Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwakinyo: Nilikwenda Uingereza kwa kuungaunga

17450 Mwakinyo+picc TanzaniaWeb

Sun, 16 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Bondia Hassan Mwakinyo jana alitua bungeni na mkanda wake, kisha akatoa siri nzito ya safari yake nchini Uingereza kwamba alikwenda kama mwizi.

Septemba 8, Mwakinyo aliibua shangwe kwa Watanzania baada ya kumchapa bondia Mwingereza, Sam Eggington kwa technical knockount (TKO) katika raundi ya pili mjini Birmingham, Uingereza.

Hivi karibuni akijibu swali la nyongeza la Ali Saleh (Malindi-CUF) bungeni mjini hapa, waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema Serikali inafahamu kuhusu safari ya mwanamasumbwi huyo na ilikuwa ikifuatilia kwa karibu pambano hilo.

Soma zaidi: Mtanzania aingia anga za Pacquiao

“Kwanza naomba radhi kwa Watanzania na wanamichezo wote kutokana na kauli yangu baada ya mkalimani wangu kule Uingereza,” alisema Mwakinyo jana.

“Lakini nakanusha vikali kuwa mimi Mwakinyo sikupata sapoti yoyote kwa mtu yeyote hata katika safari yangu, ikumbukwe kuwa niliondoka kama mwizi na hata nauli ya kwenda nilikopa hela ya mwanafunzi.”

Soma zaidi: Mtanzania atua mikononi mwa Mayweather

Alisema kibali cha kuondoka kwake nchini kilikuwa cha shida na hakuna mtu ambaye alisimama upande wake kumsaidia zaidi ya rafiki yake aliyemtaja kwa jina la Mbarouk Athuman.

Bondia huyo alisema kulikuwa na mizengwe ambayo ilitaka kumkatisha tamaa na ndipo akaamua kutumia alizoziita kuwa njia za panya hadi akafanikisha safari yake.

Alisema alipotua Uingereza aliamua kuuvaa Utanzania na alijua anapigana kwa ajili ya Taifa na si yeye kama yeye.

Alisema kuwa anatamani kukutana na Rais John Magufuli ili amweleze namna ambavyo mabondia wengi wanakosa fursa kutokana na urasimu uliopo na masharti yanavyowakwamisha kusafiri.

Apata mikataba mitatu nje

Mwakinyo alisema baada ya kumaliza pambano hilo alilofanya vizuri, amekuwa akifuatiliwa kwa karibu na kampuni mbalimbali za uwakala kutoka nje ya nchi na hadi jana alikuwa amewekewa mezani mikataba mitatu tofauti kutoka nchini Uingereza.

Hata hivyo, alisema hawezi kusaini mikataba hiyo kwa kuwa anaamini kuwa Tanzania haijashindwa, hivyo hatafanya papara kusaini mikataba hiyo.

Alisema badala yake atajipa muda wa kusubiri kuona kama kuna kampuni za hapa nchini zitakazoingia naye mikataba itakayokuwa na masilahi zaidi kwake na kwa Taifa kwa ujumla, akiamini zitamsaidia kujitangaza huku akibeba bendera ya Tanzania.

Waziri Mkuu amuita nyumbani

Jana Spika wa Bunge, Job Ndugai alimkaribisha Mwakinyo bungeni na kuomba kukutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ili ampe mkono.

Jambo hilo lilitekelezwa nje ya Ukumbi wa Bunge ambapo Waziri Mkuu alizungumza naye kisha akamuagiza mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Bakari ampeleke nyumbani kwake saa 9 alasiri.

Baada ya tangazo la Spika, Mbunge wa Sumbawanga, Hilaly Aeshi aliomba mwongozo akitaka kila mbunge amchangie bondia huyo Sh20,000, kiwango ambacho kilikubaliwa na wabunge wote.

Katibu wa Bunge

Licha ya kuwa ukumbi wa Bunge ulikuwa na wabunge wachache, katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai alisema watakaochangia ni 393 bila ya kujali waliopo au hawapo.

“Bila shaka umesikia kuwa Bunge limeazimia, hii ina maana kuwa wabunge wote watachanga maana imetolewa ndani ya Bunge na wote wameafiki, kwa hiyo kiasi kitakatwa kwa wabunge 393,” alisema.

Kwa hali hiyo, mbali ya zawadi binafsi za wabunge mmoja mmoja, Mwakinyo atakuwa ameondoka na kitita cha Sh7,860,000. Bondia huyo pia amepata fedha nyingine Dola 3,000 ambazo ni zaidi ya Sh 6 milioni za Kitanzania.

Mbarouk Athuman

Rafiki wa bondia huyo ambaye alianza kumsifia hata alipokuwa Uingereza, Athuman alimzungumzia bondia huyo akisema kuwa ni mwenye kipaji na ni mtu wa kujituma zaidi, lakini hana msaada kutoka kwa mtu yeyote

Soma zaidi: Fedha alizovuna bondia Hassan Mwakinyo hizi hapa

Athuman alisema kwamba eneo analofanyia mazoezi bondia huyo ni duni lililopo katika mazingira ambayo hayakubaliki, hivyo akaomba watu wenye uwezo wajitokeze kumwendeleza kwa kuwa anaweza kufanya makubwa katika medani ya masumbwi.

Wabunge na picha

Katika lango la Bunge jana kulikuwa na msururu mrefu wa wabunge ambao walikuwa wakipiga picha na bondia huyo huku kila mmoja akitaka kuzungumza naye na kumpongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya.

Mbali na wabunge, waandishi wa habari na watumishi wengine wa Bunge pia walipanga foleni wakitaka kuzungumza na kupiga naye picha, hali iliyowalazimu baadhi ya watu kumtoa kwa nguvu na kumpeleka katika mgahawa wa Bunge.

Soma zaidi: Wabunge kumjaza mamilioni Mwakinyo

Chanzo: mwananchi.co.tz