Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwakinyo hana mpango na wazawa

Mwakinyo Hassan 3 Bondia Hassan Mwakinyp

Tue, 16 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kama kuna shabiki wa ndondi anatamani kumwona Hassan Mwakinyo akizichapa na mabondia wazawa, basi afute kabisa wazo hilo, kwani bondia huyo amesisitiza hana mpango huo na hataki.

Kabla ya pambano la Septemba, 2018 alipomchapa Sam Eggington kwa Technical Knock Out (TKO) nchini Marekani na kupanda kwenye ubora hadi nafasi ya 14 duniani uzani wa super welter, bondia huyo alicheza na mabondia wengi wazawa akiwamo Shaaban Kaoneka, mzawa pekee aliyemchapa.

Baada ya pambano na Eggington, Mwakinyo aliwachapa kwa TKO, Said Yazidu kisha Joseph Sinkala na hilo ndilo likawa pambano la mwisho kuzichapa na wazawa na tangu Oktoba 28, 2018 alipomchapa Sinkala, bondia huyo amepigana mapambano manane ya kimataifa.

Baadhi ya mapambano hayo ameyacheza ndani na nje ya nchi, akishinda saba akipoteza moja la Liam Smith nchini Uingereza.

"Kupigana na wazawa! Hapana sina mpango huo kabisa, huo ndio uamuzi wangu, kwa sasa," alisema Mwakinyo ambaye kwenye uzani wake ndiye kinara akifuatiwa na Meshack Mwankemwa na Mfaume Mfaume.

Japo bondia wa uzani wa middle au welter wanaweza kupandisha uzani au kushusha ili kuzichapa naye, kwenye uzani huo wanaotamba ni Pius Mpenda, Abdul Ubay na Mono Ally (middle), kwenye welter ni Idd Pialari, Hamis Maya na Abdallah Luanja.

Twaha Kiduku anayepigania uzani wa super middle kwa sasa, aliwahi kutaka kuzichapa na Mwakinyo na kusema kama pambano litatiki ataomba miezi minne ya kushusha uzito, hata hivyo, Mwakinyo amechomoa akisisitiza hana mpango wa kucheza na wazawa tena kwa miaka ya karibuni.

Bondia huyo hivi karibuni atasaini mkataba wa kucheza pambano la ubingwa, ambalo litakuwa ni pambano lake la tisa la kimataifa tangu 2018 alipomchapa Eggington na kuwa staa.

Chanzo: Mwanaspoti