Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwakinyo ashinda kwa pointi, Mfilipino kisiki

86515 Mwakinyo+pic Mwakinyo ashinda kwa pointi, Mfilipino kisiki

Sat, 30 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

PIGA huyo, uaaa... mmalize kabisa huyo arudi kwao.... zilikuwa ni kelele za mashabiki wa ngumi waliofurika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kumshangilia bondia Hassan Mwakinyo akizichapa na Arnel Tinampay kutoka Ufilipino.

Katika pambano hilo kali na ambalo limeacha maswali kwa baadhi ya mashabiki kutoonekana kuridhika na ushindi wa pointi wa Mwakinyo, ambapo walitamani kuona akishinda kwa KO.

Hata hivyo, pambano hilo la Super Welter lilikuwa gumu kutokana na Tinampay kuwa mgumu na kumkabili Mwakinyo hadi kumaliza raundi zote 10 na majaji kuamua mshindi kwa pointi.

Jaji namba moja alitoa ushindi wa pointi 98-92, jaji namba mbili alitoa pointi 97-93 kwa Mwakinyo na jaji namba tatu alitoa sare ya pointi 96-96.

Katika pambano hilo lililoanza saa 5.25 usiku jana, Mwakinyo alilazimika kusubiri hadi raundi ya tatu kuwanyanyua mashabiki baada ya kumsukumia makonde mazito Tinampay. Katika raundi hiyo, Mwakinyo akishangiliwa na mamia ya mashabiki waliofurika uwanjani, alionyesha uhai mkubwa na kiu ya mashabiki ilikuwa ni kummaliza mapema mpinzani wake.

Katika pambano hilo, Mfilipino ndiye alikuwa wa kwanza kurusha ngumi baada ya mwamuzi Emmanuel Mlundwa kulianzisha tu, ambapo ilimkuta Mwakinyo mbavuni kabla ya kuanza kujibu mapigo.

Katika raundi hiyo, Tinampay aliganda kwa sekunde mbili akimkodolea macho Mwakinyo katikati ya mchezo.

Raundi ya pili, Tinampay aliendeleza mashambulizi huku akicheza kwa stahili ya kutorudi nyuma na kumbananisha Mwakinyo kwenye kamba, lakini alijibu Mtanzania huyo alijibu mapigo dakika ya mwisho ya raundi hiyo kabla ya kurudi kwa kasi raundi ya tatu.

Raundi ya nne, Mfilipino alionywa na mwamuzi baada ya kupiga ngumi chini ya mkanda, baada ya kuchezea kipigo katika raundi hiyo.

Katika raundi ya tano, Mwakinyo alianza kwa kupiga ngumi ngumi nne mfululuzo za kudokoa na ambazo zilimkuta kwenye paji la uso naye bila kuchelewa akajibu mapigo.

Dakika ya pili ya raundi hiyo, Tinampay alitumia mbinu ya kumbananisha Mwakinyo kwenye kona na kumshambulia, lakini alijihami na kujibu mashambulizi kwa kupiga ngumi zilizompata sawia Tinampay.

Tinampay, ambaye alionekana kuwa na nguvu alimpiga ngumi za tumbo mfululizo Mwakinyo raundi ya sita kwa lengo la kumkata pumzi, lakini Mwakinyo alionekana kumpuuza huku akitikisa kichwa kuonyesha ishara kwamba, hazijamuingia.

Kwenye raundi ya saba, Mwakinyo alikwenda chini lakini si kwa konde bali aliteleza na kunyanyuka kisha kuendelea huku akicheza kwa kujihami na kumpa Tinampay fursa ya kushambulia.

Raundi ya nane, Tinampay alianza kwa kasi na kumbananisha Mwakinyo kwenye kona, ingawa Mtanzania huyo alitumia mbinu ya kumkimbia huku akijibu mashambulizi kwa kustukiza na Tinampay.

Raundi ya tisa, Tinampay aliendelea kumshambulia Mwakinyo ambaye alionekana kama kulewa huku maelfu ya mashabiki wakiongozwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe wakiwa kimya huku wachache wakipiga kelele kumtaka Mwakinyo amkimbie mpinzani wake ili amalize raundi hiyo.

Raundi ya 10, Mwakinyo aliwanyanyua mashabiki uwanjani hapo baada ya kumshambulia mfululizo Tinampay, ambaye kuna wakati alionyesha ishara ya kuzikubali kwa kusimama wima katikati ya mchezo na kutikisa kichwa kwa sekunde kadhaa na kuendelea kujibu mashambulizi kwa kushtukiza.

Baada ya mchezo huo, Mwakinyo alisema amepata changamoto kubwa kusaka ushindi katika pambano hilo, lakini umati uliofurika kulishuhudia ndiyo ulimfanya kupambana zaidi ili kushinda.

 

Mfaume apeleka kilio huko Manzese

Raundi ya nane na ya mwisho imembeba bondia Mfaume Mfaume dhidi ya Keis Ally katika pambano la utangulizi kusindikiza lile la Hassan Mwakinyo na Arnel Tinampay kwenye Uwanja Uhuru, Dar es Salaam.

Pambano hilo lililokuwa na ushindani liliwakutanisha mabondia wa kambi ya Manzese na Mabibo, Dar es Salaam lilimalizika kwa mashabiki wa Mfaume kutoka Mabibo kutoka kifua mbele ikiwa ni mara ya tatu mfululizo bondia huyo anawachapa wale wa Manzese.

Ngumi kali ya kulia iliyompata sawia Keis usoni na kumpeleka chini ilitosha kumpa ushindi Mfaume, ambaye alibanwa raundi ya kwanza, ya nne na ya saba na Keis huku kocha wa Keis, Christopher Mzazi  akiingia ulingoni raundi ya saba wakati wa mapumziko na kushangilia akiamini ameshinda.

Mfaume alicheza kwa ustadi mkubwa raundi ya pili, tatu na ya tano kabla ya kumpeleka chini Keis raundi ya nane kitendo kilichoamsha shangwe kwa mashabiki wa bondia huyo anayenolewa na Rama Jaha.

Baada ya kumpeleka chini Keis, Mfaume alionyesha ishara ya kumkebehi kwa kucheka huku akimfuata kabla ya mwamuzi, Anthony Rutha kumuonya kwa kumtaka kurejea kwenye kona yake huku Keis akinyanyuka fasta na kuendelea na mpambano.

Majaji, Neneko Abdallah na Pendo Njau walitoa pointi 78-74 kila mmoja wakati Emmanuel Mlundwa akitoa ushindi wa pointi 79-72 kwa Mfaume, ambaye alitwaa ushindi kwa pointi za majaji 3-0.

Chanzo: mwananchi.co.tz