Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwakinyo kuwania mikanda miwili mabara

8064c0845b633815df30db1f713f26df Mwakinyo kuwania mikanda miwili mabara

Fri, 16 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BONDIA bingwa wa mabara wa uzito wa Superwelter, Hassan Mwakinyo atautetea mkanda wake wa Chama cha WBF Novemba 13 dhidi ya bondia wa Argentina, Jose Carlos Paz.

Pambano hilo na mengine ya utangulizi ambayo yamepewa jina la Dar Fight Night yameandaliwa na kampuni ya Jackson Group Sports. Mbali ya kutetea mkanda huo, Mwakinyo pia atawania ubingwa wa mabara wa uzito huohuo wa chama cha IBA.

Pambano hilo limepangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Dar es Salaam. Mkurugenzi wa The Jackson Group Sports, Kelvin Twissa jana alisema siku hiyo mabondia kutoka nchi tano watazichapa kumsindikiza Mwakinyo na Paz akiwamo aliyekuwa bingwa wa dunia wa WBC, Fatuma Zarika kutoka Kenya.

Twisa alisema Zarika atazichapa na Patience Mastara wa Zimbabwe na Zulfa Yusuph Macho atacheza na Alice Mbewe wa Zimbabwe. Pia siku hiyo, bondia Abdallah Pazi maarufu kwa jina la Dullah Mbabe atazipiga na Alex Kabangu wa DR Congo.

Alisema wameamua kuingia kwenye mchezo wa ngumi kutokana na kutambua vipaji vya mabondia mbalimbali hasa Mwakinyo ambaye anafanya vizuri katika mapambano yake.

Alisema kampuni hiyo chini ya udhamini wa Azam TV na Asas ina uzoefu mkubwa katika kuandaa matamasha, masoko na shughuli mbalimbali na kuahidi kufanya jambo la kihistoria hapa nchini. Kwa upande wake, Mwakinyo alisema kuwa hiyo ni fursa kwake na kuahidi kufanya vyema siku hiyo.

“Namshukuru Twisa na kampuni ya Jackson Group Sports ambao wameonesha nia ya kuubadili mchezo wa ngumi za kulipwa, sitawaangusha Watanzania,” alisema Mwakinyo.

Mwakilishi wa WBF nchini, Chatta Michael alisema Rais wa shirikisho hilo, Goldberg Howard atasimamia mapambano hayo.

Chanzo: habarileo.co.tz