Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashabiki pambano la Mwakinyo, Mzimbabwe wapewa ofa

Ngumi Pic Data.png Mashabiki pambano la Mwakinyo, Mzimbabwe wapewa ofa

Wed, 19 May 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Ili kuongeza hamasa ya mashabiki kwenye pambano la ubingwa wa Afrika (ABU) la Mtanzania, Hassan Mwakinyo na Brendon Denes wa Zimbabwe, waandaaji wametoa ofa kwa mashabiki.

Pambano hilo litapigwa Mei 28 kwenye ukumbi wa Next Door Arena kuanzia saa 2 usiku likitanguliwa na mengine sita likiwamo la ubingwa wa ABU la mabondia wa uzani wa Cruiser, Jongo Jongo na Olanrewaju Durodora.

Mkurugenzi wa Jackson Group, Kelvin Twissa amesema mashabiki wamepewa ofa ya nusu bei kwenye pambano hilo.

"Tunatarajia mashabiki 600 kushuhudia pambano hilo ukumbini, tayari tiketi zimeanza kuuzwa kwa bei ya ofa kwa watakaonunu mapema na baada ya Mei 21 bei itapanda," amesema.

Amesema viti vya kawaida kwa bei ya ofa tiketi zinauzwa Sh 50,000 na muda wa ofa utakapopita zitauzwa kwa Sh 100,000.

"Tiketi za meza ya watu wanane ni Sh 1.6 Milioni na tiketi za VVIP tayari zimekwisha," amesema.

Amesema pambano hilo lililodhaminiwa na benki ya KCB kwa Sh 94.4 Milioni litaanza kurushwa laivu kupitia Plus Television kwenye king'amuzi cha DSTV kuanzia saa 2 usiku.

"Mabondia wote wanaendelea na mazoezi, tunatarajia wale wa kutoka nje ya nchi kuanza kuwasili wiki ijayo na wote watafikia kwenye hoteli ya Onomo, Posta jijini Dar es Salaam," amesema.

Amesema kabla ya kupima uzito na afya kutakuwa na tukio la 'face off' kwa mabondia hao na Mei 27 watapima uzito tayari kupanda ulingoni.

"Maandalizi yako katika hatua za mwisho mwisho, Rumble in Dar 2 litakuwa pambano la kimataifa zaidi ambalo litatoa burudani kwa wapenzi na mashabiki wa ndondi nchini.

"Lakini pia litafungua fursa kwa mabondia wetu kuonekana katika nchi 32 za Afrika ambako litaonyeshwa laivu," alisema.

Twissa aliwashukuru wadhamini wao wakiongozwa na mdhamini mkuu benki ya KCB, DSTV, Plus Television, M-Bet, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na wengine wote kwa sapoti yao kwenye pambano hilo.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz