Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Patauli: Bondia aliyegeuka mchungaji baada ya kumwaga damu za wapinzani wake ulingoni

66967 Bondia+pic

Tue, 16 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika maisha ya binadamu hakuna anayejua kesho yake itakuwa vipi kwasababu lolote linaweza kutokea katika mazingira ambayo hukutarajia.

Hali hiyo ndio imetokea kwa bondia nguli wa zamani wa uzito wa welter, Somwe Patauli ‘Okapi’. Bila shaka mashabiki wa ngumi wanakumbuka vyema jina la Patauli ambaye alikuwa maarufu katika kumbi za Relwe Gerezani, DDC Keko, DDC Magomeni Kondoa na Lang’ata Social Hall.

Patauli ambaye enzi zake aliwatoa jasho mabondia kama Chuku Dusso, Stanley Mabesi na wengine wengi maarufu kutoka nje ya nchi sasa ni mchungaji.

Si Patauli yule mbambe wa masumbwi ambaye alizoea kumwaga damu za mabondia ulingoni. Patauli sasa ni mtu mwingine tofauti ambaye hawezi kuzungumza kwa saa kadhaa pasipo kumshukuru Mungu kwa sala.

Ndani ya Kanisa la Huduma Huru na Ukombozi (JCMC) lililopo Kigamboni Tungi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, Patauli amekuwa akifanya kazi ya Mungu akiwa na viongozi wengine wa kanisa hilo akiwemo mkewe, Elikana.

Mkewe anasema alikutana na Patauli akiwa tayari ameacha maisha ya ubondia na kumrudia Mungu baada ya kusomea uchungaji.

Pia Soma

“Nilikuwa nasikia tu stori kwamba enzi anapigana alipewa jina la utani Okapi ambalo hilo jina kwa lugha ya kiswahili ni kisu, alilopewa kutokana na ukali wa ngumi zake ambazo zilifananishwa na kisu,” anasimulia Elikana.

Anasema walikutana na Patauli akiwa tayari ameokoka, japo alipenda kujua historia yake ya nyuma na alifanya hivyo baada ya kusikia siku moja mmoja wa mabondia waliowahi kucheza na Patauli akimuita kwa jina la Okapi.

“Katika matembezi ya kawaida nikiwa na Mchungaji, tulikutana na rafiki yake wa zamani, alimtania huku akimuita kwa jina la Okapi, mchungaji aliitika na yule rafiki yake alimkumbushia maisha ya ubondia, pale ndipo nilitaka kufuatilia zaidi,” anasema Elikana.

Mchungaji

Kabla ya simulizi yake, Patauli akiwa kanisani kwake Tungi, anaanza kwa sala ambayo ilichukua dakika 10.

Kisha akaanza kwa kusema, “niliposema nimeokoka kuna watu walifikiri nimechanganyikiwa. Kila mmoja alizungumza lake, wengine walisema tangu lini bondia akaokoka, wapo waliofikiri nimepatwa na janga lililonifanya nitangaze kuokoka.

“Nilipiga magoti nikamwambia Mungu ‘kama umeruhusu nifanye kazi yako, basi jina lako lihimidiwe’, sikutaka kurudi nilikotoka.”

Akikumbuka maisha yake ya ubondia, Patauli anasema kabla ya kuokoka amewahi kwenda klabu, amewahi kutumia kilevi, lakini hayo yalikuwa ni maisha nje ya ukristo ambayo hayana nafasi tena kwa sasa.

Huku akionyesha mikono yake minene, Patauli anasema, “mikono hii ndiyo ilitumika kumwaga damu ulingoni na mikono hii ndiyo inatumika kufanya kazi ya Mungu.

“Nilizoea kumwaga damu sikuona shida kumpasua mpinzani wangu ulingoni, hayo yalikuwa maisha ya kawaida kabisa kwangu, nilifurahia kuona mpinzani wangu amelala chini hajitambui kutokana na makonde au akivuja damu.”

Sababu ya kuokoka

Nilipata neema ya kuokoka na kuacha ngumi mwaka 1992, lakini baada ya muda nikarejea kwenye ngumi wakati nikiwa nimeokoka.

“Kwa miaka miwili ambayo nilirudi katika ngumi sikufanikiwa kila nilichofanya kilifeli kilikuwa kipindi kigumu kwangu niliona kama majaribu ndipo nikakata shauri nirudi kumtumika Mungu kwa moyo wangu wote,” anasema.

Anasema alirudi nyuma kwa kufuata mkumbo wa rafiki yake ambaye ni raia wa Uganda, ambaye naye alidai ameokoka lakini hakuwa ameacha maisha ya anasa, kwani licha ya kusema ameokoka alikwenda katika kumbi za starehe.

“Bahati mbaya nikajikuta nimeingia kwenye mkumbo na kurudi nyuma kiroho, kosa langu ilikuwa ni kukosa mafundisho baada ya kuokoka, lakini ilifikia hatua nikajikuta nayachukia maisha yangu,” anasimulia.

Anasema siku moja alikutana na mwinjilisti ambaye alimuuliza swali na kushindwa kulijibu, yule mwinjilisti alimsomea fungu katika Biblia ambalo lilimgusa na kujikuta akipata msukumo wa kuachana na anasa za dunia.

“Kipindi hicho nilikuwa nimeyachukia maisha yangu ambayo yalikuwa ya anasa, nilipata mguso ndipo nikafanya uamuzi sahihi. Nilikutana na mwinjilisti aliniuliza swali, nikashindwa kujibu, alinifungulia Biblia, ule msukumo ndio ukanifanya niokoke.”

Anasema alikata shauri kwenda kusomea uchungaji akaacha kila kitu na kutundika glovu, hakuna aliyeamini, marafiki zake walihisi amechanganyikiwa, lakini yeye aliamua kufanya kazi ya Mungu.

“Nilipomaliza masomo ya uchungaji, ndipo nilikutana na Elikana tukafunga ndoa na kuanza kufanya kazi ya Mungu,” anasema Patauli ambaye ni mchungaji kiongozi wa makanisa ya JCMC yaliyopo jijini Dar es Salaam.

“Haya ni makanisa ya Kipentekosti ambayo yako katika maeneo mbalimbali nchini na kwa Dar es Salaam mimi (Patauli) ndiye mchungaji kiongozi ,” anasimulia.

Anakumbuka wakati akicheza ngumi namna alivyokuwa akiwafurahisha Watanzania kwa kuwapiga wapinzani wake na kuwatoa damu.

“Nimekuwa bingwa wa Tanzania mara tatu na mwaka 1986 nilikuwa bondia wa saba wa uzani wa welter Afrika, lakini vyote hivyo niliamua kuviweka kando na kufanya kazi ya Mungu.”

Upinzani wake na Mabesi

Stanley Mabesi ‘Ninja’ ni bondia ambaye alikuwa akimtesa Patauli kutokana na ushindani waliokuwa wakionyesha kila walipokutana ulingoni.

“Pambano na Mabesi lilikuwa na ushindani kama ambavyo unaona kwa Simba na Yanga tulikuwa tukicheza ukumbi unajaa, tambo za pambano zinafanyika mwezi mmoja kabla,” anasimulia.

Anasema hawakuona taabu kutoana damu ulingoni na baada ya pambano kila mmoja anakwenda kuuguza majeraha, kwani ushindani wao ilikuwa ni zaidi ya vita.

“Ila upinzani ule ulikuwa ukiishia ulingoni, tukishuka ni marafiki wakubwa, uadui haupo tena na hakuna aliyekuwa akikubali kupigwa na mwenzake ukipigwa utafanya juu chini ili ulipe kisasi,” anasema Patauli.

Anasema zamani ngumi zilikuwa nzuri zenye ushindani na mabondia walicheza kwa mapenzi na kujitoa kuhakisha wanapata matokeo ndani na nje ya nchi.

“Wakati wa mazoezi yalikuwa ni mazoezi kwelikweli, nakumbuka tulikuwa tukifanya bila kusimamiwa na mtu, unatoka Kinondoni hadi Kunduchi kwa kukimbia na ukifika unafanya mazoezi na baada ya mazoezi unarudi hadi Kinondoni kwa kukikimbia ili kujenga pumzi,” anasema.

Apoteza fahamu miezi mitatu

Licha ya kufanya kazi ya uchungaji kwa sasa, Patauli anakumbuka moja ya pambano ambalo alipigwa kwa knockout (KO) na kupoteza fahamu kwa miezi mitatu.

“Ilikuwa ni ngumi kali ya kidevu, nilifanya uzembe kidogo sana ukanigharimu mpaka leo sikumbuki ngumi ile nilipigwaje, lakini ilinipata sawia kidevuni.”

Anasema alicheza na bondia kutoka Zimbabwe, Nelson Chungu ambaye alimtafuta baada ya kusikia rekodi yake wakati huo Patauli akiwa bondia namba saba kwa viwango Afrika.

“Alifanya juu chini ili apigane na mimi kwani ndiyo lilikuwa kusudio lake na baada ya pambano lile hakuwahi kucheza tena Tanzania,” anasimulia.

Anasema pambano lile lilifanyika Relwe Gerezani ambapo Patauli alipigwa KO raundi ya tatu hakuamka tena. “Ilikuwa ni kweli KO na ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kupigwa KO katika mechi zangu 36 nilizocheza.”

Hadi anaacha ngumi Patauli alikuwa ameshinda mara 29 (28 yalikuwa ya knockout), amepigwa mara tano (moja likiwa la knockout) na kutoka sare mara mbili. Anasema alipelekwa hospitali ya Muhimbili kwa matibabu, lakini alihangaika kwani ilimchukua muda kukaa sawa.

“Nilihangaika miezi mitatu hospitali kuna wakati nilikuwa sioni vizuri baada ya miezi mitatu nikawa sawa nikawa na uchu wa kulipa kisasi na kuanzia hapo kila bondia aliyejitokeza kupigana na mimi nilimpiga kwa KO.”

Patauli anazungumziaje kuhusu kulipa kisasi kwa wapinzani wake, fuatilia makala haya katika gazeti la leo.

Alikujaje Tanzania kucheza ngumi?

Patauli ambaye ni Mtanzania mwenye asili ni DR Congo anasema alikuja Tanzania baada ya mjomba wake ambaye ni Mcongo pia mwenye asili ya Tanzania aliyemtaja kwa jina moja la Kiki kumuunganisha na kocha wa ngumi aliyemtaja kwa jina moja la Dk Shein.

“Dk Shein alikuwa kocha maarufu wa ngumi, alinichukua na pambano langu la kwanza nilicheza Diamond Jubillee na bondia anaitwa Ally Mohamed aliyenipiga kwa pointi.

“Pambano lile lilinitambulisha rasmi kwenye ngumi Tanzania, mashabiki walinipenda na kukubali kipaji changu,” anasimulia.

Anasema aliingia kwenye ngumi miaka ya 1970 akiwa shuleni Lubumbashi ambako mmoja wa wanafunzi aliyekuwa baunsa shuleni waliyekuwa wakimuita Tembo alimnyang’anya vitu vyake.

“Nilienda kushtaki kwa anko wangu ambaye alikuwa mwalimu, alimwambia mwanafunzi mwingine anisaidie ili nipate vitu vyangu, mtu aliyenisaidia alivikomboa vitu vyangu kirahisi mno, nikashangaa nilimuuliza umewezaje?”

Anasema aliambiwa angekuwa bondia wala hakuna mtu ambaye angemsumbua, kuanzia hapo ndipo alipenda kuwa bondia, alianza mazoezi na kuja Tanzania alipounganishwa na kocha Shein aliyemuendeleza kipaji chake.

“Ngumi zilinipa heshima nje na ndani ya nchi ambapo pia zilifanya nifahamiane na watu wengi, viongozi mbalimbali wa Taifa ambao walikuwa karibu na mimi kila nilipokuwa nikiiwakilisha Tanzania kimataifa kwani nilikuwa hodari na shujaa ulingoni,” anasema.

Aligomea pambano kwa kuokoka

Mwaka mmoja kabla ya kuokoka, Patauli anasema walikwenda Uingereza kucheza pambano wakiwa na Lucas Msomba (marehemu) aliyekuwa akichezea uzani wa juu na Anthony Nyembele ambaye alikuwa akicheza uzani wa chini.

“Tulichukuliwa kwenda kucheza mapambano ya utangulizi la ubingwa Jumuiya ya Madola ambalo Mkenya, Modest Napuli alikuwa akigombea ubingwa na bondia wa nchi ile.

“Watanzani tulicheza vizuri wote, lakini matokeo yakapinduliwa tukaambiwa tumeshinda, ila baada ya pale nikawa nimepa ofa ya kwenda kucheza na kuishi Ufaransa na Stanley Mabesi akapata ofa ya kwenda Holland,” anasema.

Anasema mkataba wa ofa ile ulimkuta akiwa katika harakati za kuokoka, hakutaka kujiuliza mara mbilimbili akautolea nje.

“Ilikuwa nikaishi Ufaransa, niliahidiwa pesa nyingi na kuishi moja kwa moja Ufaransa, niligoma kwenda na Stanley Mabesi yeye akaenda Holland ambako anaishi mpaka sasa, binafsi sikutaka kurudi nyuma tena kwa kuwa nilishaamua kuokoka,” anasema.

Changamoto za uchungaji

Patauli anasema awali alipoingia katika kazi ya Mungu, changamoto ilikuwa kubwa lakini alijifananisha na Mtume Paulo.

“Paulo alipoamini wengi hawakumkubali kwa walifahamu huyu ametokea sehemu fulani, ndivyo ilikuwa kwangu.

“Wengine waliona kama nadhihaki, wengine hawakuamini na wengine mpaka sasa hawaamini, nilipiga magoti nikamwambia Mungu kama umeamua niifanye kazi yako, basi nitendee sawa na fadhili zako, nilifanya maombi ya toba kwani bila toba shetani anakurudisha nyuma.

“Kama nilivyosema, kabla ya kuokoka nilikuwa naishi maisha ya kidunia, kunywa bia kwangu sikuona tatizo, hivyo nilipookoka ilikuwa ni shida watu wengi kuamini,” anasema mwanamasumbwi huyo mstaafu.

Anasema wapo ambao walimjaribu imani yake baada ya kuokoka ili mradi tu waone imani yangu lakini waliona mabadiliko.

“… na baadhi yao wakaamini kwani watu wamefunguliwa kupitia mikono hii na mdomo huu tukishirikiana na mke wangu ambaye amekuwa msaada mkubwa.”

Mkewe anasema wamekuwa wakifanya kazi ya Mungu kwa furaha na amani na mara kwa mara wamekuwa wakienda pia kuhubiri injili mikoani.

“Historia ya mchungaji kwenye ngumi haikunipa shida, sikuwahi kufikiria kwamba ipo siku tabia ya ngumi labda ataiendeleza, tangu tumekuwa pamoja baada ya ndoa mpaka sasa sijaona dalili za kurudia mambo ya nyuma,” anasema mkewe.

“Hajawahi kukumbushia enzi kwenye ngumi, naamini Mungu amembadilisha na kumpa karama nyingine ya kiroho kuifanya kazi yake ambayo amekuwa akiitenda kwa uwezo wa Mungu,” anasema Elikana.

Patauli anasema alipookoka alilelewa kiroho kwenye kanisa la Deeper-life kwa kushirikiana na lile la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), linaloongozwa na mchungaji Zachary Kakobe.

“Nilikuzwa katika imani ya kiroho na misimamo ya kuachana na mambo ya kidunia, wamenisaidia kusimama katika imani, sina hamu wala sikusudii kurudi nyuma bali kuwabadilisha watu kupitia neno la Mungu,” anasema.

Chanzo: mwananchi.co.tz