Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hassan Mwakinyo asogea viwango vya Ubora

Mwakinyo 1 Bondia mtanzania, Hassan Mwakinyo

Thu, 24 Feb 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Licha ya kutoonekana ulingoni kwa zaidi ya miezi mitano, pointi na rekodi yake ya nyuma ulingoni ‘imembeba’ bondia Hassan Mwakinyo kwenye viwango vipya vilivyotolewa na mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (Boxrec).

Mwakinyo amepanda kwa nafasi moja kutoka ya 15 hadi ya 14 kwenye viwango hivyo katika uzani wa super welter duniani kati ya mabondia 1,778 huku akiendelea kusalia kwenye nafasi ya kwanza Afrika.

Kwa mujibu wa Boxrec, Mwakinyo ndiye bondia pekee Afrika aliyeingia 15 bora ya dunia katika uzani wa super welter unaoongozwa na Jermell Charlo wa Marekani, Brian Carlos Castano wa Argentina na Tim Tszyu wa Australia.

Tangu alipomchapa kwa Technical Knock Out (TKO) ya raundi ya nne Julius Indongo kwenye pambano la Septemba 3, mwaka jana, Mwakinyo hajaonekana ulingoni hivyo kusababisha kuporomoka kutoka nafasi ya 10 aliyokuwa awali hadi ya 15 kabla ya jana kupanda kwa nafasi moja.

Katika mahojiano na gazeti hili hivi karibuni bondia huyo alisema kuporomoka kwake hakujamuumiza kwa kuwa ameporomoka bila kupigwa. “Kama ningeporomoka kwa kupigwa ingeniumiza mno, lakini nimeshuka kutokana na matokeo ya mabondia wengine wanaocheza huko duniani, ila naamini nitapanda mara dufu nitakapoanza kucheza,” alisema Mwakinyo hivi karibuni kabla ya jana kupanda kwa nafasi moja matokeo anayosema hajaridhika nayo kwani lengo lake ni kuwa namba moja wa dunia.

Hata hivyo kama hatopata nafasi hivi karibuni ya kucheza na kushinda kuna uwezekano wa bondia huyo akaporomoka tena kutokana na pointi za mabondia watatu walio chini yake hivi sasa kama watacheza na kushinda.

Mabondia hao ni Austin Trout na Jesus Alejandro Ramos wa Marekani wenye pointi 20.39 na 19.75 na Dennis Hogan wa Australia mwenye pointi 19.80.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz