Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maugo aomba gari la wagonjwa

11831 Pic+maugo TanzaniaWeb

Tue, 14 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katika kile kinachoonekana ni kuendeleza vituko vyake vya ndani na nje ya ulingo, bondia Mada Maugo ‘King’, ameomba gari la wagonjwa mahututi ‘ambulance’ ukumbini ili kumuokoa mpinzani wake, Charles Misanjo wa Malawi watakapozichapa Jumamosi hii.

Maugo na Misanjo watapanda ulingoni katika pambano la raundi 10, kuwania ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati uzani wa super middle, litakalofanyika kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Pambano hilo limeshaanza kuwagawa mashabiki wa ngumi nchini, baadhi wanaamini Maugo atashinda huku wengine wakiamini kuwa atachezea kichapo kutokana na rekodi nzuri alizonazo mpinzani weke kwenye masumbwi.

Maugo anayefahamika kwa tambo zake ambazo huwapa joto wapinzani kabla ya kupanda ulingoni, aliwaomba waandaaji wa pambano hilo kuleta ukumbini gari la kubebea wagonjwa mahututi ili kunusuru maisha ya mpinzani wake kutokana na kipigo atakachompa. “Ingekuwa busara kama waandaaji wa pambano watakumbuka kuleta ambulance ukumbini ili liwe msaada wa kumuwahisha Misanjo hospitali kutoka ulingoni,” alisema Maugo.

Alijitapa kuwa mazoezi aliyoyafanya ni ya kummaliza mpinzani wake mapema, hivyo Misanjo hawezi kumaliza raundi 10, bali atakwenda sakafuni raundi za kwanza.

Maugo alishawahi kutamba kufanya hivyo kwa mabondia wa hapa nchini akiwemo bingwa wa Taifa wa uzani wa middle, Francis Cheka wa Morogoro, lakini hakushinda na ahadi pekee aliyoitima ni ile ya ushindi dhidi ya Japhet Kaseba. Mabondia hao watapima uzito na afya Ijumaa tayari kupanda ulingoni siku inayofuata, siku hiyo pia bingwa wa Dunia anayetambuliwa na Global Boxing Council (GBC), Ibrahim Class atacheza na Baina Mazola pambano la utangulizi.

Mratibu wa pambano hilo, Sophia Mwakagenda alisema maandalizi yote yamekamilika na wakati wowote kuanzia leo, Misanjo atawasili nchini.

“Kila kitu kinakwenda sawa, mabondia wa Tanzania wako kwenye maandalizi ya mwisho mwisho tayari kwa pambano ambalo ni maalumu kwa ajili ya kuchangia taulo za kike ‘pedi’ katika shule mbali mbali nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz