Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MATUKIO YA KUKUMBUKWA 2019: Cheka azushiwa kifo, Mwakinyo atikisa, Vijana wasapraizi

89230 Matukio+%255Bpic MATUKIO YA KUKUMBUKWA 2019: Cheka azushiwa kifo, Mwakinyo atikisa, Vijana wasapraizi

Fri, 20 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

ZIMESALIA siku kama 10 na ushei tu kabla ya kuhitimisha siku 365 za mwaka 2019, mwaka ambao ukiachana na wanasoka, kwenye michezo mingine umeacha kumbukumbu tofauti kwa mabondia, Hassan Mwakinyo na Francis Cheka sanjari na mwanariadha, Failuna Abdi.

Mbali na Failuna ambaye alivuna medali ya shaba ya kimataifa, Cheka yeye alizushiwa kifo huku Mwakinyo akiwa bondia wa kwanza kualikwa na rais John Pombe Magufuli Ikulu na kula naye chakula, lakini pia kitendo cha Vijana Bulls kusapraizi mashabiki wa mchezo wa kikapu katika RBA.

Mualiko huo ulitokana na ushindi wa Machi 23 alipomchapa kwa TKO raundi ya tano Eduardo Gonzalez wa Argentina katika pambano la kimataifa lililopigwa nchini Kenya.

Ushindi huo wa Mwakinyo ulipelekea kuwa miongoni mwa wanamichezo walioalikwa Ikulu na Rais John Pombe Magufuli, sanjari na Taifa Stars ambapo alikula nao chakula na kuwapa zawadi ya viwanja vya kujenga nyumba kila mmoja mkoani Dodoma.

Siku tatu baada ya pambano hilo, Mwakinyo alitembelea Ofisi za kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL), Tabata Relini, Dar es Salaam na kufanyiwa sapraizi na Mkurugenzi Mtendaji, Francis Nanai huku bondia huyo akieleza kutoamini saprizi aliyokutana nayo MCL.

Mbali na pambano hilo, Mwakinyo amefunga mwaka akiwa gumzo baada ya pambano lake na Arnel Tinampay lililopigwa Dar es Salaam huku likiwagawa mashabiki wa ndondi nchini.

Aliyekuwa rais wa Marekani, Barack Obama atakumbukwa kwa kitendo chake cha kushauri ianzishwe ligi ya mpira wa kikapu Afrika Februari 19.

Tayari utekelezaji umeanza na Tanzania ni miongoni mwa timu zinazotafuta nafasi ya kucheza NBA Afrika kwa timu ya JKT ambayo iko kule Kigali Rwanda kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na timu zitakazofuzu zitashiriki NBA Afrika baadaye mwakani, mashindano yatakayokuwa chini ya Ligi maarufu ya mpira wa kikapu Marekani (NBA) kwa kushirikiana na Fiba Afrika.

Bruno bingwa wa kimataifa

Machi 10, bondia Bruno ‘Vifuaviwili’ Tarimo alitwaa ubingwa wa kimataifa wa IBF kwenye uzani wa super feather akimchapa Joel Brunker aliyekuwa akicheza nyumbani Australia kwa pointi za majaji watatu.

Septemba Bruno aliutetea ubingwa huo, kipindi ambacho Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’ alitwaa ubingwa wa WBO huko China na Tony Rashid alitwaa ubingwa wa ABU nchini Afrika Kusini.

Ngumi waundiwa TPBRC

Machi 30, 2019 itabaki kwenye kumbukumbu ya wadau wa ngumi baada ya kufanya mabadiliko na mchezo huo kuanza kuongozwa na Kamisheni moja (TPBRC).

Wadau wa ngumi walishiriki kwenye uchaguzi mkuu wa kwanza wa kamisheni moja na kumchagua Joe Anea kuwa rais wa kwanza wa TPBRC, baada ya wadau wa ndondi kuachana na mfumo wa vyama vingi na mchezo huo kuongozwa na chama kimoja, Anea alimshinda mpinzani wake, Ally Bakari ‘Champion’ kwenye uchaguzi mkuu.

Failuna atwaa medali Ujerumani

Mwanariadha nyota wa kike nchini, Failuna Abdi aliweka rekodi ya medali mwaka 2019 baada ya kutwaa medali ya shaba katika mbio za Haspa Hambarg marathoni, Aprili 28 nchini Ujerumani.

Failuna alitumia saa 2:27:56 kumaliza mbio hizo zilizomuwezesha kufuzu kushiriki Olimpiki 2020.

Waogeleaji wafuzu dunia

Ilikuwa Aprili 23 ambapo waogeleaji Hilal Hilal, Collins Saliboko, Sylvia Caloiaro na Shivani Bhatt walipofuzu kushiriki mashindano ya dunia ya kuogelea yaliyofanyika Korea Kusini, ingawa Watanzania hao hawakufanya vizuri kwenye mashindano hayo.

Mwakinyo apanda viwango

Hassan Mwakinyo amepanda kwenye viwango vya ubora wa ngumi za kulipwa hadi nafasi 18, ilikuwa Mei 15.

Watakata karate Afrika

Mikidadi Kilindo na Elisiana Katani waliibuka washindi kwenye mashindano ya karate Afrika Mashariki na kati yaliyofanyika Mei 13 nchini Uganda.

Kilindo alitwaa medali ya dhahabu wakati Elisiana akiibuka na medali ya fedha kwa wanaume na wanawake.

Mtanzania achezesha Kombe la Dunia

Mwamuzi Karim Zulficar wa Tanzania alikuwa miongoni mwa Waafrika wawili walioteuliwa kuchezesha mashindano ya dunia ya mpira wa kikapu yaliyofanyika Agosti 31 hadi Septemba 15 nchini China, mwamuzi mwingine alitoka Afrika Kusini.

Andy Ruiz atikisa

Andy Ruiz Jr alitikisa kwenye masumbwi baada ya kumchapa kwa TKO, Anthony Joshua (AJ) Juni Mosi na kumvua mataji manne ya ubingwa wa dunia.

Hata hivyo, Desemba 7, AJ aliyarejesha mataji hayo kwa kumchapa Ruiz Jr kwa pointi nchini Saudi Arabia, pambano ambalo Watanzania, Seleman Said na Swedi Mohammed walizichapa na mabondia wa Uingereza mapambano ya utangulizi na kupigwa kwa TKO na KO raundi za awali.

Simbu atwaa Shaba Marekani

Alphonce Simbu, mwanariadha nyota wa Tanzania aliweka rekodi ya kutwaa medali ya shaba nchini Marekani katika mbio za nusu marathoni za Rock in Roll akitumia saa 01:01:34.

Mwanariadha huyo pia alitwaa medali ya fedha kwenye mashindano ya dunia ya majeshi, medali ambayo ilisababisha kupandishwa cheo jeshini JWTZ ambako ni mwajiriwa.

Kocha ndondi afariki

Juni 9 ilikuwa siku ngumu kwa wadau wa ngumi nchini, baada ya taarifa za kifo cha bondia nyota wa zamani wa timu ya taifa na kocha, Benjamin Mwangata.

Mwangata alikutwa amefariki ndani ya nyumba yake iliyopo Gongo la Mboto kando kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Kipigo cha Bangaiza

Kipigo cha TKO kwa bondia Seleman Bangaiza nchini Australia kiliibua mijadala baada ya video ya pambano lake dhidi ya mwenyeji, Andrew Moloney kuonyesha akisalimu amri na kutema kilinda-ulimi bila kupigwa (mouth guard).

Ilikuwa Juni 15 kabla ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kuagiza bondia huyo afungiwe. Hata hivyo, Novemba 23 bondia hiyo alicheza Afrika Kusini na kupigwa kwa KO na Bangile Nyangani

Mfungaji Bora Kanda ya Tano

Ulikuwa mwaka mzuri kwa Baraka Athuman aliyekuwa kinara wa ufungaji kwenye mashindano ya mpira wa kikapu ya Afrika Kanda ya Tano nchini Uganda na kutwaa tuzo ya mfungaji bora Julai Mosi.

Licha ya timu ya Taifa kupoteza mechi zake zote za makundi, Baraka iliitoa Tanzania kimasomaso kwenye mashindano hayo na kuondoka na tuzo hiyo.

Panga Michezo ya Afrika

Mambo yaliiendea kombo riadha baada ya Serikali kuwaondoa wanariadha saba kwenye kikosi kilichotajwa na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kushiriki Michezo ya Afrika iliyofanyika Morocco.

Pigo hilo kwa RT ilikuwa Julai 3, ambapo liliwapitia Fabiano Sulle, Joseph Panga, Faraja Lazaro, Magdalena Shauri, Sisilia Ginoka, Atson Mbughi na Emmanuel Giniki.

Katika michezo hiyo iliyoanza Agosti 19, Tanzania iliwakilishwa na wanariadha watano na wana judo watatu ambao hata hivyo hawakufanya vizuri.

Riadha Taifa yaota mbawa

Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) liliahirisha mashindano ya taifa yaliyokuwa yafanyike Julai 6 na 7 kutokana na ukata, mpaka sasa mashindano hayo hayajafanyika huku zikisalia siku chache kabla ya mwaka kumalizika.

Kigogo BMT aondolewa

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alifanya mabadiliko Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na kumuondoa Alex Nkenyenge ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya Katibu Mkuu na kumteua Neema Msitha kukaimu nafasi hiyo. Tangu Julai 7, nafasi hiyo inakaimiwa baada ya aliyekuwa katibu mkuu, Mohamed Kiganja kuhamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu kama Mkurugenzi wa Maadhimisho na Sherehe za Taifa.

Pambano layeyukia ukumbini

Pambano la ubingwa wa UBO kati ya bondia Mtanzania, Twaha Kiduku na Tshibangu Kayembe wa DR Congo liliyeyukia ukumbini baada ya vurugu kutokea na mabondia hao kutopigana Julai 27 jijini Dar es Salaam wakati mashabiki wakiwa tayari ukumbini.

Kitendo hicho kilisababisha kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC) kumfungia promota wa pambano hilo, Kaike Siraju.

Riadha Taifa washinda na njaa

Ilikuwa ni fedheha ya kufunga mwaka kwa kikosi cha riadha cha Tanzania kushinda bila kula kwa kutokuwa na fedha za kigeni walipokuwa Cairo, Misri wakisubiri kuunganisha ndege kwenda Morocco Agosti 16.

Meneja wa timu hiyo, Donati Masawe alisema mbali na kukosa fedha za kununulia chakula Misri walipokaa kwa saa nane, hata sare za kimichezo timu hiyo haikupewa ingawa Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza alikanusha kukosa sare hizo huku akieleza kutofahamu kama walishinda njaa kwa kukosa fedha.

Tanzania yaaga kabla ya ufunguzi

Ilikuwa Agosti 19, wakati hafla ya ufunguzi wa michezo ya Afrika ikifanyika Cassablanca, Morocco, timu ya judo ya Tanzania ilipishana na hafla hiyo baada ya wachezaji wake, Abdulrabi Alawi, Anangisye Pwele na Khamis Ally kupigwa katika hatua za mwanzo siku mbili kabla ya hafla ya ufunguzi.

Cheka azushiwa kifo

Ilikuwa taharuki kwa wadau wa ngumi za kulipwa baada ya bondia Francis Cheka kuzushiwa kifo katika ajali ya moto wa mafuta mkoani Morogoro, kabla ya mkewe Toshi Asenga kuibuka Agosti 13 na kusema bondia huyo bingwa wa zamani wa dunia wa WBF ni mzima wa afya na taarifa za kwamba alionekana kwenye eneo la tukio kabla ya moto kuwaka hazikuwa za kweli.

Simbu, Failuna wakataa kambi

Agosti 5, wanariadha Failuna Abdi na Alphonce Simbu walikataa kambi ya Kenya kujiandaa na mashindano ya dunia yaliyofanyika Doha, Qatar Septemba.

Kitendo hicho kilimuibua rais wa Riadha Tanzania, Anthony Mtaka baada ya Tanzania kuboronga ambapo alisema matokeo hayo hayakuwa sapraizi kwake kwani aliyatarajia kutokana na maandalizi ambayo wanariadha hao waliamua kufanya na kukataa kuingia kambini.

Netiboli yakwama Afrika

Mwaka 2019 utabaki kwenye kumbukumbu chungu kwa timu ya Taifa ya netiboli (Taifa Queens) baada ya kushindwa kushiriki mashindano ya Afrika nchini Afrika Kusini wakiwa tayari kambini.

Taarifa ya kutoshiriki mashindano hayo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Chaneta, Judith Ilunda alitangaza Tanzania kujitoa siku moja kabla ya ufunguzi wa mashindano hayo Oktoba 18 kutokana na kukosa pesa.

Gidabuday abwaga manyanga RT

Novemba 2, Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania, Wilhelim Gidabuday alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo.

Gidabuday alichukua hatua hiyo wiki kadhaa baada ya timu ya taifa kupoboronga kwenye mashindano ya dunia nchini Qatar.

Mufuruki akumbukwa gofu

Desemba 09, Bilionea Ali Mufuruki aliyefariki duniani nchini Afrika Kusini aliagwa kwenye ukumbi wa mwalimu Nyerere Dar es Salaam kabla ya mazishi yake, huku Mwenyekiti wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU), Chris Martin akieleza namna alivyokuwa amepanga kujenga uwanja wa gofu kwenye Hifadhi ya Saadan.

Chanzo: mwananchi.co.tz