Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maugo akubali yaishe kwa Kaseba

Maugo Pic Data Maugo akubali yaishe kwa Kaseba

Tue, 10 May 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Bondia Mada Maugo amekubali kuangushwa na Japhet Kaseba kwenye kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya mwenyekiti wa Chama cha mabondia nchini.

Maugo hivi juzi alikwaa kisiki mbele ya Kaseba kwenye uchaguzi mkuu wa Chama hicho, huku mabondia wengine, Francis Miyeyusho na Abdalah Pazi 'Dullah Mbabe' wakipenya kwenye nafasi ya ujumbe.

"Wapiga kura si watu wazuri, japo nimeangushwa, lakini kwa mizengwe. Ila nampongeza Kaseba kwa kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa nafasi hiyo ambayo naamini ataitendea haki," alisema Maugo.

Maugo aliyewahi kumshinda Kaseba ulingoni mara mbili,  walipozichapa Juni 2018 na Machi 2015 na kushinda mara zote kwa  'Knock Out' (KO), hivi karibuni kibao kiligeuka ndani ya sanduku la kura, aliposhindwa kwa kura kwenye uchaguzi wa chama hicho.

'Matokeo hayajanishustua sana, ila mpinzani wangu tuliwahi kumwamini na kumpa nafasi ya kutuwakilisha kwenye ujumbe wa Kamisheni (TPBRC). Hakudumu huko na hakutueleza sababu ya kujitoa ndani ya muda mfupi, lakini yote kwa yote nampongeza kwa nafasi aliyoipata."

"Nitampa ushirikiano akihitaji, lakini pia nawashukuru walionipigia kura japo hazikutosha. Nilikuwa na dhamira ya kuwatetea mabondia hasa kwenye makato ya pesa zao wanapocheza mapambano. Mwenyekiti mpya akiona inafaa aishughulikie, la nitasubiri kipindi kijacho nigombee na itakuwa moja ya vipaumbele vyangu tukiwa hai," alisema bondia huyo.

Kaseba bingwa wa zamani wa Afrika wa kick boxing alisema nafasi aliyoipata ni hatua kwake na anakwenda kuwatumikia mabondia kama ambavyo aliahidi katika kampeni zake.

Wakati huo huo, keshokutwa, vigogo wa ndondi za kulipwa, Chata Michael,  Bakari Songoro na Chaurembo Palasa watakuwa wakichuana kusaka urais wa Kamisheni ya ngumi za kulipwa (TPBRC) kwenye uchaguzi mdogo.

Vigogo hao wanachuana baada ya aliyekuwa rais, Joe Anea kujiuzulu nafasi hiyo zaidi ya mwaka mmoja sasa, kabla ya wadau wa ndondi kuingia kwenye kinyang'anyiro hicho, nafasi hiyo ilikuwa inakaimiwa na makamu wa rais, Agapeter 'Mnazarethi' Basil.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz