Rais wa Shirikisho la Umoja wa Ngumi Afrika, Houcine Houche, amesema mabondia Fadhili Majiha ‘Stopa’ wa Tanzania na Bongani Mahlangu ‘Profesa’ wa Afrika Kusini, wanatarajia kupanda ulingoni kuwania mkanda wa ubingwa wa WBC Afrika katika pambano litakalopigwa Oktoba 28, mwaka huu kwenye Ukumbi wa PTA Sabasaba, Dar.
Pambano hilo la Royal Boxing Tour Ep 2, limeandaliwa na HB SADC Boxing Promotion ambapo pia lbrahim Class anatarajia kupanda ulingoni dhidi ya Xiao Tau Su raia wa China.
Mapambano mengini ni Nasibu Ramadhani ‘Pacman’ vs Zolisa Baty wa Afrika Kusini, Stumai Muki vs Loveleen Thakuur wa India.
Houcine amefunguka kuwa mkanda wa ubingwa utachezwa kwa mara ya kwanza Afrika na Tanzania tangu kuanzishwa kwake baada ya mkanda wa Ubingwa wa Afrika ABU.
“Natarajia kuja huko na mkanda wa WBC Afrika siku ya Alhamisi kwa ajili ya pambano la kuwania mkanda huu kati ya Fadhili Majiha na Bongani, hii itakuwa ni mara ya kwanza kuchezwa kwa mkanda wa ubingwa Afrika tangu tuanzishe maana huu ni mkanda mkubwa sana” amesema Houcine.
Kwa upande wa Bongani, amesema: “Nategemea kuja Tanzania nikiwa na timu yangu ya makocha wawili, wanisubiri na waambie nakuja kufanya kazi ambayo hakuna anayetarajia kama itatokea hiyo Oktoba 28.
“Nataka niwaambie nilikuja nikampiga Tony Rashid na ndiyo nitakavyompiga Majiha, halafu wao ndiyo wataelewa kwa nini Bongani ni Profesa, mazoezi ninayofanya ni kwa ajili ya kupiga KO na wala siyo jambo lingine, najua Majiha amejiandaa na ni bondia mzuri, lakini wanatakiwa kujua kwamba nitampiga.”