Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mandonga apata shavu Uingereza

Mandonga Mslsl Bondia Mandonga

Sun, 15 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mambo yameanza kumnyookea bondia Karim 'Mandonga' Said ambaye usiku wa kuamkia leo ameshinda kwa Technical Knock Out (TKO) pambano lake la kwanza la kimataifa nchini Kenya.

Mandonga amemchapa mwenyeji, Daniel Wanyonyi raundi ya sita ya pambano lililokuwa la raundi 10.

Wanyonyi hakurudi ulingoni baada ya kumalizika kwa raundi ya sita na kusalimu amri kwa Mandonga bondia namba tano nchini Tanzania kwenye uzani wa middle.

Baada ya ushindi huo, kambi ya Mandonga imeeleza kupata ofa za mapambano kwenye nchi za Uingereza, Maurtius na Msumbiji.

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa simu kutoka Kenya, kocha na msaidizi wa ulingo (second) wa Mandonga, Juma Ndambile amesema bondia huyo ataangalia penye maslahi mazuri zaidi ndipo atakwenda kupigana hivi karibuni.

"Tumepokea ofa tatu, ingawa pia Kenya wamemtaka arudi kama sio kurudiana na Wanyonyi basi kucheza na bondia mwingine yoyote," amesema Ndambile huku akizichambua raundi sita za Mandonga ulingoni jana dhidi ya Wanyonyi.

Amesema raundi mbili za mwanzo, alimtaka azitumie kumsoma mpinzani wake, na raundi ya tatu akamwambia asimame apigane.

"Alipoanza hakuwa na guard nzuri, nikamwambia afiche uso, alicheza kwa maelekezo, raundi ya tatu hadi ya tano alicheza vizuri na kuongoza, raundi ya sita ilikuwa ya piga nikupige, ilikuwa iko 50/50.

"Nafikiri Wanyonyi aliogopa kupigwa kwa KO (Knock Out) na kuamua kutorudi ulingoni, kwani kama tungerudi raundi ya saba, kwa namna tulivymsoma mpinzani, ilikuwa ni Mandonga kumaliza kazi," amesema.

Tangu Februari, 2021 alipochapwa na Abdallah Pazi 'Dullah Mbabe' Wanyonyi hakurudi ulingoni hadi jana alipochapwa na Mandonga.

Ushindi huo utaendelea kumuimarisha Mandonga kwenye nafasi yake ya 446 duniani kwenye uzani wa middle, huku mpinzani wake ambaye hakuwa 'active' akiwa hana cha kupoteza.

Hilo ni pambano la tatu kushinda mfululizo kwa Mandonga ambaye amepigana mara nane, ameshinda nne, amepigwa mara tatu na kutoka sare pambano moja tangu 2015.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live