Ni miaka zaidi ya saba sasa imepita, lakini tukio hili halijafutika katika kumbukumbu ya maisha ya bondia wa uzani wa juu aliyetikisa nchini, Awadh Tamim.
Bondia huyu bingwa wa zamani wa Afrika Mashariki na Kati wa uzani wa juu hivi sasa anaishi nchini Sweden na familia yake yenye watoto wanne, watatu wakiwa raia wa nchi hiyo.
Anakumbuka namna safari yake nchini humo ilivyoanza kama ‘muvi’ iliyojaa misukosuko, lakini yote hiyo ilikuwa ni sababu ya kuamini njia rahisi ya kuishi nchini humo ni kuingia kwa kuzamia.
Anasema aliijua Sweden kabla ya kuzamia kwani alikuwa na utaratibu wa kwenda nchini humo kumtembelea rafiki yake ambaye ni raia wa nchi hiyo, hivyo kujikuta anafahamu baadhi ya maeneo.
Tamim anasema mwaka 2011 alikwenda Finland kwenye pambano na huko ndiko alipopata wazo la kutorejea nchini, na badala yake alipanda boti kwenda Sweden lakini kwa kupitia njia za panya.
Anasema alipoingia nchini humo maisha yalikuwa magumu kwani kila raia wa Sweden alikuwa na namba inayomtambulisha ambayo kama mtu anaishi kihalali hiyo namba ikiingizwa kwenye kompyuta za serikali taarifa za mhusika zinaonekana, lakini yeye hakuwa nayo. “Mwenyeji wangu aliniuliza kama nimeingia nchini humu kihalali, sikutaka kumficha chochote nilimueleza ukweli kwamba nimezamia, akaniambia Tamim kama unataka maisha yako yawe magumu uishi Sweden kwa kuzamia,” anasema.
Pia Soma
- Wachezaji Watanzania waliokimbia corona nje
- Wababe wa London Marathon hawa hapa
- Atiki: Safari ya mafanikio kikapu ilianzia Mnazi Mmoja
Anasema maisha ya kuzamia nchini humo kwanza mtu hawezi kupata ajira nzuri, hivyo ilikuwa ni lazima akubali kuwa kibarua na kufanya kazi kwa malipo kidogo ili aweze kupata fedha za kula.
Japo mabondia, Omary Kimweri na Karim Matumla walizamia nchini Australia mwaka 2006 na mcheza tenisi ya meza, Fathiya Pazi mwaka 2018, Tamim anasema hakuna kitu kigumu kama kuchukua uamuzi huo.
“Mwenyeji wangu aliniambia maisha ya kuzamia ni mateso na ukubali kufanyishwa kazi kubwa na ngumu kwa malipo kiduchu na huwezi kuwa na mahali pa kulalamika,” anasisitiza.
“Na ndivyo ilivyokuwa katika kipindi kifupi nilichokaa kule kabla ya kurudi nyumbani, unapitia maisha ya mateso na unyonyaji, leo hii nikimsikia mtu ana wazo la kuzamia nitakuwa balozi mzuri sana kwake, ukitaka kuishi Ulaya fuata taratibu tu, utafurahia maisha ya huku.”
Anasema alikaa muda mfupi Sweden na kuamua kurejea nchini ili kuanza upya harakati za kwenda kuishi nchini humo kihalali na kufanikiwa ambako kwa mara nyingine alipokewa na rafiki yake. “Nikiwa huku (Sweden) nilipambana hadi nikafanikiwa kupata leseni ya udereva ambayo ndiyo inaniingizia fedha na kunifanya niishi maisha mazuri tu huku,” anasimulia.
Anasema Sweden hakuna kitu rahisi kupata kama gari hasa ukiwa na leseni, kwani nchini humo magari ni mengi yameegeshwa hakuna madereva.
“Kuna fomu unapewa unajaza na wamiliki wa magari wanakupa kwa makubaliano maalumu, kama ningekuwa nimezamia fursa hiyo nisingeipata sababu nisingekuwa na ‘code’ zaidi ningeishia kufanya kazi mashambani au nyingine ngumu kwa ujira kiduchu tofauti na sasa,” anasema.
“Sina kipingamizi chochote kufanya kazi huku, nilianza kufanya kazi ya kusafirisha mizigo, nilifungua kampuni ambayo awali ilisafirisha mizigo ya ndani na sasa tunasafirisha hadi nje ya Sweden.”
Anasema kazi hiyo imekuwa ikimuingizia fedha na kufanya maisha yake nchini humo kuwa rahisi, ingawa kipindi hiki cha janga la corona wamekuwa wakisafirisha vyakula kwenye viwanja vya ndege.
Mke mzungu
Tamim anasema baada ya kuishi kwa muda nchini humo alikutana na mwanamke wa kizungu ambaye walipendana, akamuoa
“Tulibahatika kupata watoto watatu, pamoja na mwingine mmoja ambaye nilipata nikiwa nyumbani Tanzania, nilipokuja huku nilimchukua pia,” anasema.
Ushawishi kubadili uraia
Tamim ambaye bado anatumia pasipoti ya Tanzania, anasema aliwahi kushawishiwa kubadili uraia na kuwa raia wa Sweden.
“Tangu nimekuja huku sikuwahi kufikiria hili, japo wanangu watatu ni raia wa Sweden, lakini mimi nikifanya uamuzi huu kuna vitu nitapoteza.”
Anasema kabla ya kuhamishia maisha nchini humo alikuwa amewekeza jijini Dar es Salaam, eneo la Kigamboni, hivyo kama atalazimika kubadili uraia na kuwa raia wa Sweden atapoteza haki nyingi Tanzania. Kwa sasa Tanzania haina uraia wa nchi mbili. “Sitaki kubadili kabisa uraia wangu japo nimekuwa nikishawishiwa nifanye hivyo, lakini bado naipenda Tanzania, nimewekeza nyumbani na sitarajii kama itatokea nibadili uraia wangu,” anasema.
Sweden maisha haya hayapo
Kibongo Bongo ni jambo la kawaida mtu kutoka kazini na kupitia kwa ‘washkaji’ zake kupiga stori mbili tatu kabla ya kurudi nyumbani, lakini Tamim anasema maisha hayo huko Sweden hayapo.
“Huku hakuna kupiga stori vijiweni na washkaji kama Bongo, muda huo haupo, ukitoka kazini ni nyumbani ambako huko una ratiba ya kazi nyingine.”
Anasema Sweden kuajiri mfanyakazi wa ndani ni gharama na ni baadhi ya watu ndio wanazimudu, kwani mfanyakazi wa ndani mbali na mshahara anatakiwa kulipiwa bima na masuala mengine kama walivyo waajiriwa wa maofisini.
“Gharama hizo zilinishinda, hivyo nalazimika kufanya kazi inayoniingizia kipato na vilevile kuwahudumia wanangu na kufanya majukumu mengine ya nyumbani kama kupika, usafi na kuwahudumia watoto,” anasema Tamim.
“Bahati mbaya mke wangu raia wa Sweden alikuwa mbali na mimi kwa muda, hivyo mimi ndiye mwenye majukumu yote kwa watoto wangu wanne, watatu niliwapata huku na mmoja nilizaa nikiwa nyumbani Tanzania, naye nilimchukua niko naye huku.
“Jioni lazima niwafuate watoto shuleni, niwapikie na kuhakikisha wametekelezewa majukumu yao yote, asubuhi pia kabla ya kwenda kazini lazima niwapeleke shuleni, tunafanya kazi kwa saa, hakuna kabisa muda wa stori kama nilivyokuwa nyumbani Tanzania.”
Bondia huyo ambaye alikuwa na upinzani mkali ulingoni na bondia wa Zanzibar, Ashraf Suleiman na mara ya mwisho kuzichapa nchini ilikuwa Machi 2011, pambano ambalo Tamim alishinda kwa KO raundi ya sita, anasema katika vitu anavyovikumbuka nchini ni upinzani wa ngumi uliokuwepo miaka ya nyuma.
“Sijui kama upinzani huo sasa bado upo nchini, lakini huwa nawakumbuka sana mabondia wa nyumbani na ninatamani siku moja nirudi kucheza Tanzania,” anasema bondia huyo huku akisisitiza kuwa huwa ana ratiba ya kufanya mazoezi ya ngumi nchini humo.
Unataka kuwa bondia wa uzani wa juu?
Tamim ambaye ana rekodi ya kucheza mapambano 15 na kushinda 12 (7 kwa KO) na kupigwa mara tatu zote kwa KO, anasema kuwa bondia wa uzani wa juu siyo lazima uwe na ‘bonge la mtu’ kama mtizamo wa watu wengi hasa Tanzania ulivyo.
Anasema mtizamo huo ndio unalifanya Taifa kukosa mabondia wa uzani wa juu wenye upinzani kama ilivyokuwa kwao, huku mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (boxrec) ukimtambua bondia mmoja pekee Tanzania, Alphonce Mchumiatumbo kwenye uzani huo
“Bondia wa uzani wa juu anatengenezwa, japo sifa kuu kwanza lazima uwe na afya nzuri, ule vizuri na uwe na uwezo wa kufanya mazoezi makali, lakini kwa Tanzania wengine kwa kuwa wamenenepa wanafikiri hiyo ni sifa ya kuwa ‘hevi’,” anasema bondia huyo.
“Ngumi ni moyo, ukiingia tu kwa kuwa una sifa ya kuwa mnene lazima uishie njiani, ngumi ni ngumu hivyo ili kucheza lazima pia uwe na roho ngumu, uvumilivu na malengo ambayo mwishoni utaona matunda ya kazi unayoifanya.”
Anasema bondia wa uzito wa juu lazima awe na kilo za kutosha, ale vizuri na kushiba ili aweze kufanya mazoezi na sio kuungaunga katika chakula, na ili aweze kufanikiwa lazima awe na meneja na mtu wa ‘kumpromoti’.
“Kama huna promosheni ambayo itakusimamia kuanzia chakula, mazoezi, vifaa ni lazima ukwame, Tanzania kuwa bondia ‘hevi’ ni ngumu sana kama hakuna uwekezaji, huwezi kuwa na njaa ukastahimili kurusha ngumi,” anasema.