Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mandonga: Nimeshinda lakini..!

Karim Mandonga Kenya Mandonga: Nimeshinda lakini..!

Tue, 28 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ni bahati tu! Unaweza kusema licha ya ushindi na kutawazwa bingwa wa PST, Karim Mandonga alijikuta kwenye wakati mgumu akifanya makosa matano yaliyomlazimisha kutumia nguvu kushinda, jijini Nairobi, juzi.

Mandonga alishinda kwa pointi za majaji 2-1 na kutwaa ubingwa huo wa Afrika Mashariki, ambao ni wa kwanza kwenye historia yake ya ngumi, akicheza Kenya kwa mara ya pili, safari hii akizichapa na Kenneth Lukyamuzi wa Uganda.

Jaji namba moja, Abdallah Mugayi alimnyima ushindi akimpa pointi 74-78, wakati Anthony Rutha wa Tanzania na Linda Abok kila mmoja akimpa ushindi wa pointi 77-75 kwenye Uwanja wa Ndani wa Kasarani, Nairobi, Kenya.

Msaidizi wa ulingo (second), Mzonge Hassan alitumia nguvu kubwa raundi ya pili kumtaka Mandonga abadilike, lakini haikufua dafu na bondia huyo kujikuta akifanya makosa matano ambayo kama Lukyamuzi angekuwa na utulivu, ngumi nzito na mbinu za mchezo angemaliza pambano.

Kosa la kwanza la Mandonga ni kushindwa kujilinda tangu raundi ya kwanza hadi ya saba na kuruhusu kupigwa ngumi nyingi za uso kwenye raundi hizo.

La pili ni kukosa uamuzi katika muda sahihi (timing), kwani alishindwa kumshambulia kwa wakati mpinzani wake na kurusha ngumi nyingi hewani na kupoteza nguvu.

Lukyamuzi alimsoma Mandonga na kumpimia, hivyo muda mwingi alikuwa akiinama pale Mandonga aliporusha ngumi na nyingi kupita hewani na akinyanyuka anajibu mashambuli kwa kupiga ngumi za tumbo ili kumkata pumzi au za kudokoa ambazo zilimuingia barabara.

Kosa jingine ni kutoka mchezoni kuanzia raundi ya tatu na kuhamaki huku akicheza kwa jazba. jambo ambalo halikuwa salama kwake na ilipofika raundi ya nne alianza kucheza na mashabiki akiwahamasisha wamshangilie tofauti na uhalisia.

Japo alijitetea baadae kuwa ngumi si vita, mwanzoni mwa pambano kuna sura za upendo, lakini kadri mnavyocheza roho inachukia na ndicho kilitokea kwake.

“Niliona ananichelewesha kupata nyumba ya ghorofa niliyoahidiwa nikimpiga, hata hivyo subira yavuta heri na wakati wa Mungu ni wakati sahihi,” alisema.

Kosa jingine kwa Mandonga ni kukosa mbinu mbadala, licha ya maelekezo ya ‘second’ wake raundi ya pili, hakubadilika hadi mwisho wa mchezo.

Aina ya uchezaji wa Lukyamuzi, Mandonga alipaswa kucheza ngumi za ‘upper cut’ zaidi, lakini katika raundi zote nane, hakuweza kufanya hivyo, muda mwingi alipiga ‘jabs’ na ngumi chache za ‘one two’, hakufuata maelekezo ya kocha wake aliyompa raundi ya pili.

Hakuwa anatembea na hili ni kosa jingine ambalo lilimpa Lukyamuzi nafasi ya kutawala ulingo, muda mwingi alitembea na kumfuata Mandonga ambaye alikuja kuchangamka raundi ya nane na ya mwisho kabla ya kuwa bingwa wa majaji 2-1.

Watanzania wengine walioshinda siku hiyo ni pamoja na Fatuma Yazidu na Hassan Ndonga.

Chanzo: Mwanaspoti