Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ibra Class afungukia changamoto za ughaibuni hadi kuwa mfalme ulingoni

Ibrah Class Vitasa.png Ibra Class afungukia changamoto za ughaibuni hadi kuwa mfalme ulingoni

Tue, 4 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

“Maisha ya mwanadamu ni hadithi tu hapa duniani, basi ndugu yangu kuwa hadithi nzuri kwa hao watakaosimuliwa.” Hii ni moja ya nukuu zenye ujumbe mzito zilizowahi kutolewa na Rais wa Awamu ya pili wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Ali Hassan Mwinyi.

Nukuu hiyo imebeba taswira halisi ya kijana mdogo kutokea Mafinga, mkoani Iringa, Ibrahim Class kutokana na mapito mazito aliyopitia kabla ya kuwa bondia katili anayeburudisha ndani ya ulingo.

Class ambaye kwa sasa Tanzania ni bondia wa pili kwa ubora mbele ya Fadhili Majiha, ana rekodi ya kucheza mapambano 38, ameshinda 28 na 15 ni kwa KnockOut na kapoteza sita pekee matatu yakiwa ni kwa KO.

Mwanaspoti lilifanya naye mahojiano na kuzungumza mengi kuhusu maisha yake tangu akiwa mdogo, jinsi alivyokimbiwa na baba yake na hadi sasa akiogelea pesa za kampuni kadhaa kutokana na kuwa balozi wao. Huyu hapa:

AKIMBIWA NA BABA

“Nikiwa mkoani Iringa mama mkubwa alinisimulia baba yangu alikuwa akimpiga mama na mara ya mwisho kabla ya kumkimbia mama na pamoja na mimi, alimpiga na kumchomea nguo zote moto.

“Wakati anafanya tukio hilo, mimi ndiyo bado mdogo, nilikuwa nalia sijui chochote na mama mkubwa alifika na kumfokea baba na kuacha mara moja. Baba alikuwa anamwogopa mama mkubwa.

“Siku ya pili alichukua pesa ya mtaji wa biashara ya pombe na baada ya mama na mama mkubwa kuondoka, baba alitoa vitu vyote ndani zikiwamo nguo za mama na kuzichoma moto. Nilikuwa nalia lakini hakujali na aliwasha gari na kukimbilia Arusha ambako baba yake ambaye ni babu yangu alikuwa akiishi huko na maisha yake yalikuwa mazuri maana alikuwa na uwezo mkubwa wa mali kwa kuwa alikuwa mfanyabiashara.”

Wakimbilia tanga

“Iliwalazimu sasa ile pombe waliokwenda kuchukua waanze kuiuza ili kupata pesa na majirani wakiwasaidia kupata mikeka ya kulalia maana baba alishachoma vitu vyote,” anasema Class na kuongeza kabla ya safari aliugua na pesa iliyopatikana alitibiwa nayo na hivyo waliongeza mwezi mwingine kusaka nyingine huku mama yake alikuwa na ujauzito wa mdogo wake Oswald (marehemu) naye akaanza kuumwa.

“Lakini jambo la kushukuru walipambana na tukaondoka Iringa kwenda kuishi Raskazone, Tanga kwa baba yetu mkubwa ambaye alikuwa mwanajeshi ila baada ya muda mama mambo yakawa magumu upande wake akanirudisha kwa bibi yangu mzaa mama Iringa alikosoma hadi darasa la saba.

AAJIRIWA KUCHUNGA NG’OMBE

“Nilirudi Iringa kuishi na bibi na nilisoma hadi darasa la saba. Maisha yalikuwa magumu na ilibidi nitafute kazi ya kuchunga ng’ombe na mbuzi.

“Nakumbuka nilichunga takriban mwaka mzima, lakini nikalipwa Sh3500 pesa yote iliyobakia nikadhulumiwa. Bosi akadai nimeua mbuzi wengi kwa kuwalisha majani siyo, hivyo nikapigiwa hesabu ya mbuzi iliobakia ndiyo nikapewa,” anasema Class na kuongeza baada ya kuona mambo magumu, ilibidi arudi kwa bibi yake.

ALIVYOFIKA DAR

“Hapa Dar maisha nimeanzia Manzese ambako kaka alikuwa amepanga chumba kimoja na mke alikua amemuacha Iringa kwa kuwa alikuwa mjamzito. Hata hivyo, alikuwa na mke mwingine aliyekuwa akiishi posta.

“Bahati mbaya, mke aliyekuwepo Iringa alirudi na chumba ni kimoja, hivyo usiku wa kwanza nikakesha kwenye kigodoro cha mziki jirani kwa sababu sikuweza kulala chumba kimoja na shemeji yangu,” anasema na kuongeza kutokana na kukosa mahali pa kulala, kaka yake ambaye alikuwa ana ofisi ya kutengeneza spika Kariakoo alikuwa akienda naye kwa lengo la kujifunza na wakati mwingine nikawa nalala huko kwa kutandika maboksi.

Hata niliporudi kwa kaka Manzese nikawa nalala chini ukumbini kwa kutandika mkeka yaani nakuwa wa mwisho kulala na wa kwanza kuamka.

Nini kilimshawishi kuingia kwenye ngumi?

“Unajua wakati ule nimefika Kariakoo, kaka zangu Juma Salim na Juma Mponda naweza kusema wamenishawi sehemu kubwa licha ya mwenyewe kuupenda mchezo huo tangu nikiwa mdogo.

“Walikuwa na kawaida ya kufanya mazoezi kila jioni baada ya kazi nikawa naenda kuangalia na kila nilipotaka kufanya walinizuia kwa kuona nawachelewesha.

“Walipokuwa wanamaliza mimi nilikuwa nachukua chupa zangu za maji, napanga kisha nafanya vile wao walivyokuwa wakifanya kutokana na juhudi zangu ikawabidi wanipeleke kwa mtu aliyekuwa akijulikana kama Masta Tula.

“Bahati mbaya sikukaa sana, wakanileta kwa Masta Habibu Kinyogoli (bondia wa zamani wa ngumi za ridhaa) pale Amana Ilala, nashukuru alinipokea.

“Kuna siku nikiwa nafanya mazoezi, masta alikuwa akiongea na mtu na kumwambia anavutiwa na nidhamu yangu kwa kuwa nilikuwa najituma na aliamini nitakuwa bondia mzuri.

Ilikuaje akapewa mapambano?

“Baada ya hapo nilianza kupewa mapambano madogo hadi nilipofahamiana na Kocha Rahabu Mhamila ‘Super D’ aliyekuwa na gym yake pale Ashanti United ila baada ya muda akaungana na Masta Kinyogoli,” anasema na kuongeza walikuwa wanampa mapambano madogo kwa ajili ya kumjenga.

Pambano la kwanza lilikuaje?

“Pambano langu la kwanza kubwa lilikuwa dhidi ya Yonas Segu mwaka 2021 na wakati huo alikuwa ametoka kumpiga bondia wa Morogoro Sana Temba.

“Pambano letu lilifanyika Friends Corner, Manzese halafu lilikuwa na ushindani mkubwa ila kwa uwezo wa Mungu nikampiga kisha nikaletewa bondia ambaye alikuwa mkali na maarufu wa Tanga, Said Mundu tena akiwa hajapigwa hata pambano moja, nikampiga.

“Nikapewa pambano lingine na bondia Amosi Mwamakula na marehemu Thomas Mashali alinifuata na kuniahidi Sh200,000 kama nitampiga na nilimpiga.

Vipi mapambano ya nje ya nchi?

“Niliendelea vizuri hadi nilipoenda Zambia kwa mara ya kwanza kushinda mkanda wa WBF kwa KO ya raundi ya tisa dhidi ya bondia wao anaitwa Kavinga.

Jambo gani limekufanya uchelewe kufahamika?

“Nadhani kwanza pengine wakati haukuwa sahihi, pia sasa hivi mambo yamebadilika kwa sababu wakati ule tulikuwa tunategemea sana magazeti na kama kwenye runinga basi ilikuwa ni ITV kupitia Tamasha la michezo.

“Lakini Azam kwa sasa imechangia mabadiliko makubwa sana kwa sababu watu karibu nchi nzima wanaona tunachofanya, siyo kama zamani hivyo imetusaidia kufahamika pakubwa maana hakuna sehemu ambayo sijulikani.

Pesa yako ya kwanza kubwa ulilipwa kiasi gani?

“Wakati nacheza yale mapambano madogo sijawahi kulipwa ila kuna pambano moja Masta Kinyogoli alinipa Sh20,000 tena kwa siri watu wasione kwa kuwa alikusanya viingilio.

“Kutoka hapo ndiyo nilijua ngumi kumbe ina pesa japokuwa ile nilienda kugawa mtaa mzima kwa watoto wadogo na hadi leo rafiki zangu wengi ni watoto wadogo, ila niliona pesa nyingi kwa sababu sikutegemea kama ningepewa.

“Halafu kuna pambano lingine liliandaliwa Tabata na mzee wangu mmoja anaitwa Matimbwa, tulikubaliana kugawana viingilio ila kwa bahati mbaya nilipata Sh500 lakini sikuchukulia kwa ubaya maana pambano lenyewe nilishinda.

“Lakini pesa kubwa kupata nilivyoenda nje kwa mara kwanza nililipwa Dola 1500 baada ya kurudi na kuichenji, baadhi niligawa kwa Masta na mama yangu halafu nikaficha 600,000 nikaenda kununua kiwanja Mbezi na ndiyo naishi sasa.

Ulisema baba yako aliwatelekeza, hakukutafuta tena?

“Wakati napigana nilikuwa sijui hata umri wangu ni upi ila nakumbuka baada ya kupigana na Koos Sibiya katika pambano ambalo lilikuwa la kwanza kuonyeshwa na Azam wakati ule wa Waziri Dk Harrison Mwakyembe pale Uwanja wa Uhuru, nilipigiwa simu na mtu akijitambulisha kama ndiye baba yangu na alidai namba alipewa na Waziri Mwakyembe ila nilimkataa na niliwahi kumtumia ujumbe tusijuane.

“Wakati fulani alikuwa anakuja Dar na nilikuwa nakwepa kuonana naye, akawa anaonana na mdogo wangu, marehemu Oswald kabla mara ya mwisho kukutana naye msibani baada ya kulazimishwa yeye kuja kumzika mwanaye.

Ilikuwaje alipofika Marekani?

“Binafsi nilikuwa na hamu ya kwenda Marekani. Kulikuwa na promota anachukua mabondia wengi kutoka Afrika. Aliongea na Chaurembo Palasa ili twende kule kupigana na tulienda na malengo yangu yalikuwa sio kurudi tena kuishi Bongo.

“Akili na mawazo vilijua naenda kuishi maisha mazuri na nitajikita kwenye ngumi kama ilivyokuwa dhamira yangu na nitakuwa tajiri.

“Baada ya kufika tulipekwa sehemu walikokuwa wakikusanya watu , yaani kwa huyo promota na tulikutana mabondia kutoka sehemu tofauti ikiwamo Tanzania.

Mambo yalikuaje huko?

“Mazingira yalinishangaza maana kulala ikifika usiku tunapewa magodoro ya kutandika chini, tofauti na nilivyofikiria akilini na nilimuuliza Chaurembo Palasa tutaishi hapa? Lakini Hata yeye alidhani ilikuwa kwa mara moja tu na tuliuliza Watanzania wengine na bondia Fabian Lyimo aliniita pembeni na kunieleza yale ndiyo mazingira ya kuishi na hatutapelekwa sehemu nyingine kama tulivyofikiria sisi.

“Alinieleza hakuna hata gym ambayo nitapelekwa zaidi labda kutafutiwa kibarua. Mazoezi ilikuwa unafanya popote unapopata nafasi. Kiukweli hilo jambo lilikuwa gumu na nilimwambia nimekuja huku kucheza ngumi siyo kufanya kazi.

“Muda pale wa kukaa ukawa unaenda bila ya kupigana na kula yetu tulikuwa tunategemea yule jamaa arudi na nyama zilizokaa sana kwenye Supermarket ndio ziletwe zipikwe ili tule wote pale katika jungu kubwa.

Walivyomtoroka promota

“Kutokana na kukaa sana yule promota alimtafutia kazi Palasa ila ajabu waliokuwa wakifanya hiyo kazi kila wakirudi walilalamika kuumwa migongo.

“Palasa baada ya kuona vile akaniambia hawezi kwenda kufanya hizo kazi hasa kutokana na umri wake ni sawa na kujitafutia kifo na alitafutiwa vitambulisho feki ili akafanye kazi.

“Wakati huo likapatikana pambano na nilitakiwa nipoteze. Lilikuwa la Dola 4000, huku yule promota anasubiri pesa yake ya tiketi za ndege.

“Binafsi sikuwa tayari kucheza lile pambano, niligoma kwa kumwambia Palasa sikuja huku kufanya biashara ya kuuza mapambano, nimekuja kupigana na nilitaka kucheza raundi 10 na iwe mechi ya ubingwa.

“Wakati hayo yakiendelea tayari nilishapanga kutoroka bila ya kumwambia Palasa na kama angeenda kufanya kazi basi asingenikuta ila bahati nzuri naye akagoma.

“Aliniambia kuna watu aliongea nao, wakaja kutuchukua alfajiri kwa kutoroka ingawa mlinzi alimpigia simu promota lakini hakutupata. Tulifika Texas na tuliishi kwa miezi miwili, tukahamia Wichita tulikokutana na makocha wa Mexico.

Alivyowachapa Wamexico, apigwa Sauzi

“Makocha wale waliomba wanione na kunifanyia majaribio na waliniletea mabondia wawili wa Mexico na wote niliwapiga, nikaombewa gym pale kwa mwezi niwe nalipa Dola 50 ila baada ya kupita wiki wakaniombe kufanya bure kutokana na juhudi zangu.

“Nashukuru Mungu baada ya muda wakanitafutia mechi Afrika Kusini na Azinga Fuzile, nilienda na Palasa na kwenye mechi nilicheza vizuri ingawa wale jamaa walimfanyia uhuni kwenye maji kwa kumwekea dawa zilizonifanya nisione nikapigwa kwa TKO.

“Lakini baada ya pambano nikawa nataka kurejea Marekani kwa bahati mbaya nilifanyiwa hujuma nikaachwa na ndege ikabidi nikate tena tiketi kwa pesa yangu kurudi Marekani na palasa aligoma na kurejea Bongo.

Apata ajira, apanga chumba, maisha yalikuaje?

“Nilivyofika Marekani, meneja wa kwanza alikuwa ameripoti tumepotea, ila niliwaelewesha maofisa wa uhamiaji na nikaruhusiwa kuingia tena.

“Nilirejea nikiwa na pesa na hivyo nikapanga wakati huo nikawa nafanya mazoezi na kazi ya kumsaidia mwenyeji wangu ingawa kazi hazikueleweka mara kubeba wagonjwa na ujenzi. Kuna wakati hatukuwa na maelewano mazuri ndiyo maana nikarudi Bongo, pesa pia ilikuwa inakaribia kuisha.”

Vyakula gani huwa unatumia?

“Binafsi huwa nafuata mpangilio wa daktari wangu wa lishe pamoja na mwalimu wangu, huwa ndiyo wanajua chakula gani napaswa kula.

“Mara nyingi ratiba ya chakula kwa siku hasa nikiwa kwenye maandalizi ya pambano huwa nakula mara tano, mimi siwezi kula nyama nyekundu, nakula kuku na samaki.

“Lakini kawaida kama kuku basi mzima nakula peke yangu, tena wale wa kienyeji, hivyo hata nyumbani kwangu wenyewe wanajua kama kuku akiwepo basi mmoja pekee nakula peke yangu.

Pambano gani kwako limebaki kwenye kumbukumbu?

“Binafsi kwangu hata pambano likiwa gumu huwa naligeuza kuwa rahisi ndani ya ulingo, lakini pambano ambalo sitoweza kulisahau ni lile nililocheza na bondia wa Mexico ambaye alizimia kwa kipigo pale Mlimani City.

“Unajua lile pambano lilikuwa gumu kwa sababu nilikuwa nimetoka kuumwa na mazoezi nikafanya kwa siku nne pekee tena ya kukata uzito lakini nilishinda.

Malipo ya mapambo ya ndani kuwa makubwa, yanamekunufaisha kiasi gani?

“Nimenufaika pakubwa na nisiwe muongo sasa hivi nabadilisha gari kila mwaka, maisha yangu yamekuwa tofauti na nilipotokea, namiliki magari matatu, la kwanza lilikuwa Passo kisha nikawa na Toyota Belta na sasa natumia Nissan Duals.

“Lakini ukiondoa hapo nashukuru Mungu nimewekeza kwa kununua maeneo sita na nimeanza ujenzi wa nyumba za kupangisha,” anasema Class.

Chanzo: Mwanaspoti