Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbabe, Kiduku wazidi kuporomoka, kwa Mwakinyo mh...!

Mbabe, Kiduku Mwakinyo Mbabe, Kiduku wazidi kuporomoka, kwa Mwakinyo mh...!

Tue, 17 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabondia Hassan Mwakinyo, Dullah Mbabe na Twaha Kiduku wameporoka kwenye ubora wa Tanzania katika kila uzani (pound for pound).

Mbali na ubora wa Tanzania, Mwakinyo pia ameporoka kwenye uzani wake wa super welter duniani ambako sasa ni wa 106 kati ya mabondia 1893.

Bondia huyo aliyewahi kuingia kwenye 14 bora ya dunia mwaka 2019, ameendelea kuporomoka kutokana na kutopigana muda mrefu.

Japo mwenyewe amelieleza Mwanaspoti kwamba anaendelea kujifua kujiweka fiti, huenda kifungo cha mwaka mmoja alichopewa na Kamisheni ya ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kikamporomosha zaidi.

Ifikapo Aprili 24 mwakani bila kucheza bondia huyo ataondoshwa kwenye renki za mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (Boxrec) ambazo bondia asipocheza kwa siku 365 anaondoshwa.

Pambano la mwisho la Mwakinyo lilikuwa dhidi ya Kuvesa Katembo aliloshinda kwa pointi Aprili 23 mwaka huu.

Septemba 29 aligomea pambano na Julius Indongo kwa kile ambacho alidai promota alikiuka makubaliano, jambo lililopelekea TPBRC kutangaza kumfungia mwaka mmoja na kulipa faini ya Sh1 milioni, ingawa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro alikaririwa akieleza wizara itapitia upya adhabu hiyo.

Mbali na Mwakinyo, Kiduku na Mbabe pia wameporomoka kwenye ubora wa Tanzania katika kila uzani.

Kiduku ni wa 13 kutoka nafasi ya tano wakati Mbabe amekamata nafasi ya 36 kutoka ya 14 kwenye pound for pound, wakati kwenye uzani wao wa super middle, Kiduku ameendelea kuwa namba moja na Mbabe akiporomoka hadi nafasi ya nne kutoka ya pili aliyokuwa awali.

Suleiman Kidunda ndiye amekamata nafasi hiyo, huku kwenye pound for pound akiwa wa 14. Kinara wa Tanzania ni Fadhil Majiha, akifuatiwa na Tony Rashid wakati Ibrahim Class anahitimisha tatu bora.

Mabondia wengine walioingia sita bora ni Alberto Kimario, Juma Choki na Nasibu Ramadhani.

Nahodha wa kambi maarufu ya ngumi ya Nakos, Mfaume Mfaume safari hii amepanda hadi nafasi ya 29.

Wakongwe wengine wanaoendelea kutamba ni Awadh Tamim bondia namba moja wa uzani wa juu aliyekamata nafasi ya 46 kwenye pound for pound akifuatiwa na Cosmas Cheka.

Mkongwe mwingine, Francis Miyeyusho yeye ni wa 61, wakati Karim Mandonga akiambulia nafasi ya 98 kwenye kila uzani na namba moja nchini kwenye uzani wake wa cruiser.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live