Rashid Matumla alizibariki sana ngumi za kulipwa enzi hizo kwa namna alivyotutoa kimasomaso katika mapambano mbalimbali ya kimataifa.
Jamaa alikuwa anajua kupiga ngumi na wapinzani walikiona cha moto mbele yake kutokana na jinsi alivyowatandika.
Jambo ambalo Rashid Matumla alikuwa akitufurahisha zaidi ni namna alivyoweza kumaliza mapambano mengi kabla hayajamalizika kwa maana ya ‘Knock Out’ (KO).
Sio aina ya bondia ambaye alikuwa anategemea sana ushindi wa pointi na ikitokea hivyo basi ilikuwa mara chache sana lakini mara kwa mara aliwapunja watu viingilio vyao kwa kutomfikisha mtu raundi ya 10 au 12.
Haikutokea kwa bahati mbaya Rashid Matumla kuwapasua watu wengi kwa KO bali ilikuwa ni matokeo ya nidhamu, kujituma, kujitunza na kufuata vyema ushauri wa makocha wake wakati wa maandalizi na ule wa pambano.
Na hiyo ndio siri ya mafanikio kwa mwanamichezo yeyote na hakuna kingine kwani kadri mtu anavyofanyia kitu mazoezi ndipo anapokuwa na ubora wa hali ya juu ya kukifanya.
Kwa bahati mbaya nyakati za sasa zimetunyima mabondia kama Rashid Matumla ambao wanaweza kutupa ladha ya kupiga KO na badala yake wengi wanategemea ushindi wa pointi tena baadhi ni hadi waokolewe na huruma ya majaji kwa kupewa ushindi au pointi wasizostahili.