Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hamasa ya ngumi iendane na kipato kwa mabondia

Ibrahim Class.png Bondia wa ngumi za kulipwa nchini Tanzania, Ibrahim Class

Mon, 30 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hamasa kwenye ngumi za kulipwa nchini kwa miaka ya karibuni imeongezeka, ukiachana na mapromota tuliozoea kuwaona wakiandaa mapambano makubwa kama Ally Mwazoa, Jay Msangi, Shomari Kimbau, Kaike Siraju, mzee Kyando ‘Don King’ na wengine wengi, hivi sasa mapromota wapya wengi wanajitokeza kuwekeza kwenye mchezo huo.

Tunafahamu, ngumi za kulipwa ni biashara, ni mchezo wa nipe nikupe, bondia atasaini mkataba kabla ya pambano, akipigwa au akishinda pesa yake iko pale pale na kila upande una dau lake kulingana na renki na rekodi za bondia husika, japokuwa kuna adhabu ya kutolipwa au kupunguziwa malipo kama ukionekana umepanga matokeo kwa kujiangusha.

Hapa nchini baada ya soka, ngumi hasa za kulipwa huenda ndiyo ukawa mchezo unaofuatia kwa kuwa na mashabiki wengi, ile dhana ya kwamba ngumi ni uhuni sasa imetoweka, mabondia wanauchukulia ni kazi ya kuwaingizia kipato.

Hata mashabiki wake, sio tena wale wa oya oya kama ilivyokuwa imezoeleka miaka ya nyuma, japo wa aina hiyo wapo na ndiyo wenye ngumi zao, lakini nao wamebadilika kulingana na mazingira yaliyopo sasa.

Jitihada zimefanyika leo hii tunashuhudia mapambano yanachezwa kwenye mazingira rafiki kwa shabiki wa rika na jinsia zote kushuhudia hata ukiwa na familia yako ukumbini, tofauti na miaka 15 iliyopita, shabiki ukienda kwenye ngumi lazima ujikoki haswa ili kukabiliana na lolote liwe la heri au shari.

Huu ni moja ya mifano michache niliyowahi kuishuhudia kwenye ngumi za kulipwa, katika moja ya pambano lililowakutanisha mabondia wakubwa nchini, baada ya matokeo kutangazwa vurugu zikaanza, kila shabiki ilibidi ashike njia yake kujinusuru kuumizwa kwa chupa zilizokuwa zikirushwa ukumbini siku hiyo, binafsi nililazimika kukimbia kwa umbali kama mita 700 hivi ili kujinusuru tena ikiwa ni usiku mkubwa.

Usalama wa shabiki ulikuwa ni finyu kwenye mapambano mengi, jambo ambalo ilisababisha wapenzi wengi wa mchezo huo kuzipa kisogo na kuuona ni mchezo wa watu fulani, hiyo ilikuwa ni kabla ya mambo kuanza kubadilika.

Kuna mapromota wametengeneza njia kwenye mchezo huo, ambao sasa wenzao wanaendelea kunyoosha pale palipokuwa pamepinda ili kufikia kwenye kilele cha mafanikio katika mchezo huo.

Miaka ya kuanzia 2010 mambo yalianza kurudi kwenye mstari ikiwamo Hall of Fame kuwaleta mabondia wakubwa nchini, akiwamo nyota wa zamani wa dunia, Frans Botha na wengineo, taratibu ile hamasa ya mchezo wa ndondi ikaanza kurudi.

Serikali baada ya Dk Harrison Mwakyembe kukabidhiwa kijiti cha kuwa waziri wa michezo pia ilipoamuakuziondoa ngumi kwenye mfumo wa vyama vingi na kuundwa kwa Kamisheni moja ya TPBRC kuusimamia mchezo huo, ilisaidia kuleta utulivu na kuwavutia mapromota wengine wapya kama kina Jackson Group ambao walimleta Kubrat Pulev mmoja wa mabondia wakubwa wa uzani wa juu duniani, pia mapromota wengine wapya wameendelea kuongezeka.

Hamasa imeendeea kuongezeka kila siku, ngumi zinapendwa na watu wengi wa rika tofauti wake kwa waume, kampuni mbalimbali zinajitokeza kuandaa mapambano.

Nakumbuka katika moja ya ‘interview’ zangu na rais wa TPBRC, Chaurembo Palasa aliwahi kuniambia, ndoto yake kadri siku zinavyosonga ni ngumi ziwe zinapigwa hata kwenye kumbi tatu au nne tofauti kwa siku moja kama tunavyoona kwenye soka, mechi mbili hadi tatu za Ligi zinachezwa siku moja kwenye viwanja tofauti.

Huo ni mpango mzuri kuendelea kuongeza hamasa kwenye ngumi nchini, lakini wakati hayo yakifanyika, hamasa hiyo iendane na malipo mazuri kwa walengwa ambao ni mabondia.

Ifikie mahali yale mapambano ya Sh 100,000 hadi 30,000 yabaki historia hata kama ngumi za kulipwa ni biashara, lakini biashara hiyo iwe ya kubadili kwa namna moja au nyingine maisha ya mabondia wetu kwa kupata mapato mazuri.

Umaarufu wa mabondia wetu uendane na vipato vyao, bahati nzuri TPBRC imeweka bei elekezi ya pambano kulingana na renki ya bondia, japo sio sheria, lakini bado kuna haja ya vipato vya mabondia kwenye pambano kuboreshwa kulingana na mazingira ya sasa.

Kwa mujibu wa Palasa, nikimnukuu anasema: “katika mikataba ya ngumi, bondia anapopata madhara uligoni hilo ni jukumu lake binafsi halimhusu promota.”

Jambo ambalo kwa namna moja au nyingine kuna haja ya kuwa na bima, lakini pia mabondia kuwa na watu wa kuwasimamia ili wanufaike na jasho lao, majina waliyoyatengeneza kwenye ndondi yaendane na kipato chao, zile ngumi za oya oya zibaki historia.

Ngumi za sasa ni za watu wote, zina mashabiki na kampuni nyingi zinaingia kuandaa mapambano, kinachohitajika ni mapromota wapya na wazamani kuwa na uwezo wa kuandaa mapambano na kuwalipa mabondia vizuri ili ushindani uzidi kuongezeka, ushindani ukiongezeka na hamasa itakuwa kubwa zaidi.

Tanzania itapiga hatua kwenye ngumi, mabondia wetu wataanza kusogea kwenye renki nzuri kidunia na kupanua soko la ngumi zetu katika anga za kimataifa na tukijaliwa siku moja mabondia wetu watafika kwenye levo ya kuwania mikanda mikubwa ya ngumi kama WBC, WBA na WBO, hakuna kinachoshindikana.

Chanzo: Mwanaspoti