Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Papp staa wa ngumi aliyekufa akilaani serikali kumbania

Laszlo Papp Laszlo Papp

Fri, 14 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mchezo wa masumbwi ni tofauti na ule wa bao, karata au chesi kwani huhitaji mpiganaji kuwa na nguvu na ndio maana sio rahisi kwa mpiganaji kudumu muda mrefu.

Hii ni kwa sababu umri mkubwa humpunguzia nguvu na wengi huumia na kulazimika kustaafu mapema.

Vile vile wapo wanandondi ambao hata hapa kwetu tunaona wakiwa na majigambo ya kuonyesha bado wamo wakiwa na umri mkubwa na matokeo yake ni kuja kufedheheswa na kijana mdogo.

Lakini Laszlo Papp wa Hungary alionyesha maajabu kwa kung’ara kwa zaidi ya miaka 10 kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1940 hadi mwishoni mwa miaka ya 1950.

Aliweka historia ya Olimpiki ya kuwa mpiganaji wa kwanza kunyakua medali tatu za dhahabu za mashindano ya uzito wa kati (middleweight) katika kipindi cha miaka 12.

Kwanza alichukua ubingwa huo katika michezo ya 1948 iliyofanyika mjini London na alirudia kufanya hivyo hivyo katika michezo ya Olimpiki ya 1952 katika mji wa Helsinki, Finland.

Kwa mshangao wa wengi Papp alifanikiwa tena kutwaa medali hiyo ya dhahabu kwa mara ya tatu katika michezo ya Olimpiki ya 1956 iliyofanyika Melbourne, Australia.

Tokea Papp alipoweka rekodi ile ya kihistoria ni wana ndondi wawili tu, wote kutoka Cuba, Teofilo Stevenson na Felix Savon, ndio waliopata mafanikio ya aina hii katika historia ya Olimpiki.

Stevenson alifanya hivyo katika michezo ya Olimpiki ya kuanzia 1972 hadi ilipofanyika michezo ya 1980 na Savon alikuwa kidedea katika michezo ya 1992, 1996 na 2000.

Papp ambaye hadi hii leo anahesabika kama mmoja wa wapiganaji masumbwi wazuri duniani na wa kwanza wa aina yake kutoka Hungary pia alikuwa bingwa wa Ulaya mara mbili, kwanza katika middleweight kwenye mashindano ya 1949 yaliyofanyika Oslo, Norway. Baadaye alifanya hivyo katika kiwango cha light middleweight kule Milan, Italia, mwaka 1951.

Lakini ushindi mashuhuri na wa kuvutia zaidi kwa Papp katika Olimpiki ni wa kumtwanga mpiganaji maarufu wa zama zile, Jose Torres wa Marekani, ambaye baadaye alikuja kuwa bingwa wa dunia katika ndondi za kulipwa katika fainali za Olimpiki za 1956.

Papp aliweka rekodi ya kushinda mashindano 55 kwa kuwatoa wapinzani wake nje ya ulingo. Wengine walipoulizwa baada ya kuchapwa kama wanakusudia kuwa na pambano la marudiano na Papp walikasirika.

Mwanamasumbwi mmoja alipotajiwa pambano la marudiano alimwambia mwandishi wa habari aingie yeye kwenye ulingo badala yake na akiiaga dunia atasimamia mazishi yake. Mwingine alisema: “Hafikirii ndoto hio kwa vile kipigo alichokipata kilikuwa kibaya sana.”

Kila aliposhinda kwa pointi alikosa furaha na kusema mpinzani wake alimuudhi kwa vile alimpotezea muda katika ulingo kwa sababu alitaka amalize shughuli na kwenda kufanya mambo mengine.

Aliwahi kushauri mchezo wa ndondi usiamuliwe kwa pointi na badala yake wana ndondi wachapane mpaka mmoja asalimu amri mwenyewe.

Wataalamu wa michezo na hasa wanaojihusisha ndondi waliueleza ushauri wa huyu Mhangaria kama kauli ya kichaa aliyehusudu kujeruhi au kuuwa kwa kutumia makonde. Papp aliomba radhi kwa ile kauli yake na kusema alikuwa anafanya mzaha ili kufurahisha watu. Katika michezo yake yote Papp alionekana kutumia sana akili, lakini kauli zake zilikuwa kama za mtu ambaye waya mmoja kichwani ulikuwa umefyatuka.

Alikuwa anaporomosha makonde mazito, hasa kwa mkono wa kushoto ambao ulijulikana kama kitanzi cha machinjioni. Uzito wa baadhi ya makonde yake uliwashitua hata waamuzi na mmoja wao alijisahau na kumtaka aonewe huruma kwa kusukumiwa makonde laini kidogo.

Alikuwa mwana ndondi wa kwanza katika nchi za kikomunisti za zama zile kuruhusiwa kujiunga na ndondi za kulipwa 1957 na kuchukua ubingwa wa Ulaya wa middleweight 1962. Hata hivyo, katika mwaka 1965, serikali ya Hungary kutokana na shindikizo za Urusi ilimfutia kibali cha kupigana ngumi za kulipwa na kumkosesha nafasi ya kunyakuwa ubingwa wa dunia uliokuwa karibu kuutia mikononi.

Sababu iliyotolewa na Hungary ya kumzuia asiendelee kuwa mpiganaji wa kulipwa na kumzuia asitoke nje ya nchi ni kuwa ngumi za kulipwa zilikuwa haziruhusiwi na serikali ya kikomunisti ya Hungary kwa vile mfumo huo una harufu mbaya ya ubepari. Wakati ule Papp alikuwa hajashindwa hata katika pambano moja, bali alishinda mara 27 na kutoka sare mara 2 na alishinda mpambano 15 kwa kuwamaliza wapinzani kwa kuwatoa nje ya ulingo mapema (KO).

Orodha ndefu ya wapiganaji mashuhuri aliowashinda kwa kuwatoa katika mashindano raundi ya kwanza na ya pili ni pamoja na Valfrid Resko (Finland), Jean Welter (Luxembourg), Auguste Cavignac (Ubelgiji), Ivano Fontana (Italia) na John Wright (Uingereza).

Wengine ni Spider Webb (Marekani), Charlie Chase (Canada), Petar Spassoff (Bulgaria), Eladio Oscar Herrera (Argentina), Theunis Jacobus van Schalkwyk

(Afrika Kusini) Alberto Saenz (argentina). Katika mwaka 1989 Rais wa Shirikisho la Ndondi la Dunia (WBC), Jose Sulaiman, alimtunuku Papp tuzo ya kuwa “Mwana masumbwi bora wa ridhaa wa kulipwa wa wakati wote” na kumpa heshima ya ubingwa ya WBC.

Papp aliyezaliwa Hungary Machi 25, 1926 alichomoza kuwa mpiganaji masumbwi mzuri tangu akiwa na umri wa miaka 14 na alipotimiza miaka 18 wakati akifanya kazi ya karani ndani ya treni ya Shirika la Reli la Hungary. Mara nyingi alifanya mazoezi ndani ya mabahewa na alipotokea abiria kufanya uhuni Papp aliitwa kumuweka sawa.Ngumi zake mbili tatu au kibao kimoja ni dawa tosha ya kumtuliza abiria aliyejifanya mbabe wa sinema na kuwa tishio kwa abiria wenzake.

Wafanyakazi wa reli walikuwa na utani kwamba yeyote aliyefanya ukorofi aliambiwa aache kabla hajaitwa Papp kumshughulikia. Papp alipostaafu aliwatia unyonge mashabiki wa ndondi wa Hungary na nje, lakini wengi walifarijika alipochaguliwa kuwa kocha wa taifa wa ndondi wa Hungary, kazi aliyoifanya 1971 na 1972.

Alifariki dunia akiwa na maisha magumu Okt16, 2003 na aliwahi kusema katika miaka ya mwisho ya maisha yake kama angeruhusiwa na watawala wa kikomunisti kuwa mpiganaji wa kulipwa shida za maisha alizozipitia na tabu uzeeni zingepungua.

Chanzo: Mwanaspoti