Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majiha kuzichapa na Mfilipino ubingwa wa dunia

Majiha Bondia Fadhil Majiha katika picha akiwa ulingoni kwenye baadhi ya mapambano yake

Tue, 12 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Bondia wa ngumi za kulipwa, Mtanzania Fadhili Majiha atapigana na Mfilipino, Renz Rosia katika pambano la kuwania mkanda wa ubingwa dunia UBO uzito wa super fly litakalofanyika Septemba 30, mwaka huu jijini Mwanza.

Pambano hilo litatanguliwa na mengine sita likiwemo la Francis Miyeyusho dhidi ya Said Mkola katika uzito wa Lightweight na Lulu Kayange na Stumai Muki uzito wa flyweight champion.

Mfilipino amepigana mapambano 29, ameshinda 17 (9 kwa KO), amepigwa mara 10 (2 kwa Ko) na sare mbili, huku Majiha akipigana mapambano 48, ameshinda 30 (15 kwa KO), amepoteza 14 (3 kwa Ko) na sare mara manne.

Kwa mujibu wa mratibu wa pambano hilo, Hamis Kombucha kutoka HB SADC Boxing, mapambano hayo yatafanyika Septemba 30, mwaka huu katika ukumbi wa Rock City Mall, Mwanza kuanzia saa 12 jioni kwa kiingilio cha Sh100,000 (VIP A), Sh50,000 (VIP B) na Sh10,000 mzunguko.

Mabondia wengine watakaozichapa ni Francis Miyeyusho dhidi ya Said Mkola, Lulu Kayage na Stumai Muki, Salehe Kassim na Fredy Sayuni, Pacho Reagan na Ndam James, Issa Maneva na Ahmad Pelembela na John Chuwa dhidi ya Ramadhan Kumbele.

Kombucha amesema mapambano hayo ni sehemu ya mkakati wa kukuza na kutangaza mchezo wa ngumi Kanda ya Ziwa ambapo kupitia tamasha la Royal Tour Boxing Kanda ya Ziwa mapambano mengine yatapigwa Septemba 25, mwaka huu Karagwe mkoani Kagera huku mabondia wakipata nafasi ya kutalii katika mbuga ya Burigi-Chato.

"Tumekuja kuleta ngumi sato ngumi sangara kuinua mchezo wa ngumi Kanda ya Ziwa na kuonyesha kwamba mchezo huu unaweza kutangaza vivutio vya utalii, ambapo Septemba 25 watakwenda Chato kutembelea mbuga na Septemba 30 watakuja kupigana hapa Mwanza,"

"Maandalizi ya pambano hili ni makubwa kutokana na sifa za mabondia watakaopanda ulingoni na ni somo kwa mabondia chipukizi. Mabondia wataripoti Karagwe Septemba 23, Septemba 25 kutakuwa na pambano Karagwe, Septemba 26 watakwenda Burigi chato kutembelea vivutio, Septemba 30 mchezo wa ubingwa wa UBO utapigwa Mwanza," amesema Kombucha

Baadhi ya mabondia watakaopigana kutoka Mwanza, Peter Msyoka na Jiha Bahandwa wamesema wamejiandaa vyema kuwapa burudani wakazi wa Kanda ya Ziwa na kutuma ujumbe kuwa ngumi za mkoa huo ni bora na kuna vipaji vikubwa.

"Mabondia wa Kanda ya Ziwa ni kama tumesahaulika ujio wa pambano hili ni fursa kubwa kwetu, niwaahidi mashabiki wetu tutawakilisha vyema wapinzani wajiandae kwa vipigo vikubwa naamini baada ya hapa watu watajua namna gani kanda hii ina mabondia wazuri," amesema Msyoka

Chanzo: Mwanaspoti