Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwakinyo aibukia ulingoni Zanzibar

Hassan Mwakinyo Jrrrr Bondia Hassan Mwakinyo

Wed, 8 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Licha ya kufungiwa mwaka mmoja na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania Bara (TPBRC), bondia Hassan Mwakinyo ameibukia visiwani Zanzibar na anatarajiwa kucheza Novemba 24, pambano la kimataifa.

Japo Mwakinyo alipotafutwa juzi na jana simu yake haikupokelewa, Kamisheni ya ngumi za Kulipwa Zanzibar imelithibitishia Mwanaspoti, imepokea maombi ya bondia huyo akitaka kuwa bondia wa visiwa hivyo na tayari kuna promota (ilimtaja) aliyemwandalia pambano ambalo liko kwenye ratiba ya kupigwa mwisho wa mwezi huu.

“Ni kweli Mwakinyo aliomba kuwa bondia wa huku na kuna pambano anatakiwa apigane Novemba 24 pale Ngome kongwe,” alisema mmoja wa viongozi wa juu wa kamisheni hiyo aliyeomba hifadhi ya jina.

Alisema pambano hilo ndilo litakuwa kubwa na bondia huyo atapigana na Mmalawi, Hannock Phiri, likisindikizwa na mengine sita.

“Pambano lipo, kinachochelewesha kutangazwa ni kesi yake ya Bara ambayo waziri wa michezo wa huku aliagiza baraza la huku liifuatilie kujua nini kinaendelea ndipo litangazwe,” alisema kiongozi huyo.

Katibu mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha jana alipotafutwa simu yake iliita bila kupokelewa wakati yule wa Zanzibar (BTMZ), Said Marine akikiri kuwepo kwa pambano hilo.

“Lipo Novemba 24, lakini tunasubiri maelekezo kutoka kwa wenzetu wa BMT, ninachokifahamu ni Mwakinyo alifungua kesi kupinga adhabu aliyopewa na TPBRC na jana (juzi) ndiyo ilisikilizwa na baraza la Bara.

“Tunasubiri taarifa kutoka kwao, wakimruhusu basi atapigana hiyo Novemba 24 hapa Zanzibar,” alisema Marine.

Rais wa TPBRC, Chaurembo Palasa alipoulizwa kuhusu bondia huyo kuomba kupigania visiwani Zanzibar na kutambulika kama bondia wa visiwa hivyo alijibu kwa kifupi huo ni uamuzi wake.

“Aende kokote anapotaka,” alisema Palasa bila kufafanua kama adhabu itaongezeka kama atacheza kwa kupewa kibali na kamisheni nyingine, ingawa taratibu za ngumi za kulipwa, bondia anaweza kutumia kibali cha nchi nyingine yoyote na kupigana popote kama amefungiwa nchini kwake.

TPBRC pia iliwahi kutoa kibali kwa bondia aliyefugiwa Ghana akaenda kupigana Ulaya, ingawa taratibu hizo zinataka bondia huyo kulipia asilimia kadhaa ya pesa atakayoingiza kwenye nchi hiyo, kwa nchini TPBRC hutoza asilimia tano.

Wiki kadhaa zilizopita TPBRC ilimfungia mwaka mmoja Mwakinyo na kumtaka kulipa faini ya Sh1 milioni kwa madai ya alikiuka mkataba wa pambano lake na Julius Indongo lililoandaliwa na kampuni ya PAF Promotion.

Baada ya adhabu hiyo, PAF pia ilieleza kumfungulia shauri la madai Mwakinyo ambalo linatarajiwa kutajwa kwa mara ya kwanza Novemba 13, katika Mahakama ya Kisutu.

Katika madai hayo, wametaka Mwakinyo aombe radhi kwa kugoma kupanda ulingoni Septemba 29 na kutoa taarifa za uongo kupitia vyombo vya habari sanjari na kulipa fidia Sh142.5 milioni kama hasara ya kukosa mapato.

Madai hayo yanataka pia arejeshe Sh7.4 milioni alizopokea, kulipa Sh8 milioni za gharama ya ukumbi, Sh1.2 milioni za malazi ya mpinzani wake na Sh3.8 milioni za gharama za tiketi za ndege za mpinzani na wasaidizi wake.

Kabla ya shauri hili, bondia huyo aliliambia Mwanaspoti, promota wa pambano hilo alikiuka makubaliano yaliyosababisha kugomea pambano hilo na kurejea kwao Tanga akitokea Dar es Salaam saa chache kabla ya pambano.

Kuhusu kufunguliwa shauri la madai, Mwakinyo hivi karibuni aliliambia gazeti hili kwa kifupi watakutana mahakamani.

Hata hivyo, kama BMT itampa baraka za kucheza ngumi Zanzibar, bondia huyo atatakiwa ashinde ili kujinasua kuporomoka zaidi kwenye renki ambako sasa ni wa 106 kati ya mabondia 1,912 duniani kwenye uzani wa super welter.

Mwakinyo aliyepata umaarufu 2018 alipomchapa Sam Eggington na kupanda hadi nafasi ya 14 duniani amekuwa na panda shuka hadi sasa akiporomoka zaidi.

Phiri yeye ni wa 178 kati 2,092 duniani kwenye uzani wa welter, hivyo mmoja kati yao atatakiwa kupunguza au kuongeza kilo ili wazichape Novemba 24 kama pambano litatiki, wote ni namba moja kwenye uzani wao kwenye nchi zao.

Chanzo: Mwanaspoti