje watu wengi wanajua nilikuwa nalipwa pesa nyingi sana, lakini haikuwa hivyo kabisa,” anasema.
KIPATO CHAKE
Katika mapambano ambayo anaamini yangemlipa ni lile la Italia dhidi ya Paolo Pizzamiglio mwaka 1999 alipozichapa kuwania ubingwa wa dunia wa WBU. “Lile pambano liliingiza Sh70 milioni, lakini nililipwa Sh2 milioni pekee niliporejea nchini na Dola 500 nilipokuwa Italia.”
Anasema wakati huo alikuwa chini ya promota (anamtaja) ambaye alikwenda kuomba pambano akasaini mkataba, lakini ikashindikana. “Hilo jambo lilileta mgogoro sana, nakumbuka mkataba ulikuwa wa Sh70 milioni, lakini pesa iliingia kwa promota niliyekuwa chini yake.
“Nikiwa Italia nilipewa Dola 500, baada ya kurejea nikapewa Sh2 milioni na gari Toyota Chaser basi, hata hivyo gari nililiuza kutokana na gharama za uendeshaji,” anasema.
KUKATA MAKALI YA MAISHA
Bondia huyo sasa hana nguvu za kuonyesha uwezo ulingoni, anamalizia maisha ya ustaafu nyumbani kwake Mbagala Kuu, Dar es Salaam katika nyumba ambayo anasema ilitokana na kipaji chake cha ndondi.
“Nimechoka kuishi bondeni Keko, nimeamua kuja kwenye nyumba yangu Mbagala ambayo hapa kuna eneo nimetenga mabondia wanajifua ngumi,” anasema na kwamba pesa za ujenzi alizipata kwenye pambano dhidi ya Harry Simon huko Windhoek, Namibia alikolipwa Sh30 milioni.
Katika pambano hilo alikutana na ‘upper cut’ ya maana iliyomchana chini ya mdomo na kushi-ndwa kuendelea.
Mapambano yake mengi anadai alilipwa sio zaidi ya Sh3 milioni hadi Sh4 milioni na baada ya Namibia alipigana mengine 10 - moja Ujerumani na kuamua kustaafu, Agosti 10, 2013. Baada ya kustaafu ndondi, anasema alianza kupata maumivu ya miguu na mgongo ambayo awali hakufahamu chanzo chake.
“Rais Kikwete (Jakaya - Rrais wa Awamu ya Nne) alinilipia matibabu nikatibiwa na kupona.”
Anasema kabla Kikwete hajawa Rais alikuwa mpenzi wa ngumi na kuna wakati alikwenda ukumbini kuangalia laivu ndondi. “Alikuwa shabiki wangu kwenye ngumi, huko ndiko tulikutana na akawa anapenda uchezaji wangu.
“Nakumbuka hata pambano langu na Cheka (Francis aliyekuja kuwa bingwa wa dunia wa WBF baadaye) JK alinisapoti sana, alinisaidia tukakodi gari mbili aina Coaster kwenda Morogoro na mashabiki wangu kwenye pambano hilo,” anasema.
Pambano hilo lilipigwa Februari 13, 2009 Uwanja wa Jamhuri na Matumla alipigwa kwa pointi akivunja rekodi ya kumchapa Cheka mara mbili kwa TKO na KO.
“Wakati ule Cheka ndiyo alikuwa anakuja juu, naamini lile pambano nilishinda lakini majaji waliamua kumpa tu Cheka ushindi kwa kuwa ndiyo alikuwa anaandaliwa kuchukua nafasi,” anasema na kwamba hilo ni moja ya pambano lake gumu aliyowahi kupigana.
APOTEZA MAWASILIANO NA JK
Katika vitu ambavyo vinamuumiza bondia huyo ni kupoteza mawasiliano na Rais mstaafu Kikwete ambaye anamtaja kama rafiki yake.
“Nilikuwa nampigia tunazungumza, nakumbuka mara ya mwisho nilitumia simu ya Ridhiwan (mtoto wa JK) kuzungumza naye, aliniambia Matumla hakikisha unaangalia afya yako.
“Huwa natamani nifunge safari niende Msoga kumtafuta, lakini wasiwasi wangu nitafanikiwa kumuona? Mambo mengi sana ya kumwambia siku nitakayobahatika kumuona. Rafiki yake sasa naumwa, afya yangu si nzuri, naamini ningebahatika kumuona asingesita kunisaidia ili nifanyiwe upasuaji wa tatizo linalonisumbua sasa,” anasema.
“Hata niliposhinda ubingwa wa dunia kule Italia alikuja uwanja wa ndege kunipokea, ni kiongozi aliyenipa hamasa sana na mafanikio yangu ulingoni amechangia.”
MAUMIVU MIAKA SITA
Bondia huyo sasa ni mgonjwa, anasumbuliwa na maumivu makali ya miguu na mgongo.
“Mwaka wa sita sasa niko kwenye maumivu makali, nilipimwa nikagundulika nasumbuliwa na ugonjwa, natakiwa kufanyiwa upasuaji, ila nimekosa pesa ya matibabu,” anasema na kutaja gharama za upasuaji kuwa ni Sh 3,080,000 ambazo anawaomba wadau kumsaidia ili atibiwe.
HUYU HAPA MRITHI
Licha ya kutofahamiana na familia ya Amir, Matumla ameamua kumlea kijana huyo ambaye ana ndoto ya kufuata nyayo zake.
Bondia huyo anayejiita Amir Rashid Matumla ni mzaliwa wa Songea aliyesikia habari za Matumla na kuamua kumtafuta.
“Nilikuwa naishi Tabata na kaka yangu, nilipenda sana ngumi, siku moja tukiwa tunafanya sparing ‘mazoezi ya kuzichapa ana kwa ana’ kuna tukio lilitokea ambalo lilinifanya niwe katika wakati mgumu sana, nashukuru lilipita.
“Ndipo nilianza kumtafuta Matumla huko Keko ingawa siku ya kwanza sikumkuta, nilipewa mawasiliano yake ila aliniambia yupo Dodoma atakaporudi niende, nikafanya hivyo na aliamua kunichukua na kuishi naye, nimewaeleza wazazi wangu kuhusu hili,” anasema Amir.
“Baba yuko Songea na mama Morogoro, huwa wanawasiliana kwenye simu na wazazi wangu wanafahamu huyu ndiye baba yangu na mimi ndiye Snake Junior, ananilea katika misingi mizuri, ananipenda na ninamuahidi sitamuangusha.”
Matumla anasema tangu siku ya kwanza alipomuona kijana huyo alijua ni bondia, licha ya umri wake wa miaka 19 anajituma na ana nidhamu ya mchezo.
“Huyu ndiye atakuwa mrithi wangu ulingoni, nilitamani wanangu wafuate nyayo, lakini ndiyo hivyo, yupo mmoja JKT, Daudi (aliwahi kuwa timu ya taifa) nilitarajia ndiye angefuata nyayo kweli kweli.
“Alianza vizuri sana na alikwenda hadi Olimpiki ya vijana, aliporejea nchini tu akakataa ngumi mpaka leo, Mudy ‘Mohammed’ pia alikuwa ameanza kutamba, lakini akapata matatizo,” anasema.
Mudy alipasuliwa fuvu la kichwa baada ya kupigwa KO na Mfaume Mfaume miaka kadhaa iliyopita, hivyo alishauriwa kuwa nje ya ulingo kwa miaka miwili.
“Sasa hajambo, lakini kurudi bado, hayupo sawa ingawa kuna muda anafundisha mabondia, lakini hajawa fiti kurudi kwenye ngumi.
“Kama angenisikiliza angecheza ngumi muda mrefu, nilimuelekeza sana lakini hakusikia, nilimwambia nimecheza ngumi nazifahamu mpaka sasa nakufundisha, nisikilize lakini vijana hawa akianza kushika pesa zinakuwa tamu anashindwa kufuata maelekezo,” ansema
KUUZA PAMBANO
Kumekuwepo na madai ya baadhi ya mabondia kudaiwa kutumika kuwatengenezea rekodi mabondia wengine kwa kukubali kupigwa wanapokwenda kucheza nje ya nchi.
“Binafsi sijawahi kushawishika wala kukutana na kitu hicho katika maisha yangu yote ya ngumi.
“Kama yupo bondia anapaswa kutambua hayo ni maisha yake, akishinda anatengeneza rekodi na huenda akapata pesa nzuri zaidi baadaye, binafsi siwezi hata ningekuwa bado napigana nisingekubali kudanganyika,” anasema.
Matumla amestaafu ngumi akiwa na rekodi ya kupgana mapambano 72, ameshinda 49 (34 kwa KO), amepigwa 19 (7 kwa KO) na sare nne tangu 1993 hadi 2013.
Imeandikwa na Imani Makongoro, Mwanahiba Richard na Thomas Ng’itu