Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfaume apeleka kilio huko Manzese

86512 Mfaume+pic Mfaume apeleka kilio huko Manzese

Sat, 30 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Raundi ya nane na ya mwisho imembeba bondia Mfaume Mfaume dhidi ya Keis Ally katika pambano la utangulizi kusindikiza lile la Hassan Mwakinyo na Arnel Tinampay kwenye Uwanja Uhuru, Dar es Salaam.

Pambano hilo lililokuwa na ushindani liliwakutanisha mabondia wa kambi ya Manzese na Mabibo, Dar es Salaam lilimalizika kwa mashabiki wa Mfaume kutoka Mabibo kutoka kifua mbele ikiwa ni mara ya tatu mfululizo bondia huyo anawachapa wale wa Manzese.

Ngumi kali ya kulia iliyompata sawia Keis usoni na kumpeleka chini ilitosha kumpa ushindi Mfaume, ambaye alibanwa raundi ya kwanza, ya nne na ya saba na Keis huku kocha wa Keis, Christopher Mzazi  akiingia ulingoni raundi ya saba wakati wa mapumziko na kushangilia akiamini ameshinda.

Mfaume alicheza kwa ustadi mkubwa raundi ya pili, tatu na ya tano kabla ya kumpeleka chini Keis raundi ya nane kitendo kilichoamsha shangwe kwa mashabiki wa bondia huyo anayenolewa na Rama Jaha.

Baada ya kumpeleka chini Keis, Mfaume alionyesha ishara ya kumkebehi kwa kucheka huku akimfuata kabla ya mwamuzi, Anthony Rutha kumuonya kwa kumtaka kurejea kwenye kona yake huku Keis akinyanyuka fasta na kuendelea na mpambano.

Majaji, Neneko Abdallah na Pendo Njau walitoa pointi 78-74 kila mmoja wakati Emmanuel Mlundwa akitoa ushindi wa pointi 79-72 kwa Mfaume, ambaye alitwaa ushindi kwa pointi za majaji 3-0.

Chanzo: mwananchi.co.tz