Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kutoka kupiga debe, kudansi hadi ngumi

Mandonga Mslsl Kutoka kupiga debe, kudansi hadi ngumi

Tue, 22 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Safari ya kujitafuta hadi kujipata ya Karim ‘Mandonga’ Said, haikuwa nyepesi, japo alifanya vitu vingi, lakini wengi walianza kumfahamu kwenye masumbwi ikiwa ni baada ya kutundika glovu kwa miaka mitatu, tangu Julai 2015, alipochapwa kwa TKO na Benki Mwakalebela kwa mara ya kwanza, hakurudi tena ulingoni hadi 2018, akapigwa tena na Juma Misumali.

Aliporejea kwa mara nyingine, Agosti 2021 na kumchapa Omari Mgoa na kutoka sare na Mohamed Mkude, Desemba 2022, bado hakuwa kwenye nyoyo za mashabiki. Maneno na tambo zake kabla na baada ya pambano la Machi 26, 2022 dhidi ya Magambo Christopher ndivyo vilipendwa na mashabiki, kabla ya pambano hilo, wengi walitaka kuona kama maneno yatakuwa vitendo, ikawa kinyume baada ya kupigwa kwa KO.

Hata hivyo, hakujali matokeo yale, aliendelea na tambo, mashabiki wakimpenda hivyo hivyo na kuanzia hapo 'gari likawaka', miezi minne baadae alichapwa KO nyingine na Shaban Kaoneka.

'Mandonga Mtu Kazi', jina lake hilo la utani linayaangazia maisha yake halisi, anasema hakubagua kazi, alifanya vitu vingi, yote hiyo ikiwa ni kujitafuta katika maisha, alifanya hayo akipambana na haso za mtaani.

“Nimefanya vitu vingi sana hadi kufika hapa, nilikuwa na vipaji tofauti vya Sanaa, lakini sikujua nitasaidiwa na nani katika kutimiza ndoto zangu, hadi nilipopata uelekeo kupitia ngumi," anasema.

Amesema baada ya udansa kutokuwa fursa kwake wakati ule, alipata kibarua cha kupiga debe na kupokea wageni kwenye stendi kuu ya mabasi mkoani Morogoro ya Msamvu.

“Nimepiga debe kwa miaka mingi sana, asilimia kubwa ya maisha yangu niliyawekeza pale stendi katika kazi hii, ilikuwa ni kazi ambayo baadaye imekuja kunipa chaneli nyingine ya maisha,” anasema.

Amesema akiwa pale, alijiunga kwenye gym ya Msamvu ambayo ilikuwa ikifundisha masumbwi ndipo alikoanzia kujifunza mchezo huo unaompa maisha hivi sasa. “Nilikuwa na ratiba maalumu ya kazi, asubuhi naingia kwenye kibarua stendi, jioni nakwenda kufanya mazoezi, haikunipa wakati mgumu kwa kuwa gym ilikuwa jirani kabisa na kituo changu cha kazi.

Amesema kazi yake ya kupiga debe aliifanya kwa muda mrefu hadi pale Mwenyezi Mungu alipomuonyesha mwanga wa kujikita kwenye ngumi. “Ni Mungu tu, naona alitaka kunionyesha kuliko kung’ang’ania sehemu moja, natakiwa sasa nitoke kwenye kupiga debe nijikite kwenye ngumi na sasa ninafanya na filamu ,” anasema na kufafanua.

“Nilikuwa comedian (mchekeshaji), baunsa lakini kabla ya yote nilikuwa dansa. "Siku moja yalifanyika mashindano ya Afrika Mashariki pale Morogoro, nikajitosa na kuwa dansa bora, hata hivyo hakukuwa na maslahi, nikatoka, nimefanya vitu vingi hadi sasa napigana na kufanya filamu.

Dau lake liko hivi

Mandonga ambaye alipata bahati ya kukubalika kwa mashabiki licha ya kupigwa, na kila alipoendelea kupigwa ndipo aliendelea kufuatiliwa na mashabiki anasema hana dau maalumu.

“Huwa sitangazi dau langu, akitokea promota anataka nipigane kwenye pambano, tutakaa chini na kukubaliana, likinilipa nacheza, hata kwenye filamu nilivyoingia ndivyo vivyo hivyo, sijawahi kusema nalipwa kiasi gani kwenye kazi ninazofanya, japo zote zinanipa maslahi mazuri,” amesema.

Bondia huyo anayejiita nabii aliyeamua kuzitangaza ngumi za Tanzania, amesema alikuwa akimkubali zaidi Mike Tyson. "Ngumi zilikuwa moyoni mwake, aliufanya mchezo huo uonekane ni rahisi, akiingia ulingoni mapema tu anamaliza," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live