Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelekeza bondia maarufu nchini Hassan Mwakinyo, kupelekewa wito wa kufika mahakamani kupitia gazeti la Mwananchi kufuatia kesi ya madai inayomkabili mahakamani hapo.
Uamuzi huo umetolewa leo Novemba 13, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Amiri Msumi, baada ya Mwakinyo kukataa kupokea hati ya wito wa kufika mahakamani iliyowasilishwa kwake na msambaza nyaraka wa Mahakama.
Mwakinyo alifunguliwa kesi ya madai na kampuni ya Kampuni ya PAF Promotion, ambapo pamoja na mambo mengine iliwasilisha madai manane mahakamani hapo, likiwemo la kumtaka bondi huyo kuilipa Sh 150 milioni kampuni hiyo ikiwa ni madhara ya jumla waliopata baada ya bondia huyo kushindwa kupanda ulingoni tofauti na mkataba wake aliosaini.
Kampuni hiyo imemfungulia Mwakinyo kesi hiyo baada ya kushindwa kupanda ulingoni katika pambano lililoandaliwa na kampuni hiyo, lililopangwa kufanyika Septemba 29, 2023 jijini hapa kwa kile alichonukuliwa akisema ni waratibu hao kukiuka masharti ya makubaliano.
Awali, Wakili anayewakilisha kampuni hiyo, Herry Kauki alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama bondia huyo amepewa wito wa kufika mahakamani.
Wakili Kauli alidai kuwa wao walipeleka wito Serikali ya mtaa, lakini Mwakinyo aligomea kupokea wito wa kufika mahakamani.
Na pia walimtuma msambaza nyaraka wa Mahakama maalumu kwa ajili ya kupeleka viapo, pia Mwakinyo aligoma kupokea wito huo, hivyo msambaza nyaraka za mahakama huyo alikula kiapo kuelezea haya maelezo kuwa amepeleka wito lakini Mwakinyo amekataa kusaini wala kupokea wito huo.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Msumi alitoa amri kwa upande wa mlalamikaji ambaye ni kampuni hiyo kutangaza wito wa Mahakama katika gazeti la Mwananchi, ukimtaka Mwakinyo kufika mahakamani hapo Novemba 20, 2023 ili kusikiliza kesi yake.
Amri hiyo inaelekeza kuwa iwapo Mwakinyo atakaidi wito huo uliotolewa na Mahakama hiyo, hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yake.
Katika kesi hiyo ya madai namba 227 ya mwaka 2023, Kampuni hiyo imeiomba Mahakama, kwanza itamke kwamba bondia huyo amevunja mkataba wa kupigana.
Pili inaomba Mahakama kumtaka Mwakinyo aombe radhi kwa kuichafua kutokana na kutoa taarifa za uongo kupitia Vyombo vya Habari alivyotumia kuichafua Kampuni na Wakurugenzi wake.
Tatu, PAF inaomba ilipwe fidia ya Sh 142 milioni kutokana na hasara ya kukosa mapato iliyotegemea kutoka kwa wadhamini.
Nne, inaomba Mahakama imwamuru Mwakinyo arejeshe Dola za Marekani 3,000 alizopewa kuelekea pambano hilo alilotakiwa kupigana.
Tano, PAF inaomba kurejeshewa Sh8 milioni yakiwa ni malipo ya kulipia ukumbi.
Sita, inaomba kurejeshewa Sh 1.2 milioni ikiwa ni gharama za malazi ya mpinzani wa bondia huyo.
Saba, kampuni hiyo, inaomba Mwakinyo kurejeshewa Sh 3.8 milioni ambazo ni gharama za tiketi za ndege za mpinzani wake pamoja na wasaidizi wake.
Nane, PAF inaomba Mwakinyo kuilipa kampuni hiyo jumla ya Sh 150 milioni ikiwa ni madhara ya jumla waliopata baada ya bondia huyo kushindwa kupanda ulingoni tofauti na mkataba wake aliosaini.