MENEJIMENTI ya bondia Hassan Mwakinyo imesema kama bondia huyo hatabadilishiwa mpinzani hatocheza Jumamosi ijayo huko Dominican Republic.
Mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (boxrec) umemtaja Mwakinyo kuwa miongoni mwa mabondia 30 watakaopanda ulingoni siku hiyo kwenye Hotel ya Marien, Santiago Rodriguez, kuwasindikiza Liliana Martinez na Grecia Novas Mateo.
Boxrec inaonyesha Mwakinyo atazichapa na Julio de Jesus Rodriguez, pambano la utangulizi ambalo meneja wake amesema kama hatobadilishiwa mpinzani basi hatocheza kwa kuwa ni hasara kwake.
“Wamekuwa na pupa ‘haraka’ ya kuliweka boxrec wakati tangu mwanzo tuliwambia huyo mpinzani hafai kucheza na Mwakinyo, ni hasara kubwa bondia wetu kupigana naye,” alisema Huzeifa Huzeifa meneja wa Mwakinyo.
Alisema Mwakinyo ambaye kwa sasa anaishi Marekani si bondia wa kucheza na Rodriguez ambaye kwenye renki ya dunia ana nyota moja na nusu akiwa nafasi ya 316 kati ya mabondia 1908 na Mwakinyo ni wa 17 na nyota nne kwenye uzani wa super welter.
“Itakuwa ni hasara kubwa kwa Mwakinyo kucheza hilo pambano, halitomuongezea chochote hata kama atashinda, alipoletwa kwetu huyu mpinzani tulimkataa.
“Tuliwaambia bondia wetu atacheza na mabondia wenye renki za juu kidogo au waliowahi kucheza na miamba ya dunia na wale waliowahi kuwania mataji makubwa ya dunia kutokana na rekodi yake lakini si kwa huyu ambaye tumeletewa, tulimkataa mapema wao wamefanya pupa kumuweka boxrec,” alisema.
Akizungumzia maneno yanayoendelea kuwa Mwakinyo kakubali kucheza pambano hilo ili apate pesa sababu ana ukata huko Marekani ambako kwa miezi kadhaa sasa ndiko anaishi, meneja wake alisema hayo ni maneno ya watu na hawawezi kuwazuia watu kusema watakacho.
“Kila mtu ataongea anavyoweza, lakini sisi tunafahamu nini tunakifanya na Mwakinyo yuko kwenye levo gani kidunia,” alisema Huzeifa.
Alisema kama promota wa pambano la Jumamosi ataridhia kufuata taratibu na kubadilisha mpinzani kama wakivyokubaliana basi Mwakinyo atapigana la sivyo bondia huyo namba moja nchini hatacheza pambano hilo hadi pale itakavyoamuliwa vinginevyo.