Bondia Karim Mandonga haishiwi maneno na tayari ameanza tambo kuelekea katika pambano la usiku wa mabingwa ambapo atachuana na bondia Alibaba Ramadhan Desemba 26, mwaka huu mkoani Arusha.
Mandonga ametoka kushinda pambano lake la mwisho dhidi ya Said Mbelwa hivi karibuni mkoani Morogoro na hivyo amepata dili lingine la kufunga mwaka.
Akizungumzia pambano hilo, Mandonga alisema hajawahi kufika mkoani Arusha hivyo atatumia siku hiyo vizuri kuhakikisha anafanya vizuri kwani amejiandaa kuonesha staili mpya ya ngumi.
“Sijawahi kukanyaga Arusha, lakini naamini kitakachotokea ni hatari kwa sababu nimepanga kuonesha staili mpya watu wasiyoijua,” alisema na kuongeza kuwa anakuja na kaulimbiu inayosema: ‘Nikikupiga nimekupiga ukijilegeza nimekuua’.
“Usiku wa mabingwa watamjua Mandonga mtu kazi,” aliongeza bondia huyu anayejulikana kwa tambo nyingi na kaulimbiu za kila pambano.