Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwakinyo, Ibra Class waporomoka viwango

Bondia Hassan Mwakinyo Hassan Mwakinyo

Tue, 4 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mabondia Ibrahim Class na Hassan Mwakinyo wameporomoka kwenye ubora nchini na kupoteza nusu nyota kila mmoja katika viwango vya kimataifa.

Mwakinyo aliyewahi kuwa bondia namba moja Tanzania kwenye kila uzani (pound for pound) na Class aliyewahi kuwa namba mbili wameporomoka na sasa wanakamata nafasi ya tatu na nne nchini.

Anguko hilo limetokana na kutopigana kwa muda mrefu, huku kwenye nyota ambazo miezi ya karibuni wote walikuwa na nyota tatu, kila mmoja amepoteza nusu nyota.

Kwa mujibu wa mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (Boxrec), mabondia hao sasa wana nyota mbili na nusu kati ya tano, ikumbukwe Mwakinyo aliwahi kufikisha nyota nne baada ya kumchapa Sam Eggington 2018. Kuporomoka kwa mabondia hao kumewapandisha Tony Rashid na Fadhil Majiha ambao sasa ndiyo wako kileleni kwenye pound for pound ya Tanzania.

Tony bondia namba moja ameongeza nyota, sasa ana nyota tatu na nusu, akihitaji nyingine moja na nusu ili kuingia kwenye orodha ya mabondia viara wa dunia wanaomiliki nyota tano.

Majiha aliyewahi kucheza pambano la utangulizi kumsindikiza Manny Pacquiao miaka ya nyuma nchini China yeye amefikisha nyota tatu akiwapiku Mwakinyo na Class nusu nyota.

Bondia said Chino amehitimisha tano bora ya Tanzania kwenye kila uzani, wakati Twaha ‘Kiduku’ Kassim akitajwa kwenye nafasi ya sita, akifuatiwa na Nasibu Ramadhan, Salim ‘Mtango’ Jengo, George Bonabucha na Juma Choki amehitimisha 10 bora ya Tanzania.

Mabondia wengine maarufu nchini na nafasi zao kwenye mabano ni Seleman Kidunda (12) Idd Pialari (16), Abdallah ‘Dullah Mbabe’ Pazi (19), Mfaume Mfaume (36), Francis Miyeyusho (39) na Awadh Tamim (43).

Chanzo: Mwanaspoti