Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilichompa ushindi Mwakinyo chatajwa

86659 Pic+mwakinyo Kilichompa ushindi Mwakinyo chatajwa

Mon, 2 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati ushindi wa bondia Hassan Mwakinyo dhidi ya Arnel Tinampay wa Ufilipino ukiwa gumzo nchini, mabondia wakongwe wameeleza sababu zilizompa ushindi Mtanzania huyo.

Juzi usiku, Mwakinyo alitangazwa mshindi kwa pointi za majaji 2-1 kwenye pambano la ngumi la kimataifa lililofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini hapa, huku mwenyewe akikiri kushinda kwa tabu.

Katika pambano hilo, Tinampay alionekana kucheza kwa kujiamini zaidi na kutumia mbinu ya kutompa nafasi Mwakinyo kumshambulia ambapo muda mwingi alikubali kubanwa kwenye kona.

Tinampay alicheza raundi zote bila kurudi nyuma huku Mwakinyo akitaka kucheza kwa kushindana naye mbinu ambayo ilikuwa ngumu kwake kwani mpinzani wake alikuwa na vizuri.

Kutokana na hali hiyo ilimchukua muda mrefu kumsoma na kuanza kumrushia ngumi na kumkimbia, mbinu ambayo kama angeitumia mapema ingempa tabu Mfilipino.

Kilichompa ushindi

Licha ya mashabiki kutoka uwanjani wakiwa wamegawanyika kutokana na ushindi wa Mwakinyo, mabondia wakongwe wameeleza kilichombeba Mtanzania huyo.

“Hata ningekuwa mimi jaji, Mfilipino ningempa ushindi katika raundi tatu pekee na raundi saba ningempa Mwakinyo,” alisema bondia wa zamani, Emmanuel Mlundwa ambaye alikuwa mwamuzi wa pambano hilo.

Alisema katika ngumi matokeo ya kila raundi yanajitegemea bila kujali umepigwaje katika kila raundi.

“Anayeshinda anapewa pointi 10 na anayepigwa anapewa pointi tisa, kama ukipigwa hadi kuhesabiwa ndipo unakatwa pointi moja na kupewa nane na aliyeshinda katika raundi hiyo anabaki na pointi zake 10,” alisema Mlundwa.

“Katika lile pambano hakuna aliyehesabiwa na Mwakinyo alipiga ngumi nyingi zilizomkuta mpinzani wake kulinganisha na Tinampay.”

Bingwa wa zamani wa dunia wa WBF, Karama Nyilawila alisema: “Haijalishi umempigaje mpinzani wako katika kila raundi, hata umpige ngumi nyingi kiasi gani kama hajasalimu amri maana yake wakimaliza raundi hiyo aliyeshinda ana pointi 10 na aliyepigwa ana pointi 9, hivyo zilipokuja kujumlishwa mwishoni ikaonekana Mwakinyo ana pointi nyingi sababu aliongoza raundi nyingi kulinganisha na mpinzani wake.”

Naye bondia Mada Maugo alimpongeza Mwakinyo kwa ushindi, lakini akasema pambano lilikuwa gumu kwake.

Ubora wa Tinampay

Ukiachana na uzoefu wa Tinampay ambao ni mara tatu ya Mwakinyo ulingoni, bondia huyo kutoka kambi ya mwanamasumbwi wa kimataifa, Manny Pacquiao, alijiamini kupitiliza ulingoni na mara kadhaa alionekana kutumia mbinu ya kumtisha Mwakinyo pale alipomkosakosa kwa makonde.

Chanzo: mwananchi.co.tz