Nyota wa mchezo wa Ultimate Fighting Championship (UFC) Conor McGregor amethibitisha hamu yake ya kutaka kucheza mchezo mwingine wa masumbwi akidai kwamba mwili wake sasa uko vizuri na hivyo anaendelea kujiandaa kurejea katika Octagon ya UFC.
Licha ya Conor McGregor kusema kwamba anataka kupigana tena Masumbwi, lakini amesisitiza kuwa lengo lake kuu kwa sasa ni kurejea kwanza UFC. Raia huyo wa Ireland hajapanda kwenye ulingo wa UFC tangu Julai 2021, alipopata kipigo cha knockout baada kuumia vibaya mguu wake wa kushoto dhidi ya Dustin Poirier kwenye pambano la UFC.
Pambano lake pekee la awali alilocheza la ngumi za kulipwa lilikuwa dhidi ya Floyd Mayweather mnamo mwaka 2017, ambapo McGregor alipoteza kwa TKO katika raundi ya 10, Lakini nyota huyo amesisitiza kwamba atapanda tena katika ulingo wa ngumi siku zijazo.
Hadi kurejea kwake kwenye UFC McGregor atakua hajapigana kwa takriban mwaka mmoja tangu apate jeraha kubwa la mguu katika pambano lake dhidi ya Poirier.
Zikiwa zimesalia sekunde chache kumalizika kwa raundi ya kwanza, mguu wa McGregor ulijikunja chini kwenye kifundo cha mguu, kisha kocha wake John Kavanagh baadaye alisema kwamba hali hiyo ilitokea wakati McGregor alipojaribu kumpiga teke la tumbo mpinzani wake Poirier.