Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Coastal Union ya Tanga, Salim Bawaziri amesema kitendo cha kumfungia Bondia, Hassan Mwakinyo mwaka mmoja sio dawa ya kumsaidia Bondia huyo, bali ni kuua kipaji chake.
Mapema juma hili, Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) ilimfungia Mwakinyo mwaka mmoja kushiriki mchezo huo ndani na nje na kumlima faini ya Sh. Milioni Moja kutokana na kugomea pambano lililokuwa lifanyike Septemba 29 dhidi ya Rayton Okwiri kutoka Kenya aliyebadilishiwa kwani awali alitakiwa kupigana Julius Indonga.
Bawaziri amesema hata Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) zamani lilikuwa likiwafungia wachezaji kwa miaka mingi lakini baada ya kugundua kuwa linaua vipaji likaamua kubadilika na kuwapa adhabu nyingine za faini na kukosa baadhi ya mechi.
“Mwakinyo anatakiwa kusaidiwa na chama cha ngumi na sio kumfungia, inatakia watafutwe watu wa karibu na kumzungumza naye kumsaidia kwa fikra na mawazo lakini unapomfungia unaua kipaji chake,” amesema Bawaziri akisisitiza kulihitajika busara zaidi kuliko kumuondoa Mwakinyo kwenye ulingo wa ngumi.
“Chama cha ngumi nia yake ni kukuza mchezo huo, isifike mahali mtu akikosea anaitwa na kuzungumza naye na kumuonya na hata kumpiga faini,” ameongeza Bawazir na kutaka chama cha ngumi kuwaita watu wake ili kumshauri bondia huyo.