Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hii ndio siku Mike Tyson aliyowatoa machozi wapenzi wa Masumbwi

Tyson Lost To Kevin McBride Bondia Mike Tyson

Tue, 7 Mar 2023 Chanzo: Luqman Maloto

Ilikuwa Juni 11, 2005. Mike Tyson alipanda ulingoni, MCI Centre, Washington. Kilikuwa kipute dhidi ya Kevin McBride wa Ireland.

Simba aliyelala hawi paka. Tyson alikuwa ameshapoteza mapambano matano. Hata hivyo, hakuna aliyemtabiria McBride ushindi.

Pambano lilianza. Tyson alikuwa vizuri raundi ya kwanza mpaka ya tano. Kufika ya sita, Tyson akawa hoi. Akalambishwa sakafu. Kengele ikalia. Mapumziko.

Raundi ya saba, Tyson aliomba poo. Alishindwa kuendelea. Inaitwa retired (RTD). McBride akashinda kwa TKO. Ushindi mkubwa zaidi katika career yake.

Baada ya pambano, mtangazaji Jim Gray, alimuuliza Tyson kama alitamani kuendelea na mchezo?

Tyson akajibu:

“Nilipenda niendelee, ila nilipoanza kupigwa nikaona siwezi.” Nina uwezo wa kubaki kwenye umbo zuri, lakini sina ujasiri tena wa kupambana. Naomba msamaha nimemwangusha kila mtu. Huu mchezo haupo tena moyoni. “Napigana kwa ajili ya kukabili bili zangu. Nawazingatia zaidi watoto wangu. Sina tena ile sura ya kutisha. Mimi sio mnyama tena.”

Gray akamuuliza:

“Maneno yako yanamaanisha hutapigana tena?”

Tyson: “Sitapigana tena. Sitaki kuendelea kuukosea heshima huu mchezo kwa kupoteza dhidi ya aina hii ya mabondia.”

Kingine, Tyson alisema hakuupenda mchezo wa Boxing tangu mwaka 1990. Hivyo, kipindi chote alikuwa anajilazimisha kupigana ili apate pesa.

Arena yote ilikuwa kimya. Binadamu aliyepata kuitwa “The Baddest Man On The Planet”, alitamka mwenyewe kuwa hakuwa tishio tena.

Kweli, Tyson hakurudi tena kwenye ulingo wa professional boxing. Aliilinda heshima. Akaacha masumbwi.

Kuna waliolia. Mtu mbaya kwenye sayari, aliyepiga watu atakavyo ulingoni, aligeuka mchovu. Naye alikiri. Maneno ya Tyson yalishawishi machozi ya kila aliyemwona kwenye prime yake na jinsi alivyoishia.

Yes, Februari 11, 1990, Tyson alipigwa na Buster Douglas. Lilikuwa pambano la kwanza Tyson kupigwa. Tyson alipaswa kushinda raundi ya 8. Refa alirefusha hesabu Douglas akiwa chini.

Kuanzia hapo Tyson aliamini alishindwa kwa mizengwe. Hakupenda tena Boxing. Alipanda ulingoni kutafuta pesa aishi vizuri. Mahaba na mchezo yalikufa kabisa.

Chanzo: Luqman Maloto