Unalikumbuka lile pambano la mwisho la Bondia Ibrahim Mgender ‘Ibrah Class’ akimkung’uta Mmexico Gustavo Pina Melgar ‘Alan Pina’ kwa Knockout (KO) raundi ya tisa uzito wa Super Feather katika Ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam? Mwamuzi wa pambano lile alikuwa mwanamke. Aliitwa Pendo Njau, alionyesha ubora wa hali ya juu?
Basi haya ni mahojiano na refa huyo aliyefunguka mwanzo hadi mwisho kuhusu safari yake hadi kuwa refa wa ngumi.
KASEBA AMCHOREA RAMANI
Pendo amemtaja bondia wa zamani wa kick boxing, Japhet Kaseba ndiye aliyechorea ramani ya kuwa mtu wa ngumi kwa maana ya bondia na refa muda mchache tu tangu walivyokutana jijini Dar es Salaam mwaka 2002.
“Kaseba ndiye amenifanya niingie kwenye ngumi, kabla ya hapo nilikuwa nafanya biashara zangu za kununua na kuuza mbao, natoa Morogoro, naleta Dar, Tanga, Mombasa ya Kenya na sehemu mbalimbali.
“Siku moj nikiwao Dar na rafiki zangu tumekaa sehemu tunakula, nikamuona Kaseba akimpigisha mazoezi mdada mmoja kwenye televisheni.
“Hapo hapo nikawaambia wenzangu napenda sana huu mchezo lakini sijawahi kujaribu, jamaa mmoja akaniuliza wewe utaweza kucheza ngumi kweli? Nikamwambia ndio napenda, basi jamaa yule akaniambia anamfahamu Kaseba na atanikutanisha naye.
“Nilijua ni masihara kwani mwanzo nilijua Kaseba sio Mtanzania na alivyokuja sikuamini ila tulipiga stori mbili tatu aliniambia anapoishi na nikamueleza nilipofikia kwani nilikuwa hapa mjini kwa ajili ya biashara zangu za mbao tu.
“Baada ya hapo nilianza mazoezi mdogo mdogo hadi nikaiva na nilipigana mapambano mengi tu ikiwemo mawili ya ubingwa wa World Kick-Boxing Network na Best Kick-Boxing League na kushinda yote nikiwa chini ya Kaseba,” anasema Pendo.
KUTOKA BONDIA HADI REFA
Refa huyo asiye na uoga ameeleza chanzo cha kuacha ubondia na kugeukia kwenye urefa ni moja ya makocha wa gym ya Kaseba kumuona hafai tena kupigana bali kuwa refa.
“Sababu kubwa ya kuhamia kwenye urefa, kuna kipindi nilisafiri muda mrefu kwenda Dubai na nilipokuwa huko sikufanya mazoezi nilivyorudi Bongo 2018 nilikuja gym hapa kwa Kaseba lakini nilivyokuwa nafanya mazoezi, mmoja wa waongozaji akamwambia Kaseba huyu binti yako sio mchezaji ngumi tena bora awe refa.
“Hiyo ni kutokana na mara nyingi niliporudi nilikuwa mzembe kiasi na wakati mabondia wengine wakipigana pale gym nilikuwa nawaamulia nadhani ndio chanzo cha kocha kumwambia Kaseba nafaa sana kwenye urefa na safari ikaanzia hapo,” anasema Pendo anayeongeza kuwa haikumsumbua kuzoea kwani ni kitu alichokuwa anakijua.
“Ukiangalia kucheza ngumi na kuwa refa ni majirani, nafanya urefa kwa ubora kwa kuwa nimewahi kupigana pia hivyo najua sheria zote, pia najua uzito wa ‘punch’ na maumivu yake, kwahiyo nipo mulemule tofauti na mtu anayekuwa refa wakati hajawahi kupigana.”
PAMBANO LA KWANZA
Anasimulia hali aliyokuwa nayo kwenye pambano la kwanza kuchezesha kuwa alikuwa na uoga lakini ni pambano lililomtengenezea njia na uaminifu kwa waandaaji wa mchezo huo.
“Sikumbuki ilikuwa pambano la nani na nani lakini ilikuwa Bagamoyo. Ilikuwa tofauti na nilivyokuwa nimefundishwa kwani mara nyingi nilikuwa najifunzia kwenye eneo la wazi bila ringi hiyo ilikuwa kwa mara ya kwanza nilikuwa na mawazo mengi sana aisee.
“Pamoja na yote nililimaliza lile pambano kiutaalamu zaidi baada ya bondia mmoja kupigwa punchi moja nzito na ile anataka kupigwa ya pili nikaingilia kati na kumaliza pambano na baada ya hapo nilivyoshuka jukwaani na kupongezwa na kila mmoja kuwa nimefanya vizuri na hapo ndio ukawa mwanzo wa kuaminiwa na kupewa mapambano mengi zaidi.
“Kwa sasa mimi ni refa mkubwa, nimechezesha mapambano mengi ya kawaida na ya ubingwa nimeshafanya WBF, ABU, UBO na mikanda mingine mikubwa nimechezesha vizuri, hivyo kwa sasa naweza kuchezesha pambano lolote lile duniani,” anasema Pendo.
KIDUKU, MBABE NOM
Licha ya kuchezesha mapambano kibao, Pendo amelitaja pambano la Dulla Mbabe na Twaha Kiduku kuwa miongoni mwa mapambano yaliyompa changamoto kubwa kuchezesha lakini akalimaliza kibabe.
“Kila pambano linachangamoto zake lakini mengi nimekuwa nikiyamudu na kwenda nayo freshi lakini miongoni mwa mapambano ambayo siwezi kuyasahau, mojawapo mi ni lile la Mbabe na Kiduku.
“Ujue Kibongo bongo ile ilikuwa kama dabi, wadau wa ngumi walitaka kuona nini kinatokea na lilikuwa na mvuto wa aina yake.
“Kwa namna walivyocheza kulikuwa na changamoto zao na presha kubwa lakini mwishowe nilisimama kama refa mweledi na kila kitu kilienda sawa,” anasema.
UHAI WA BONDIA
Moja ya vitu vilivyompa sifa zaidi Pendo akiwa kama refa ni ushujaa wake wa kuwahi kumuokoa bondia Alan Pina baada ya kupigwa punchi mbili nzito na Ibra Class siku chache pale Mlimani City na hapa anaeleza kwa nini alifanya vile.
“Miongoni mwa vitu refa unapaswa kufanya ni kuilinda afya ya bondia, unatakiwa uwe tayari kiakili, ujiandae vyema kabla ya kuanza pambano usiwe muoga na na mawazo mengine tofauti na pambano hilo.
“Kilichotokea pale niliona Pina mambo yamemuwia magumu na alikuwa katika hali ya hatari zaidi ikabidi nimpe huduma ya kwanza.
Pendo anasema pambano la Ibra na Pina lilikuwa gumu na tensheni ilikuwa kubwa sana na yeyote kati yao alikuwa anaweza kupigwa KO, ila Pina alikuwa hataki kuanguka chini na hakutaka kuonyesha kama alikuwa akipigwa punchi kali.
“Ujue kwenye pambano refa ndiye anayeshikilia uhai wa mabondia, hivyo unatakiwa kufanya kila uwezavyo kuhakikisha kila mmoja anatoka salama,” anasema Pendo huku akisema alikuwa anaujua uzito wa punchi za mabondia hao.
“Ibra alikuwa amebadilika sana tofauti na mapambano mengine ambayo nilikuwa nayasiamamia.
Njau anasema hufanya maandalizi mapema kwani siku ya pambano unaweza kuchezesha mapambano hata matatu, hivyo anaiseti akili yake kwa ajili ya ngumi tu na sio kitu kingine.
NI MAMA WA FAMILIA
Pamoja na ubabe aliokuwa anauonyesha wakati akiwa bondia na sasa refa, Pendo amefunguka mbele ya Mwanaspoti ni mama wa watoto wawili mmoja mkubwa akiwa kidato cha pili na mwingine yupo darasa la tano.
“Ni mama wa watoto wawili, mmoja amezaliwa 2007 wakati huo nilikuwa bondia na mwingine ana miaka tisa na wote wanapenda mchezo huu wa ngumi.
“Baba yao yupo na anatusapoti wote kwa kiasi kikubwa sana, anaamini katika sisi na utendaji wao, nashukuru Mungu ananielewa kwenye kazi zangu na tunaishi freshi,” anasema Pendo na kueleza changamoto anazopitia kwenye mchezo wa ngumi kama mtoto wa kike.
“Watu wengi wanaamini ngumi sio mchezo salama na ni wa watu wagumu jambo ambalo sio kweli, wanawake wamekuwa wachache lakini kwa sasa wameongezeka na wanaendelea kuingia huku na nawaomba wajae.
“Nakumbuka wakati naingia kwenye ngumi niliwaficha wazazi wangu ila siku moja nakaribia kupigana pambano nilienda kwenye redio ya taifa kuhojiwa ndipo baba akasikia.
“Nakumbuka alinipigia simu sikupokea na baadaye akapiga tena ndio nikapokea akaniuliza umeingia kwenye masumbwi? Nikashindwa kumjibu nikawa natetemeka baadaye akaniambia ongea na mama yako kwanza ndio nikamchana ukweli mama na yeye akanitakia kila la kheri na huo ndio ukawa mwanzo wa wao kujua.”
AWAITA WANAWAKE
Pendo amewataka wanawake wengi kujiunga kwenye ngumi na kwenye urefa wa masumbwi kwani mchezo huo ni biashara na unamfanya mtu kuwa imara zaidi kiafya na kiuchumi.
“Ujue hii ni biashara kama biashara nyingine, watoto wa kike wanapaswa kuitazama kama fursa kwani huku unapata pesa lakini pia unaimarisha afya yako, hivyo waje kwa wingi.
“Kingine naomba wadhamini waje kwa wingi hususan kwetu wanawake, tunaomba tupate mlezi na wadau wengi waje upande wetu ili tusimame wenyewe na kufikia malengo na naamini tutafika tunapotaka,” anasema Pendo ambaye bado yupo kwenye menejimenti ya Kaseba.
MALENGO MAKUBWA
Kila mmoja ana malengo yake kwenye maisha na Pendo ameeleza malengo yake ni kusaidia watu wengi zaidi kuingia na kupata mafanikio kwenye mchezo wa ngumi pia anatamani kuchezesha mechi kubwa zaidi duniani akiwa refa.
“Kwanza natamani niwe na kituo changu chenye kila kitu kwa maana ya gym na kambi za kuwasaidia watu wengi, nataka siku moja niwainue zaidi wanawake na watoto kwenye mchezo huu.
“Kingine natamani nichezeshe mapambano makubwa, namaanisha yale ya mabondia wakubwa ulimwenguni, mfano wa mabondia wenye hadhi kama ya Mike Tyson na wengine,” anasimulia Pendo anasema licha ya kuwa refa bado anapiga mazoezi ya ngumi na inamsaidia kujilinda na watu wenye nia mbaya.
Huku akitumia msemo wa ‘Mtu akinizingua, tunazinguana.’ ambao hata Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewahi kuutumia katika hotuba zake.