Mabingwa wa zamani wa mataji ya Chama cha Ndondi Afrika (ABU) Rayton “Boom Boom” Okwiri na Daniel Wanyonyi wameapa kunyamazisha wapinzani kutoka Tanzania kwenye mapigano yasiyo ya kuwania taji jijini Nairobi, mnamo Jumamosi.
Okwiri aliye na ushindi wa mara nane, sare moja na amepoteza mara moja, atalimana na Shabani Ndaro, ambaye hajapoteza mapigano yake matano. Watalimana katika pambano la raundi tano la uzani wa kati katika Jumba la Mikutano la KICC. Pigano kati ya Okwiri na Ndaro ndilo pambano la siku kwenye menyu ya mapigano 11.
Wanyonyi, ambaye ana rekodi ya 27-14-2, 22 KO, atarushiana makonde na domokaya Karim “Mtu Kazi” Mandonga (3-3-1) katika raundi 10 za pigano la uzani wa kati wa ‘Super’.
“Ndaro ajiandae kulia kwa sababu nitamrudisha darasani ajifunze masumbwi. Hatakamlisha raundi zote. Nimemuona akicheza na bila ya tashwishi nasema kuwa hayuko ligi yangu,” aliapa Okwiri, 36.
“Nataka kuwapa mashabiki wangu burudani kwa kuadhibu Mtanzania huyo…Nitakuja na gari la wagonjwa kumpeleka hospitali baada ya kumchapa,” alisema Okwiri ambaye amekuwa akifanyia mazoezi katika ukumbi wa Kaloleni na Advanced chini ya makocha David Kiilu na Dan Shisia.
Mara ya mwisho afisa huyo wa Magereza alicheza nyumbani ilikuwa Desemba 2019 alipohifadhi taji la ABU kwa kumzima Augustine Matata kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika ukumbi wa Charter mjini Nairobi.
Hata hivyo, alionja kichapo cha kwanza Juni 2022 mjini Johannesburg dhidi ya mkazi wa Afrika Kusini Emmany Kalombo kutoka DRC. Okwiri alisalimu amri katika raundi ya saba kati ya 12 zilizopangwa baada ya kuumia kidole cha gumba cha mkono wa kulia katika pigano la taji la Shirikisho la Ndondi ya Kimataifa (IBF).
Wanyonyi alisema ameruhusu Mandonga kupiga mdomo anavyotaka tangu awasili Nairobi Jumatano, lakini maneno yataisha kinywani Jumamosi.
“Sioni kibarua chochote mbele yangu Jumamosi. Mandonga hatapumua wala kuonyesha mbinu anazojigamba nazo,” alisema Wanyonyi, akidai kuwa amepigana na mabondia wazuri kuliko Mandonga.
“Wakenya wasiwe na wasiwasi,” aliapa Wanyonyi ambaye amekuwa akifanyia mazoezi yake ukumbini Palpal mtaani Eastleigh chini ya kocha Julius Odhiambo.
Mandonga amevuma kwenye mitandao ya kijamii kwa majivuno yake katika mahojiano ya kabla ya baada ya mapigano.
Pia, amefanya mazoezi ya kuingiza wapinzani baridi kwa kupiga miti ngumi mikono mitupu na kukimbia akiwa amebeba magogo ya miti.
“Mimi hushinda mapigano yangu kwa kuzungumza na pia ulingoni. Nimeleta vita kwa Wanyonyi na hakuna mlango atatumia kutoroka,” aliapa Mandonga.