Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwenye Masumbwi umri ni namba tu

Foreman Jimmy Custom 2074c17b13f9e63f081e978a872a67b7e56c77ea Kwenye Masumbwi umri ni namba tu

Wed, 26 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kwenye mchezo wa ngumi, ubingwa wa uzito juu (Heavy Weight Champion), ndiyo unaopewa heshima kubwa zaidi.

Wengi wameupata lakini wakiwa vijana kwani inahitaji nguvu na akili nyingi kuweza kufanikisha hilo.

Lakini sio tu vijana wanaofanikisha hilo, historia inaonyesha hata mabondia wenye umri mkubwa nao wamewahi kushinda ubingwa huu, tena mbele ya vijana.

Hawa hapa ni mabondia 10, waliowahi kushinda uzito wa juu wakiwa na umri mkubwa.

10. Jess Willard

Willard ndiye bondia aliyeshinda uzito wa juu akiwa na umri mdogo zaidi katika orodha hii.

Alishinda pambano la uzani wa juu mwaka 1915 alipompiga Jack Johnson akiwa na umri wa miaka 33.

Alikaa na mkanda huo hadi mwaka 1919, alipochapwa na Jack Dempsey na kunyang’anywa akiwa na umri wa miaka 27.

Pambano hilo lililomvua ubingwa lilimwacha Willard akiwa na majeraha sana baada ya kuchapika vilivyo.

9. Muhammad Ali

Anajulikana kama mmoja kati ya mabondia bora kuwahi kutokea katika mchezo wa ngumi.

Rekodi zinaonyesha alitumia miaka tisa na miezi mitano kuwa na ubingwa wa uzito wa juu katika vipindi tofauti tofauti akianzia mwaka 1964, 1974, na 1979.

Katika mapambano 61 aliyopigana kabla ya kustaafu, Ali alishinda 56.

Aliingia katika rekodi ya kushinda uzito wa juu akiwa na umri mkubwa mwaka 1978, akiwa na umri wa miaka 36 na miezi saba na akavuliwa mwaka 1979, akiwa na umri wa miaka 37.

8. Corrie Sanders

Unaweza kumwita ‘Corrie’, alikuwa bondia wa kulipwa wa Afrika Kusini, aliyevuma sana baada ya pambano lake la mwaka 2003 dhidi ya Wladimir Klitschko na alishinda.

Ushindi wake ulimshangaza kila mtu kwani Klitschko kwa wakati huo alikuwa bingwa wa uzito wa juu mara mbili.

Licha ya kushinda pia aliingia katika rekodi ya kuchukua mkanda huo wa uzito wa juu akiwa na umri mkubwa (miaka, 37).

Alidumu na mkanda hadi mwaka 2004 alipofikisha umri wa miaka 38 na alipoteza pambano dhidi ya kaka yake ndugu yake Wladimiri, Vitali Klitschko mwaka 2004.

7. Evander Holyfield

Mashabiki walimwita ‘The Warrior,’ Evander Holyfield, moja ya matukio yakukumbwa zaidi yaliyowahi kutokea wakati alipokuwa ulingoni ilikuwa ni kung’atwa sikio na Mike Tyson.

Katika maisha yake ya ngumi aliwahi kushinda mikanda mbalimbali kama WBA, WBC, na IBF.

Aliingia katia rekodi yakuwa bingwa wa uzito wa juu mwenye umri wa mkubwa mwaka 2000 alipomchapa Andy Ruiz akiwa na umri wa miaka 37 na akalipoteza mwaka huo huo akiwa na miaka 38.

Kabla ya kustaafu mwaka 2014, Holyfield alikuwa ameshinda mapambano 44 kati ya 57.

6. Lennox Lewis

Mwaka 2002 ulikuwa ni wakipekee kwa bondia huyu baada ya kumchapa Mike Tyson kwa TKO, mbali ya kuchukua mkanda wa uzito wa juu, pia aliingia katika rekodi ya kushinda mkanda huo akiwa na umri mkubwa (miaka 36) na alidumu nalo hadi alipofikisha umri wa miaka 38.

Kabla hajastaafu mwaka 2004, alikuwa ameshacheza mapambano 44 na kushinda 41, pia alishinda medali ya dhahabu katika michezo ya Olympic mwaka 1988.

Kwa sasa Lewis ni mtangazaji wa ngumi.

5. Joe Walcott

Jina lake kamili ni Arnold Raymond Cream, lakini anajulikana kama Jersey Joe Walcott, alikuwa bondia raia wa Marekani ambaye aliyeingia katika rekodi ya kushinda uzito wa juu aliodumu nao hadi alipofikisha umri wa miaka 39 na akakaa na mkanda kuanzia 1951 hadi 1952, ikiwa ni siku 433.

Kabla ya kustaafu mwaka 1953, Joe Walcott alikuwa ameshinda mapambano 49 kati ya 70 aliyocheza.

Baada ya kustaafu mwaka wa 1953, alihamia katika uigizaji na utangazaji wa vipindi vya televisheni.

4. Oleg Maskaev

Oleg ambaye ana asili ya Urusi na Marekani aliingia katika rekodi ya mabingwa wa uzito wa juu wenye umri mkubwa zaidi mwaka 2006 aliposhinda pambano dhidi ya Hasim Rahman akiwa na umri wa miaka 37 Alidumu na mkanda huo hadi mwaka 2008 alipovuliwa akiwa na miaka 39.

Alianza rasmi ngumi za kulipwa mwaka 1993 baada ya kuacha kazi za migodini na katika kipindi chote cha maisha yake ndani ya mchezo huu kabla ya kustaafu mwaka 2013, alishinda mapambano 39 kati ya 46.

Alisifika sana na ngumi yake ya mkono wa kulia ambayo ilikuwa nzito na iliangusha mabondia wengi.

3. Wladimir Klitschko

Bondia huyu wa zamani wa Ukraine, alianza kupanda ulingoni rasmi katika ngumi za kuliapa mwaka 1996 hadi 2017.

Katika kipindi hicho alifanikiwa kushinda mkanda wa uzito wa juu mara mbili na ule wa pili ndio alidumu nao kwa muda mrefu kuanzia mwaka 2006 hadi 2015 na hii ndio ilimpa rekodi kwani alishinda akiwa na umri wa miaka 30 na kulipoteza akiwa na umri 39.

Kabla ya kustaafu alicheza mapambano 69 na kushinda 64.

2. Vitali Klitschko

Amewahi kushinda mkanda wa uzito wa juu mara tatu na mara ya mwisho alikaa nao kwa siku 1,892 ambazo zilikuwa ni kuanzia mwaka 2008 hadi Desemba 2013.

Aliweka rekodi mwaka 2008 aliposhinda Samuel Peter kutoka Nigeria wakati huo akiwa na umri wa miaka 37 na akalipoteza mwaka 2013 akiwa na miaka 42.

Huyu ni ndugu yake Wladimiri Klitschko ambaye pia yupo katika orodha hii, lakini Vitali ndio anatajwa kuwa bora zaidi kuliko kaka yake.

Bondia huyu ambaye kwa sasa ni meya wa Manispaa ya Kyiv huko Ukraine, kabla hajastaafu ndondi alikuwa ameshinda 45 kati ya 47.

1. George Foreman

Huyu ndio bingwa wa uzito wa juu mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kutokea katika historia ya mchezo huu.

Aliweka rekodi hii mwaka 1994, akiwa na umri wa miaka 45 alipomshinda Axel Schulz na alivuliwa akiwa na miaka 46.

Foreman ambaye ni raia wa Marekani ni mmoja kati ya mabondia walioacha alama kubwa katika mchezo wa ngumi.

Aliwahi pia kushinda medali ya Dhahabu katika michuano ya Olimpiki ya mwaka 1968.

Kijumla kabla ya kustaafu alishinda mapambano 76 kati ya 81.

Mikanda ya kwanza kushinda ilikuwa ni WBA na WBC mnamo 1973 alipokuwa na umri wa miaka 24.

Chanzo: Mwanaspoti