Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pacquiao mstaafu wa ngumi anayezidi kupiga pesa

Man Pacquiao Manny Pacquiao

Mon, 9 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kwenye ngumi kwa sasa Antony Joshua na mabondia wengine wanatamba sana kuanzia ulingoni na nje ya ulingo kwa maana ya maisha, pesa ipo.

Hata hivyo, miaka 10 iliyopita ulimwengu wa masumbwi ulikuwa unatawaliwa na mafundi kama Floyd Mayweather na Manny Pacquiao.

Mastaa hao kwa sasa wamestaafu ingawa wamekuwa wakirudi ulingoni pale wanapopokea ofa nono.

Mastaa hao walivuna pesa nyingi sana kutokana na mchezo huo na Pacquiao licha ya kujiweka pembeni na mchezo huo na kuingia kwenye siasa, bado anaendelea kupiga pesa kutokana pia na miradi na kazi mbalimbali ikiwamo uigizaji na ni balozi wa kampuni mbalimbali. Cheki hapa utajiri wake wote.

ANAPIGAJE PESA

Anapiga pesa ndefu kutokana na ngumi na ndio zilizomfanya awe tajiri mkubwa na pambano lililowahi kumpa pesa ndefu zaidi ni dhidi ya Floyd Mayweather mwaka 2015 na alipata jumla ya Dola 130 milioni.

Mara ya mwisho kupanda ulingoni ni mwaka 2016 dhidi ya Adrien Broner na akakunja Dola 10 milioni.

Kijumla tangu aanze kupanda ulingoni hadi sasa, staa huyu amelipwa jumla ya Dola 446 milioni.

Pacquiao pia anapata pesa kupitia siasa na kwa sasa anahudumu kama seneta wa Ufilipino.

Pia amewahi kuonekana kwenye muvi na kwa mara ya kwanza alionekana kwenye muvi ya Tosh.0 na kumekuwa na tetesi huenda akaonekana kwenye muvi moja wapo Marekani.

Bondia huyu pia anapiga pesa kupitia ubalozi wa kampuni ya Cleto Reyes ambayo imekuwa ikimvalisha glovu kwenye mapambano yake.

Pia ni balozi wa Hewlett-Packard na ANTA ambayo ni kampuni ya mavazi kutoka China. Pia ni balozi wa I AM WORLDWIDE.

Kijumla anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 222 milioni.

MSAADA KWA JAMII

Ana taasisi yake iitwayo Manny Pacquiao Foundation inayotoa misaada kwa watu wa hali mbalimbali na wakati wa majanga.

Pia taasisi hiyo imekuwa ikikusanya pesa kupitia tovuti yao rasmi. Pacquiao hutoa misaada mbalimbali Ufilipino kama kusomesha watoto wasiojiweza na kugawa pia vyakula.

MIJENGO

Jamaa ana nyumba nyingi sana Ufilipino na Marekani na zinapatikana kwenye fukwe za bahari.

Amejenga maeneo ya Sarangani na mjengo wake upo ufukweni, nyingine ipo maeneo ya Pacman, nyingine ipo General Santos ambayo imepewa jina la utani la ‘White house’.

Pia nyumba zake za Marekani zinaripotiwa kupatikana maeneo ya Beverly Hills na Los Angeles.

Kwa pamoja staa huyu anadaiwa ana mijengo yenye thamani ya zaidi ya Dola 50 milioni.

NDINGA

1. Mitsubishi Pajero Sport-Dola 62,440

2. Porsche Cayenne-Dola 79,200

3. Ferrari 458 Italia-Dola 364,995

4. Cadillac Escalade- Dola $153,815

5. Hummer H2-Dola 73,500

6. Mercedes-Benz SL-Dola 109,900

7. Lincoln Navigator-Dola 84,660

BATA NA MAISHA BINAFSI

Yupo kwenye ndoa na Jinkee Pacquiao tangu mwaka 2000, ambaye amefanikiwa kuzaa naye watoto Emmanuel Pacquiao Jr, Michael Pacquiao, Israel Pacquiao na Mary Divine Grace Pacquiao.

Jamaa sio mtu wa bata sana na muda mwingi anapoonekana kwenye maeneo ya starehe huwa na familia yake.

Chanzo: Mwanaspoti