Kila kitu freshi. Bondia wa zamani wa ngumi mchanganyiko ambye amenogewa na masumbwi ya kawaida, Francis Ngannou atapigana na Anthony Joshua katika pambano linaloelezwa kwamba litampa mkwanja mrefu bondia huyo mwenye asili ya Cameroon.
Pambano hilo limepangwa kufanyika Machi 8, Saudi Arabia na linatajwa pia kuwa ni pambano litakalomnufaissha zaidi AJ (34) ambaye ametoka kushinda dhidi ya Otto Wallin, mwaka jana.
Sasa ni kama amenogewa na masumbwi hayo na inaelezwa baada ya kuondoka na Dola 10 milioni kwenye pambano dhidi ya Tyson Fury, Ngannou atapiga tena mkwanja kama huo au zaidi kwenye pambano lijalo dhidi ya AJ.
Meneja wa bondia huyo, Marquel Martin ameliambia gazeti la Sports Business Journal kwamba Ngannou atapata zaidi ya Dola 10 milioni, lakini jarida la Forbes likatabiri pamoja na bonasi nyingine atakazopata, Mkameruni huyo atapata zaidi ya Dola 20 milioni, lakini likaenda mbali zaidi na kuandika atakayevuna pesa ndefu zaidi ni AJ.
Joshua alisaini dili la kupigana na Deontay Wilder na wawili hao walitarajiwa kuvuna Pauni 100 milioni. Hata hivyo, pambano liliota mbawa baada ya Wilder (38) kupata kichapo kutoka kwa Joseph Parker (31) na hivyo AJ baada ya kumchapa Otto ameamua kuangalia mwingine wa kupigana naye pambano lijalo.
Lakini sasa Ngannou anaonekana ndiye mtu sahihi wa kupigana na AJ na wawili hao watazichapa Machi 8, baada ya Joshua kuvujisha tarehe ya pambano.
Tangu Oktoba, mwaka jana, Ngannou (37) aliamua kuhamia kwenye ngumi za kawaida na pambano lake la kwanza dhidi ya bingwa wa uzito wa juu, Fury licha ya kupoteza kwa tofauti ya pointi za majaji, alionyesha kiwango kizuri ikiwamo kumwangusha mpinzani wake wakati wa pambano.