Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyuma ya pazia kifungo cha Mwakinyo

Mwakinyo Gloves .jpeg Bondia Hassan Mwakinyo

Wed, 11 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Licha ya Kamisheni ya Ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC), kutangaza kumfungia bondia Hassan Mwakinyo kwa mwaka mmoja, wabobezi wa masuala ya ngumi nchini wamesema kifungo hicho kitamuathiri bondia huyo nchini, lakini kimataifa bado ana uwezo wa kupigana.

Hata hivyo, rais wa TPBRC, Chaurembo Palasa ameliambia gazeti hili jana jioni kama bondia huyo atatumia ujanja wa kutumia kibali cha nchi nyingine kucheza kimataifa, atakuwa amekiuka kanuni na hatua zaidi dhidi yake zitachukuliwa.

Jana Katibu Mkuu wa TPBRC, George Silas alitangaza kufungiwa kwa bondia huyo na kutozwa faini ya Sh1 milioni kwa kile alichodai ni kujichukulia uamuzi bila kuheshimu mkataba kwenye pambano lake na Julius Indongo.

Alisema, bondia huyo anaweza kukata rufaa ndani ya siku saba, huku adhabu hizo zikiwa aziathiri uamuzi wa PAF, promota aliyeandaa pambano hilo kwenda mahakamani kwa hatua zaidi.

Mwakinyo amefungiwa, zikiwa zimepita siku kadhaa tangu alipogomea pambano na Indongo la Septemba 29, kwa kile alichodai promota alikiuka mkataba.

Baada ya vuta nikuvute ya pande zote, TPBRC iliomba vielelezo vya pande zote mbili, kabla ya jana kutoa uamuzi wa kumfungia Mwakinyo kuzichapa ndani na nje ya nchi kwa mwaka mmoja na kutakiwa kulipa faini ya Sh 1 milioni haraka kwenye kamisheni hiyo.

Hata hivyo, baadhi ya wabobezi wa masuala ya ngumi nchini walisema, adhabu hiyo itamuathiri Mwakinyo hapa nchini na si kimataifa kama ataamua kutumia leseni ya nchi nyingine.

Akitolea mfano wa bondia, Harrison Nii Lartey wa Ghana aliyewahi kufungiwa nchini mwake na TPBRC kumpa leseni ya Tanzania kwenda kuzichapa Russia na Abdulkerim Edilov mwaka 2021, bondia wa zamani aliyewahi kuongoza ngumi nchini alisema:

“Anaweza kutumia leseni ya nchi nyingine na akacheza bila wasiwasi, hizi ni ngumi za kulipwa ni kama biashara, utafungiwa huku unakwenda kucheza kwingine, hapa nchini adhabu itamuathiri ukizingatia hata mapromota wa hapa wengi ni kama wamemchoka, lakini akipata pambano kimataifa, akaamua kucheza anaweza kwa kutumia leseni ya nchi nyingine na TPBRC haitofanya chochote,” alisema kiongozi huyo aliyeomba hifadhi ya jina.

Aliyewahi kuwa promota wa Mwakinyo, Ally Mwazoa alisema adhabu hiyo itamuathiri bondia huyo kama Kamisheni itaamua kumuongezea kwa kukiuka taratibu.

“Kucheza kimataifa wakati wowote anaweza kwa kutumia kibali cha nchi nyingine, lakini Kamisheni kwa hapa nchini ndiyo imeshikilia mpini, akifanya hivyo inaweza kumkomoa kwa kumpa adhabu zaidi ya hiyo kwa hapa Tanzania, ni vyema akawa mpole tu,” alisema.

Palasa alisema ili Mwakinyo acheze kipindi hiki cha adhabu ni kuhama nchini, akifanya hivyo haitamzuia, lakini kama atatumia ujanja huo, watamsubiri atakaporudi adhabu itaendelea.

Chanzo: Mwanaspoti