Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwani Mwakinyo anatuonaje?

Hassan Mwakinyo Liam Kwani Mwakinyo anatuonaje?

Thu, 8 Sep 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kama kuna dhana inatumika vibaya nchini kwa sasa ni ile ya uzalendo. Watu wengi wanadhani kuwa mzalendo ni kusifia kila kitu. Watu wengi wanadhani kuwa mzalendo ni kupongezana tu na kutiana moyo. Bondia wa Tanzania Hassan Mwakinyo amepigwa nchini England kwenye mazingira ya kutatanisha, lakini watu wanapongezana tu na kutiana moyo.

Hakuna asiyejua uwezo wa Mwakinyo. Ni moja kati ya mabondia wetu wanaojielewa. Moja kati ya mabondia wenye timu kubwa ya watu mgongoni kwake. Mpambanaji na mtu kazi kwelikweli.

Kupigwa kwa Mwakinyo kumeacha maswali mengi na watu wanajificha kwenye Kivuli cha uzalendo. Ni mwendo wa kutiana moyo tu. Ni mwendo wa kujipa matumaini. Mwakinyo baada ya kupigwa amekuwa akitoa taarifa nyingi kupitia mitandao ya kijamii akijaribu kueleza kile alichokiona na hujuma dhidi yake.

Ukimsikiliza kwa makini utagundua kwamba kauli zake hazina mashiko. Watu wanamuonea aibu kwa kigezo cha uzalendo. Tunatumia vibaya dhana ya uzalendo kwa vijana wetu tukidhani kuwa tunawasaidia. Kama tuna nia ya dhati ya kusonga mbele, tujenga utamaduni wa kuambiana ukweli na kutafuta majibu ya maswali magumu. Uzalendo sio kuogopana. Uzalendo sio kulindana. Uzalendo ni kuambiana ukweli.

Mwakinyo ameanza kwa kueleza kile alichokiita ni fitina kwa begi lake kushindwa kufika kwa wakati mjini Liverpool kutokea Amsterdam, Uholanzi. Hii hoja haina mashiko hata kidogo. Kupotea kwa mizigo au kuchelewa kufika sio fitina. Inatokea mara nyingi sana kwenye usafiri wa ndege.

Usafiri wa ndege una changamoto zake na hiyo ni mojawapo. Abiria tu wa kawaida mizigo yao inapotea au kuchelewa kila siku na hakuna anayesema ni fitina na hasa pale unapolazimika kubadilisha ndege ili kufika unapotaka kwenda.

Ukiondoka Shirika la Ndege la KLM ni lazima uende kwanza Uholanzi kabla ya kuendelea na safari. Ukiondoka na ndege za Kenya Airways ni lazima upite Nairobi, Kenya kwanza kabla ya kwenda unapotaka kwenda. Ni Jambo la kawaida kabisa mizigo kuchelewa kufika.

Unaposafiri na Ethiopian Airlines ni lazima upite kwanza Addis Ababa kabla ya kuendelea na safari yako. Mwakinyo ameleta sababu nyepesi sana. Lakini hata kama begi lililokuwa na viatu vyake lilichelewa kufika, Liverpool ni moja kati ya majiji makubwa matatu nchini Uingereza. Hakuna kiatu unachotaka unaweza kukikosa pale. Hakuna!

Uzalendo sio kupongezana tu, ila uzalendo ni pamoja na watu kuambiana ukweli. Mwakinyo angeweza kupata viatu vingine vizuri tu pale Liverpool. Mwakinyo angepata viatu vya saizi yake pale Liverpool kabla ya pambano. Baada ya bondia wetu kupigwa sababu za kupewa viatu vinavyombana nazo zikaibuka.

Hivi ni kweli Mwakinyo alipewa viatu akiwa ulingoni? Jibu ni hapana. Kuna kitu kimejificha juu ya kupigwa kwa Mwakinyo pale Liverpool. Hatuhitaji saa mbili kujua kama kiatu kinakubana. Mwakinyo alipaswa kujua mapema. Inafurahisha kuona baada ya pambano bado alikuwa amevaa viatu vilevile vinavyombana na kujirekodi. Inafurahisha kuona Mwakinyo aliyeshtua enka hata baada ya kutoka ulingoni bado alikuwa amevaa viatu.

Watanzia sio wajinga. Watu wanafuatilia mambo. Kupigwa sio tatizo, shida kubwa ipo kwenye aina ya kupigwa. Sababu ya kuachwa begi na kupewa viatu vilivyombana haina mashiko kabisa kutoka kwa Mwakinyo. Labda kama mwanetu atakuja na sababu mpya.

Mwakinyo bado ni bondia bora Afrika kwenye uzito wake. Ni heshima kubwa kwake na kwa nchi, lakini hiki kilichotokea juzi nchini Uingereza kinaleta maswali mengi ambayo hayajibiwi na majibu yake. Somo la uzalendo inabidi tufundishwe upya. Kusifia kila kitu na kutia moyo matokeo yake ndiyo haya ya mtu kubanwa na viatu wakati amezungukwa na maduka kila kona yanayouza viatu vinavyomtosha.

Unakubaliana na Mwakinyo kuwa alihujumiwa kwenye pambano lake? Mimi hapana. Labda kama atakuja na sababu nyingine yenye mashiko. Unakubaliana kuwa alikosa duka lolote mjini Liverpool lenye viatu vinavyomtosha? Mimi jibu ni hapana. Kuna kitu kitakuwa kimejificha tu nyuma ya Mwakinyo kupigwa.

Ukitazama pambano lenyewe kabla ya bondia wetu kuanza kuleta mauzauza, Mwakinyo alikuwa ametawala kila kona. Smith ni bondia mzuri na mwenye rekodi nyingi nzuri, lakini umri umeanza kumkimbiza. Kama Mwakinyo angeshinda pambano hilo lingempeleka mbali.

Kwa ufupi ni kwamba kijana ametuangusha. Kifupi ni kwamba kijana katumwaga. Hiki ni moja ya vipigo vya mauzauza. Hiki ni moja kati ya kichapo chenye maswali mengi kuliko majibu. Sina tatizo na bondia wetu kupigwa, nina tatizo na sababu alizozitoa. Zimekuwa nyepesi mno. Ni sababu ambazo kwa ufupi hazina mashiko.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz