Wakati Ibrahim ‘Class’ Mgender akishinda kwa TKO na Karim ‘Mandonga’ Said kuchapwa kwa pointi usiku wa kuamkia jana visiwani Zanzibar, baadhi ya makocha wa ndondi nchini wamevunja ukimya kuhusu matokeo hayo, huku Dullah Mbabe akitajwa kufunika.
Mbabe ambaye jina lake halisi ni Abdallah Pazi alimchapa kwa Knock Out (KO) ya mapema raundi ya kwanza, Mussa Banja katika moja ya mapambano yasiyokuwa ya ubingwa kwenye viwanja vya Mao Tse Tung akimpiga ngumi kali mpinzani wake kwenda chini na kuhesabiwa lakini hakuweza kunyanyuka kuendelea na pambano.
Mandonga alichapwa na Muller Jr kwa pointi baada ya kumaliza raundi sita, huku Class akimtandika kwa Technical Knock Out (TKO) ya raundi ya saba Hamis Muay Thai ambaye ni bingwa wa kick boxing (ngumi na mateke) visiwani humo aliyesalimu amri kwa kunyanyua mikono kutoendelea akiwa amebakisha raundi moja kumaliza pambano
Wakiyachambua matokeo hayo, makocha Emmanuel Mlundwa na Rajabu Mhamila (Super D) walisema yameonyesha ukomavu wa mabondia wote.
“Mbabe amepigana vizuri sana, lakini kwa Class pamoja na kushinda ni kama alikuwa anamlea mpinzani wake, muda mwingi ngumi zake zilikuwa hazina power (nguvu) sijui nini kilimtokea, lakini alicheza chini ya kiwango tulichokizoea,” alisema Mlundwa.
Kauli ambayo haina tofauti sana na iliyotolewa na msaidizi wake wa ulingo, Super D ambaye alisema Class alimlea sana mpinzani wake.
“Hadi kuna muda nilimwambia, lile pambano lilikuwa la kumaliza hata raundi ya pili, lakini Class hakufanya hivyo hadi nikamfokea raundi ya tano ndipo akarudi kwenye mchezo wake hadi mpinzani wake akasalimu amri,” alisema Super D ambaye pia ni kocha msaidizi wa bondia huyo.
Upande wa Mandonga ambaye juzi alipoteza pambano la tatu mfululizo, makocha hao kwa nyakati tofauti walisema pamoja na kupigwa, lakini bondia huyo namba moja kwenye uzani wa light heavy alioyesha kubadilika.
“Amepigwa lakini kapigana vizuri, kiwango chake kimebadilika. Jana (juzi) amecheza kombinesheni ya ngumi inayotakiwa, sema ndiyo hivyo lazima mmoja ashinde ukizingatia pambano lake lilikuwa na ushindani,” alisema Mlundwa.
Super D alisema bondia huyo alizidiwa pointi na si uwezo, kwani wote wawili walikuwa na stamina na kiwango kizuri.
Akizungumzia kipigo hicho, Mandonga alisema alizidiwa ufundi kwenye ‘ku-score’ pointi na mpinzani wake lakini anaamini watarudiana na atalipa kisasi.
Bondia huyo ambaye amepoteza nusu nyota hivi karibuni baada ya kuchapwa na Daniel Wanyonyi nchini Kenya alidai akipigwa ni kama amepiga na akipiga amepiga, hivyo bado ataendelea kung;’ara katika medani ya ngumi nchini.