Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Parker aharibu pambano la Joshua, Wilder

Wilder Vs Parker Parker aharibu pambano la AJ, Wilder

Sun, 24 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya bondia Mmarekani Deontay Wilder kupoteza pambano lake dhidi ya bondia kutoka New Zealand, Joseph Parker pambano lake na Antony Joshua huenda likaota mbawa, licha ya kwamba wawili hao bado wanatamani kuzichapa.

Tetesi zinadai mpango wa kwanza ulikuwa ni Wilder kucheza na Parker huku Joshua akicheza na Otto Williams na kama wote wangeshinda ndio wangekutana lakini aliyeshinda ni Joshua peke yake ambaye alimpiga Otto huku Wilder akipoteza pambano na yote mawili yalifanyika jijini Riyadh, Saudi Arabia, Jumamosi usiku.

Wilder mwenye umri wa miaka 38, alidaiwa huenda angechukua uamuzi wa kustaafu baada ya kupoteza pambano hilo, lakini aliibuka na kusema atarejea tena huku akiwaomba msamaha mashabiki wake kupitia video aliyoiweka kwenye ukurasa wake wa Instagram.

“Sijui nini kilitokea kusema ukweli, shabaha zangu hazikuwa sahihi, sikuwa naiachia mikono yangu jinsi nilivyotakiwa niachie. Kuna muda haya huwa yanatokea, bado nina furaha, samahani kama nimemuumiza mtu yeyote, lakini tutarudi tena imara na huo ndio uzuri wa jambo hili (ngumi).”

Kauli hizi za Wilder zimefifisha zile tetesi zilizochochewa na mahojiano yake baada ya pambano lake dhidi ya Parker aliyofanya na DAZN na alipoulizwa juu ya hatma yake alisema: “Tutaona kitakachotokea.”

Kwa upande wa Joshua yeye baada ya kuibuka na ushindi aliongea kauli zilizoonyesha bado anamtamani Wilder licha ya Mmarekani huyo kupoteza.

“Sikuwa naangalia. Nilikuwa nimewekeza kila kitu kwenye pambano langu, nimesikia kweli amepoteza, kwa hiyo ndio nini? Ninakwenda kujiandaa zaidi kwa sababu nina imani atarudi tena.”

Mwandaaji wa mapambano ya ngumi, Eddie Hearn kwa upande wake alithibitisha Joshua anaweza akacheza na Filip Hrgovic kwenye pambano lijalo kuwania ubingwa wa uzito wa juu wa dunia wa mkanda wa IBF kwa sababu Wilder ameshindwa kupata ushindi.

Akizungumza na talkSPORT, Hearn alisema: ”Tulisaini kupigana na Wilder, lakini amepoteza usiku wa leo. Labda ni baraka kwa sababu AJ (Joshua) anataka kuwa bingwa wa dunia mara tatu, hivyo pambano lijalo litaenda kuwa kati ya AJ na Hrgovic kwenye kuwania ubingwa wa dunia.

Miongoni mwa mastaa ambao huenda wameumizwa sana na kupoteza kwa Wilder ni Cristiano Ronaldo ambaye ni shabiki mkubwa wa bondia huyo na alikuwepo kwenye pambano na picha zilimwonyesha akiwa amekaa sambamba na bondia Conor McGregor.

Katika picha mbalimbali ziliwaonyesha wawili hao wakijadili juu ya kile kilichokuwa kinaendelea ulingoni na muda mwingi wa mchezo Wilder alionekana kuzidiwa.

Wachambuzi mbalimbali wanaeleza Wilder hakujiandaa vyema na pambano hili kwani wakati wa pambano alionekana mzito sana kwenye kufanya mashambulizi na aliruhusu sana mpinzani wake kupitisha ngumi.

Wilder amepigana mapambano 47, ameshinda 43, amepigwa mara tatu na sare moja.

Chanzo: Mwanaspoti